Aug 04, 2025 02:18 UTC
  • Jumatatu, 04 Agosti, 2025

Leo ni Jumatatu 10 Mfunguo Tano Safar 1447 Hijria, mwafaka na tarehe 4 Agosti 2025.

Siku kama ya leo miaka 1118 iliyopita, alifariki dunia msomi mashuhuri wa Iran, Abul-Fadhl Bal'ami.

Bal'ami alikuwa mtu wa Bukhara, moja ya miji maarufu ya nchi ya Uzbekistan ya leo. Alijulikana kwa jina la Bal'ami kutokana na mmoja wa mababu zake kuishi mji wa Bal'am huko Asia ya Kati. Abul-Fadhl Bal'ami alikuwa waziri mwenye hekima na msomi mkubwa enzi za utawala wa Wasamani na aliandika vitabu mbalimbali.

Kitabu cha tarjama ya ‘Taarikh Tabari’ ni moja ya vitabu vinavyonasibishwa kwa msomi huyo na kilichopata umashuhuri katika karne ya nne Hijiria. Kitabu kingine maarufu cha msomi huyo ni ‘Taarikh Bal'am’ ambapo ameashiria masuala mbalimbali ya historia.

Miaka 233 iliyopita alizaliwa Percy Bysshe Shelley malenga wa Uingereza.

Percy alianza kupenda taaluma ya fasihi tangu utotoni na kuonyesha kipawa kikubwa katika uwanja huo. Alikuwa mfuasi na muungaji mkono wa thamani za upendo, urafiki na uhuru na sababu hiyo ndiyo iliyomfanya avutiwe na Mapinduzi ya Ufaransa ambayo ndio kwanza yalikuwa yametokea. 

Percy Bysshe Shelley aliaga dunia mwaka 1822 akiwa na umri wa miaka 30 baada ya boti yake kuzama katika Bahari ya Mediterrania. 

Miaka 220 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa William Rowan Hamilton mwanahisabati na mtaalamu wa elimu ya fizikia wa Ireland. 

Alikuwa na kipaji cha hali ya juu kiasi kwamba akiwa na umri wa miaka 13 alikuwa amejifunza lugha 12 za dunia zikiwemo Kiarabu na Kifarsi. William Rowan Hamilton talivutiwa sana na elimu za fizikia na hisabati na alifanikiwa kuanzisha baadhi ya kanuni na mifumo muhimu katika elimu hizo. Akiwa na umri wa miaka 22 Hamilton alikuwa tayari mwalimu wa elimu ya nujumu. Msomi huyo aliaga dunia 1865.

Katika siku kama ya leo miaka 150 iliyopita, aliaga dunia Hans Christian Andersen mwandishi wa vitabu vya watoto wa nchini Denmark.

Alizaliwa mwaka 1805 na tangu akiwa mdogo alikuwa na mapenzi makubwa na visa. Baada ya kuaga dunia baba yake, Hans Christian Andersen akiwa na umri wa miaka 11 aliacha shule na kuanza kufanya kazi. Baada ya kuingia katika maonyesho na michezo ya kuigiza ya kifalme, hali yake ya maisha iliboreka na hivyo akaamua kuendelea na masomo.

Mwandishi huyo wa Kidenmark awali alianza kujihusisha na utungaji mashairi na kuandika visa na simulizi. Hata hivyo baadaye Andersen aliondokea kuwa na mapenzi makubwa na visa vya watoto na alionyesha kipaji kikubwa alichokuwa nacho katika uwanja huo. 

Siku kama ya leo miaka 103 iliyopita, vikosi vilivyokuwa na mrengo wa utaifa nchini Uturuki vikiongozwa na Mustafa Kemal Ataturk vilianza kuwashambulia wanajeshi wa Ugiriki waliokuwa wameikalia kwa mabavu nchi hiyo.

Baada ya kusambaratika utawala wa Othmania katika Vita vya Kwanza vya Dunia, ardhi asili ya utawala huo yaani Uturuki iliangukia mikononi mwa tawala waitifaki.   

Ataturk na mke wake

Katika siku kama ya leo miaka 95 iliyopita, alizaliwa Ayatullah Sayyid Ali Sistani faqihi, alimu na marjaa taqlidi wa Kislamu katika mji wa Mash'had, Iran.  

Alianza kujifunza Qur'ani akiwa na miaka 5, na akiwa na umri wa miaka 11 alianza kusoma masomo ya kidini ya utangulizi baada ya kutakiwa na baba yake kufanya hivyo. Baadaye alielekea katika mji wa Qum kwa ajili ya kujiendeleza zaidi kielimu. Ayatullah Sistani alielekea katika Chuo Kikuu cha Kidini mjini Najaf, Iraq hapo baadaye.

Hii leo Ayatullah Ali Sistani si tu kwamba, anahesabiwa kuwa marjaa mkubwa zaidi nchini Iraq bali pia amekuwa na nafasi muhimu katika kuimarisha umoja, mshikamno na utulivu katika nchi hiyo ya Kiarabu.

Siku kama ya leo miaka 61 iliyopita Marekani ilishindwa katika vita vya baharini vilivyozishirikisha meli za kivita za Marekani na Vietnam ya Kaskazini katika Ghuba ya Tonkin inayopatikana kwenye Bahari ya China ya Kusini.

Mikwaruzano hiyo ya kijeshi iliipa Marekani kisingizio cha kuingia vitani moja kwa moja na Vietnam ya Kaskazini. Wakati huo Washington ilikuwa ikiiunga mkono kwa pande zote Vietnam ya Kusini dhidi ya ile ya Kaskazini. Wanajeshi wa Marekani waliingia vitani moja kwa moja kupigana dhidi ya Vietnam ya Kaskazini.