Aug 18, 2025 11:02 UTC
  • Jumatatu tarehe 18 Agosti 2025

Leo ni Jumatatu tarehe 24 Safar 1447 Hijria sawa na Agosti 18 mwaka 2025.

Katika siku kama ya leo miaka 1062 iliyopita Sahib bin Abbad, mwanafasihi maarufu na msomi wa Kiislamu wa kizazi cha Dailami alifariki dunia.

Sahib alikuwa mwandishi hodari na mtu mwenye hadhi na mashuhuri sana katika zama zake. Licha ya kwamba alikuwa waziri katika serikali ya kizazi cha Dailami, lakini alikuwa mtu mnyenyekevu na mwema kwa watu wa chini yake.

Sahib bin Ubbad ameandika vitabu vingi, na maarufu zaidi ni kile cha "al Muhiit" chenye juzuu saba.   ****

Alipozikwa  Sahib bin Abbad katika mji wa Isfahan

 

Siku kama ya leo miaka 1372 iliyopita, vilitokea vita vya Ajnadeen katika eneo la Ajnadeen huko Palestina kati ya Waislamu na Warumi. Katika vita hivyo ambavyo havikuwa na mlingano hasa kwa kuzingatia kuwa, askari wa Kirumi walikuwa wengi mara kadhaa kuliko Waislamu, jeshi la Waislamu liliibuka na ushindi mkubwa kutokana na wapiganaji wake kuwa na irada na imani thabiti. Baada ya Warumi kushindwa vibaya na Waislamu waliamua kurejea nyuma hadi katika mpaka wa Palestina na Syria sambamba na kupoteza maeneo mengi yaliyokuwa chini ya udhibiti wao. ***

 

Siku kama ya leo miaka 61 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 18 Agosti 1964, Afrika Kusini ilipigwa marufuku kushiriki kwenye mashindano ya 18 ya Olimpiki yaliyofanyika Tokyo Japan, baada ya kukataa kulaani vitendo vyake vya ubaguzi wa rangi dhidi ya wazalendo weusi nchini humo. Uamuzi huo ulichukuliwa na Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC) baada ya kumaliza kikao chake huko Lausanne Uswisi. Ujumbe wa Afrika Kusini ulisusia kikao hicho.   ***

Mnamo tarehe 18 Agosti mwaka 1977, mwanaharakati wa kupinga ubaguzi wa rangi wa Afrika Kusini Steve Biko alikamatwa na utawala wa ubaguzii wa rangi. Biko alikamatwa baada ya kusimamishwa kwenye kizuizi cha barabarani akiwa na Peter Jones, walipokuwa wakisafiri kwenda Cape Town. Steve Biko alifariki dunia akiwa chini ya ulinzi wa polisi mnamo Septemba 12, 1977, kutokana na majeraha aliyopata wakati wa kuhojiwa.

Biko, aliyekuwa mwanaharakati mashuhuri wa kupinga ubaguzi wa rangi na kiongozi wa Black Consciousness Movement, aliwahi kuzuiliwa na kuwekewa vikwazo na serikali ya ubaguzi wa rangi mara kadhaa. 

Kukamatwa huko na baadaye kifo chake, viliibua hasira na kulaaniwa kimataifa.