Sep 01, 2025 07:31 UTC
  • Jumatatu, tarehe Mosi Septemba, 2025

Leo ni Jumatatu tarehe 8 Rabiul Awwal 1447 Hijria sawa na tarehe Mosi Septemba mwaka 2025.

Siku kama ya leo miaka 1,187 iliyopita aliuawa shahidi Imam Hassan Askari (as) ambaye ni mmoja wa wajukuu wa Mtume wetu Muhamamd (saw) katika mji wa Samarra nchini Iraq.

Imam Askari alizaliwa katika mji mtakatifu wa Madina mwaka 232 Hijria na alishika hatamu za kuongoza Umma baada ya kuuawa baba yake mwema Imam Ali al Hadi (as). Kipindi cha uongozi wa Imam Hassan Askari kilijawa na misukosuko mingi kutokana na kuzaliwa ndani yake Imam wa Zama Mahdi (as). Kwani viongozi wa utawala wa kizazi cha Abbas walikuwa wakichunga mno na kumsaka Imam huyo aliyeahidiwa kudhihiri katika aheri zamani.

Alisifika kwa elimu, ukarimu na ucha-Mungu. Imam aliuawa shahidi na watawala madhalimu wa Bani Abbas kwa kupewa sumu katika siku kama hii leo. 

Miaka 851 iliyopita katika siku kama ya leo, ilianza kazi ya kujenga mnara maarufu wa Pisa huko katika mji wa Pisa nchini Italia. Mnara huo ulijengwa kwa ajili ya kuitundika saa juu yake.

Hata hivyo mnara huo uliokuwa na urefu wa mita 55 ulipinda kwa karibu mita tano muda mfupi baada ya kuanza kujengwa. Hitilafu hiyo imeufanya mnara huo ujulikane kwa jina la"Mnara Uliopinda wa Pisa."

Hadi kufikia sasa mnara huo umefanyiwa marekebisho ya kiwango fulani kufuatia juhudi za wahandisi na wataalamu wa nchi mbalimbali.     

Siku kama ya leo miaka 102 iliyopita, mtetemeko mkubwa wa ardhi ulioambatana na uharibifu mkubwa na kuua idadi kubwa ya watu, ulitokea nchini Japan.

Zilzala hiyo iliyokuwa na ukubwa wa 8.3 kwa kipimo cha Rishta iliua watu zaidi ya laki moja na 40 elfu. Mtetemeko huo uliyakumba hata baadhi ya maeneo ya miji ya Tokyo na Yokohama.

Mbali na hasara kubwa zilizosababishwa na mtetemeko huo, idadi kubwa ya Wajapani pia walikosa makazi yao na nyumba nyingi ziliteketea kwa moto. 

Katika siku kama ya leo miaka 86 iliyopita, Vita vya Pili vya Dunia vilianza baada ya jeshi la Ujerumani ya Kinazi kuanzisha mashambulizo dhidi ya Poland.

Adolf Hitler alianza kuliandaa jeshi lenye nguvu wakati alipokuwa madarakani huko Ujerumani kwa kutumia vibaya hadhi yake na hisia za ubaguzi na utaifa wa wananchi wa nchi hiyo, ambao walikuwa wamefedheheka sana baada ya kushindwa vibaya katika Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia.

Katika kipindi kifupi, Hitler alifanikiwa kuikalia kwa mabavu sehemu kubwa ya ardhi za Ulaya na kaskazini mwa Afrika.   

Siku kama leo miaka 64 iliyopita, yaani tarehe Mosi Septemba mwaka 1961, ulifanyika mkutano wa kwanza wa wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya Isiyofungamana na Upande Wowote NAM huko Belgrade mji mkuu wa Yugoslavia ya zamani kwa kuhudhuriwa na viongozi wa nchi 25 duniani.

Jumuiya ya NAM iliasisiwa lengo kuu likiwa ni kuziunga mkono nchi za ulimwengu wa tatu mkabala na kambi za Mashariki na Magharibi. Masharti makuu ya kujiunga na jumuiya hiyo, ni kutokuwa mwanachama rasmi katika muungano unaofungamana na madola makubwa ya Mashariki na Magharibi.  

Na miaka 56 iliyopita katika siku kama ya leo, kulifanyika mapinduzi ya kijeshi nchini Libya yaliyomuingiza madarakani Kanali Muammar Gaddafi.

Kabla ya mapinduzi hayo, Libya ilikuwa ikiongozwa na utawala wa Mfalme Idris wa Kwanza. Wakati mfalme Idris alipoelekea nchini Uturuki kwa ajili ya matibabu, kundi moja la wanajeshi ambalo liliongozwa na Kanali Muammar Gaddafi lilifanya mapinduzi na kumvua madaraka mfalme huyo sambamba na kutangaza utawala wa kisoshalisti nchini Libya. Baada ya hapo Libya ilifuata siasa za Urusi ya zamani na kutaifisha sekta ya mafuta na benki.

Baada ya kusambaratika Urusi ya zamani, Muammar Gaddafi alianza kufuata siasa za Wamagharibi na kuwakabidhi viwanda vya mafuta vya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika, hali inayodaiwa kuchangia hasira za wananchi. Muammar Gaddafi aliondolewa madarakani na kuuawa kufuatia mapinduzi ya tarehe 21 mwezi Agosti 2011.