Jumamosi, 30 Agosti, 2025
Leo ni Jumamosi 6 Mfunguo Sita Rabiul-Awwal 1447 Hijria mwafaka na 30 Agosti 2025.
Siku kama ya leo miaka 155 iliyopita, alizaliwa Ernest Rutherford, mtaalamu mkubwa wa fizikia wa nchini Uingereza maarufu kwa jina la baba wa nishati ya nyuklia. Baada ya kuhitimu masomo yake ya awali eneo alikozaliwa, Ernest alielekea katika mji wa kielimu wa Cambridge na kujiunga na chuo kikuu cha mji huo. Kuanzia mwaka 1919 Rutherford alitokea kuwa mhadhiri mwenye tajriba katika uga wa fizikia chuoni hapo, huku akijiunga na jumuiya ya kifalme ya mjini London hapo mwaka 1903. Mwaka 1904, msomi huyo alisambaza kitabu chake alichokipa jina la ‘Shughuli za Mionzi’. Baadaye Ernest Rutherford aliongoza kundi la utafiti katika chuo kikuu cha Manchester, kundi ambalo haraka liliweza kuandaa nadharia mpya kuhusiana na muundo wa atomiki. Mwaka 1908 Miladia, msomi huyo alitunukiwa zawadi ya Nobel kutokana na shughuli zake hizo na kupata umaarufu mkubwa katika uga huo.

Miaka 118 iliyopita katika siku kama ya leo, kulitiwa saini mkataba mbaya wa kuigawa Iran kati ya Urusi na Uingereza. Mkataba huo ulitiwa saini katika zama za utawala wa Mohammad Ali Shah Qajar. Urusi na Uingereza zilikuwa katika ushindani mkali kwa maslahi yao nchini Iran kwa miaka mingi. Kila upendeleo ambayo nchi moja kati ya hizo mbili ilikuwa ikipata, basi nchi ya pili nayo ilifanya juhudi za kupata kitu kama hicho pia. Hata hivyo, baada ya Mapinduzi ya Kikatiba, makubaliano yalifikiwa ghafla kati ya Urusi na Uingereza, ambapo Iran iligawanywa katika maeneo yenye ushawishi. Kwa mujibu wa makubaliano ya kugawanywa kwa Iran, eneo la kati la nchi lilitangazwa kutoegemea upande wowote. Mikoa ya kaskazini na sehemu ya kanda ya magharibi ya Iran ikawa chini ya udhibiti wa Urusi, na mikoa ya kusini ikawa nyanja ya ushawishi ya Uingereza.

Siku kama ya leo miaka 35 iliyopita, Jamhuri ya Azerbaijan ilitangaza uhuru wake kutoka Urusi ya zamani. Ardhi ya Azerbaijan ilitekwa na kukaliwa kwa mabavu na silsila ya Kiirani ya Wasasani tangu mwanzoni mwa karne ya Tatu Miladia na katika kipindi kikubwa cha historia yake ilikuwa sehemu ya ardhi ya Iran. Vita kati ya Urusi ya zamani na Iran vilijiri mwanzoni mwa karne ya 19 Miladia, kufuatia kupenda kujitanua kwa utawala wa kifalme wa Tsar huko katika Umoja wa Kisovieti. Iran ilipata pigo katika vita hivyo na kupelekea sehemu moja ya ardhi ya kaskazini ya Azerbaijan kukaliwa kwa mabavu na Urusi ya zamani mwaka 1813 kwa mujibu wa mkataba wa Golestan.

Siku kama ya leo miaka 26 iliyopita, wananchi wa Timor ya Mashariki huko kusini mashariki mwa bara Asia walishiriki katika kura ya maoni na kuchagua kujitenga nchi hiyo na Indonesia. Kisiwa cha Timor ya Mashariki sambamba na visiwa vingine vya Indonesia kilivamiwa na kukaliwa kwa mabavu na wakoloni wa Kireno mwaka 1511 Miladia. Timor Mashariki iliunganishwa na Indonesia mwaka 1976.

Tarehe 8 mwezi Shahrivar mwaka1360 Hijria shamsia kwa mujibu wa kalenda ya Iran inayosadifiana na tarehe 30 Agosti mwaka 1981 ni kumbukumbu ya kuuawa shahidi Rais Mohammad Ali Rajaee na Mohammad Javad Bahonar Waziri Mkuu wa wakati huo wa Iran pamoja na wawakilishi wengine wa serikali katika mlipuko uliotokea katika ofisi ya Waziri Mkuu. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran mwaka 1997, zaidi ya raia elfu 17 na maafisa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran waliuawa shahidi na kundi la kigaidi la Munafiqin na vijikundi vingine vya ugaidi. Baada ya kuanzisha hujuma za kigaidi nchini Iran, wanachama wa kundi hilo la kigaidi kwanza walikimbilia Paris na kisha Iraq. Mwaka 1991 na 1992, Saddam, dikteta wa zamani wa Iraqi, aliwatumia mamluki wa Munafiqin kuwakandamiza Wakurdi na kupanga mauaji ya kimbari ya raia hao wa Iraq ambapo maelfu kadhaa ya wanawake na watoto waliuawa kwa umati.
