Aug 12, 2025 02:34 UTC
  • Jumanne, Agosti 12, 2025

Leo ni Jumanne tarehe 18 Mfunguo Tano Safar 1447 Hijria inayosadifiana na tarehe 12 Agosti 2025.

Miaka 1410 iliyopita yaani mwaka 37 Hijria, kwa mujibu wa baadhi ya mapokezi, Uwais al Qarani, mmoja wa tabiina watukufu na wafuasi watiifu wa Imam Ali bin Abi Talib (as) aliuawa shahidi katika vita vya Siffin.

Uwais aliishi katika eneo la Qaran huko Yemen na hakufanikiwa kuonana na Mtume (saw) kutokana na kumuuguza mama yake aliyekuwa mgonjwa. Hata hivyo Mtukufu Mtume daima alikuwa akimtaja kwa wema na kumuombea dua Uwais. Baada ya kufariki dunia Mtume (saw), Uwais al Qarani alikuwa miongoni mwa masahaba wa karibu wa Imam Ali bin Abi Talib.

Alipigana katika vita vya Siffin vilivyotokea kati ya jeshi la Imam Ali (as) na Muawiya bin Abi Sufian na akauawa shahidi katika vita hivyo. Haram ya Uwais al-Qarani inapatikana katika mji wa ar-Raqqah, Syria.

Mahali lilipo kaburi la Uwais kabla na baada ya kubomolewa na Daesh

Siku kama ya leo miaka 141 iliyopita alifariki dunia mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu, Allamah Mir Hamid Hussein Mussawi Hindi. Alizaliwa mwaka 1246 Hijria nchini India na kupata elimu katika taaluma za fiqhi, Hadithi, teolojia na elimu nyingine za Kiislamu.

Miir Hamid Hussein alitumia sehemu kubwa ya umri wake kufunza elimu za kidini na kuandika vitabu. Kitabu muhimu zaidi cha Allamah Miir Hussein Hindi ni A'baqaatul Anwar. Vitabu vingine vya msomi huyo wa Kiislamu ni pamoja na Asfarul Anwar na Sham'ul Majalis.   

Allamah Mir Hamid Hussein Mussawi Hindi

Tarehe 12 Agosti mwaka 1949 hati ya makubaliano ya kimataifa ya kuwalinda majeruhi na mateka wa kivita ilipasishwa kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa huko Geneva, Uswisi.

Hati hiyo ilibuniwa kufuatia miamala isiyo ya kibinadamu na jinai zilizokuwa zikifanywa dhidi ya majeruhi na mateka wa kivita wakati wa Vita vya Pili vya Dunia.

Siku kama hii ya leo miaka 48 iliyopita sawa na tarehe 12 Agosti 1976, kambi ya wakimbizi wa Palestina ya Tel al Zaatar iliyoko karibu na Beirut mji mkuu wa Lebanon, ilitekwa baada ya kuzingirwa kwa muda mrefu na wanamgambo wa Kimaroni wa nchi hiyo na wakazi wake wakauawa kwa umati.

Kambi hiyo ilikuwa ikiwahifadhi maelfu ya wakimbizi wa Palestina na ilianza kuzingirwa mwanzoni mwa mwaka 1976 kwa uungaji mkono na uingiliaji wa utawala wa Kizayuni wa Israel. Utawala wa Kizayuni ulifanya hivyo kwa lengo la kushadidisha vita vya ndani huko Lebanon.

Mauaji ya Wapalestina Tel al Zaatar

Na miaka 26 iliyopita, Umoja wa Mataifa uliitangaza Agosti 12 kila mwaka, kuwa ‘Siku ya Vijana Duniani’ ili kueleza umuhimu wa vijana katika dunia ya sasa.

Tabaka hili lenye utanashati la jamii ndiyo sababu ya maendeleo ya kila nchi kwa msingi huo vijana katika kila nchi wanapaswa kupewa umuhimu mkubwa. Kutokana na umuhimu wao vijana wanapaswa kulindwa na kusaidiwa na serikali hususan katika masuala ya ajira, makazi na kujenga familia.

Katika upande mwingine kizazi cha leo cha vijana kinakabiliwa na changamoto nyingi za kimwili na kiroho ikiwa ni pamoja na ongezeko la matumizi ya dawa za kulevya, magonjwa ya kuambukiza kama Ukimwi na virusi vya HIV, intaneti na michezo ya computa ambayo inawatumbukiza vijana wengi katika ufuska na utovu wa maadili.

Kutangazwa Siku ya Vijana Duniani kunaweza kusaidia juhudi za kuwakumbusha vijana umuhimu wao na kuzuia changamoto mbalimbalizinazolikabili tabaka hilo muhimu.