Alkhamisi, Agosti 21, 2025
Leo ni Alkhamisi tarehe 27 Mfunguo Tano Safar 1447 Hijria, mwafaka na tarehe 21 Agosti 2025.
Leo tarehe 30 Mordad kwa kalenda ya Kiirani ni siku ya kumbukumbu ya Allamah Muhammad Baqir Majlisi, alimu na mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu.
Allama Majlisi ndiye mwandishi wa kitabu muhimu na mashuhuri cha Bihar al-Anwar. Alionyesha kipaji kikubwa katika masuala ya elimu tangu akiwa mdogo wakati huo akiwa chini ya malenzi na mafundisho ya baba yake. Baba yake alikuwa mwanazuoni, msomi na mchamungu. Alipofikisha umri wa miaka 14 alipata idhini kutoka kwa Mulla Sadra, mwanafalsafa mkubwa wa Ulimwengu wa Kiislamu ya kupokea na kunakili Hadithi.
Alllamah Majlisi alikuwa mmoja wa maulamaa wa Kiislamu waliokuwa na taathira chanya na muhimu katika harakati za kisiasa na kijamii katika kipindi cha utawala wa ukoo wa Safavi. Nafasi na daraja ya kielimu aliyokuwa nayo Allamah Majlisi mbele ya matabaka mbalimbali ya watu ilimfanya mtawala Shah Suleiman Safavi ampatie cheo cha Sheikh al-Islam.
Allamah Majlisi ameandika vitabu vingi, lakini kitabu chake mashuhuri zaidi ni Bihar al-Anwar. Kitabu hiki ni Dairatul Maarif yaani Ensaiklopidia kubwa ya Hadithi ambayo imekusanya masuala yote ya kidini, kihistoria, fikihi, itikadi, tafsiri ya Qur'ani na kadhalika. Kitabu hiki kina zaidi ya hadithi 85,000 zilizonukuliwa kutoka kwa Bwana Mtume (saw) na Ahlul-Baiti wake watoharifu (as).
Ilimchukua Allamah Majlisi miaka zaidi ya 30 kuandika kitabu hiki. Kundi la wanafunzi wa Allamah Majlisi wakiwa chini ya usimamizi wake walikuwa na nafasi muhimu kkatika kuandika na kupatikana kitabu hiki.

Siku kama ya leo miaka 66 iliyopita, iliasisiwa The Central Treaty Organization ambayo ilikuwa ikijulikana kwa jina la Cento na kuchukua nafasi ya mkataba wa Baghdad.
Taasisi hiyo iliundwa na Iran, Uturuki, Pakistan na Uingereza mjini Ankara Uturuki. Pamoja na kuwa Marekani haikuwa mwanachama rasmi wa Taasisi ya Cento na ilishiriki kwenye vikao vya jumuiya hiyo kama mtazamaji tu, lakini ilikuwa na nafasi kuu katika maamuzi yote ya taasisi hiyo.
The Central Treaty Organization ilivunjika baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na kujiondoa nchi hiyo katika mkataba huo mwaka 1979.

Tarehe 21 Agosti mwaka 1965 yaani katika siku kama hii ya leo miaka 60 iliyopita Wamarekani wenye asili ya Afrika katika mji wa Alabama walifanya maandamano wakitaka kutekelezwa sheria ya haki ya kupiga kura.
Maandamano hayo yalizidisha harakati ya vuguvugu la kupigania haki za kijamii za Wamarekani weusi. Harakati hiyo ilianza mwaka 1955 kwa lengo la kupigania usawa kati ya Wamarekani weusi na wazungu na ilimalizika mwaka 1968 baada ya kupasishwa sheria ya haki za kiraia.

Siku kama ya leo miaka 56 iliyopita, inayosadifiana na 21 Agosti 1969, Masjidul Aqsa Kibla cha Kwanza cha Waislamu, kilichomwa moto na Wazayuni.
Katika tukio hilo, eneo hilo takatifu na la kihistoria liliharibika vibaya sana. Utawala wa Kizayuni wa Israel ulidai kuwa, kitendo hicho kilifanywa na mtalii wa Kiaustralia. Utawala huo wa Kizayuni ulitayarisha mahakama ya kimaonyesho tu mjini Tel Aviv na kuchukua uamuzi wa kumuachilia huru mhalifu huyo kwa madai kwamba alikuwa na matatizo ya kiakili.
Baada ya kutokea kitendo hicho, nchi za Kiislamu zilikutana na kuamua kuunda Jumuiya ya Nchi za Kiislamu (OIC).

Miaka 34 iliyopita katika siku kama hii ya leo Latvia ambayo ni miongoni mwa nchi za Baltic huko magharibi mwa Urusi ya zamani ilijitangazia uhuru.
Latvia ilikuwa chini ya satwa ya Urusi ya zamani kufuatia makubaliano ya siri yaliyofikiwa mwaka 1939 Miladia kati ya Hitler na Stalin. Mwaka 1991, karibu asilimia 80 ya wananchi wa Latvia walishiriki kwenye kura ya maoni na kupelekea kutangazwa uhuru wa nchi hiyo katika siku kama hii.

Tarehe 21 Agosti inatambuliwa kama Siku ya Kimataifa ya Msikiti.
Upasishwaji wa siku hii ulijiri mwaka 1382 Hijiria Shamsia, sawa na tarehe 22 Agosti mwaka 2003 katika mkutano uliofanyika mjini Tehran na kwa pendekezo la Shirika la Utamaduni na Mahusiano ya Kiislamu la Iran na kupitishwa na Wizara za Mashauri ya Kigeni za nchi za Kiislamu.
Kikao hicho kilifanyika kwa mnasaba wa wiki ya kumbukumbu ya kuchomwa moto Msikiti wa Al-Aqsa na utawala wa Kizayuni wa Israel tarehe 21 Agosti mwaka 1969. Katika kikao hicho, nchi za Kiislamu zilitakiwa kutoa himaya kwa misikiti kama mahala patakatifu na kuenzi maeneo hayo.
