Jumanne, tarehe Pili Septemba, 2025
Leo ni Jumanne tarehe 9 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1447 Hijria mwafaka na tarehe Pili Septemba 2025.
Siku kama ya leo miaka 1180 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, baada ya kuuawa shahidi Imam Hassan Askari (AS) kilianza rasmi kipindi cha uongozi wa Imam wa Zama, Imam Mahdi (AF).
Imam Mahdi ni mwana wa Imam Hassan Askari (AS) na miongoni mwa wajukuu wa Mtume Muhammad (saw). Imam Mahdi yuko ghaiba kwa amri ya Mwenyezi Mungu (SW) na hadi mwaka 328 Hijria alikuwa akiwasiliana na watu kupitia wawakilishi wake maalumu. Kipindi hicho kilipewa jina la "Ghaiba Ndogo".
Baada ya hapo kilianza kipindi cha Ghaiba Kubwa ambapo Imam wa Zama hakuainisha mwakilishi makhsusi, na mafakihi wenye ujuzi wa dini ya Kiislamu, wacha-Mungu na watambuzi wa masuala ya zama ndio wawakilishi wa mtukufu huyo katika Umma.
Kwa mujibu wa hadithi tukufu za Mtume (saw), Imam Mahdi (AF) atadhihiri tena kwa ajili ya kueneza haki na uadilifu.

Siku kama ya leo miaka 224 iliyopita, baada ya vita kadhaa baina ya vikosi vya utawala wa Othmania na jeshi la Uingereza kwa upande mmoja na vikosi vya Ufaransa kwa upande mwingine, hatimaye Wafaransa walishindwa katika vita na kulazimika kuondoka kikamilifu nchini Misri.
Ikumbukwe kuwa, baada ya Napoleone Bonaparte kuikalia kwa mabavu ardhi ya Misri, Uingereza ambayo katika zama hizo ilikuwa ikihesabiwa kuwa hasimu na mshindani mkuu wa Ufaransa katika masuala ya kiuchumi na kijeshi, ilihisi maslahi yake yakiwa hatarini.
Ni kwa sababu hiyo ndio maana Uingereza ikaungana na utawala wa Othmania kwa shabaha ya kwenda kuitoa Ufaransa huko Misri na kuzuia jeshi la Ufaransa lisisonge mbele.

Katika siku kama ya leo miaka 160 iliyopita, William Rowan Hamilton mwanahisabati na mtaalamu mahiri wa elimu ya fizikia wa Ireland alifariki dunia.
Alizaliwa mwaka 1805 na kuonyesha kuwa mwerevu na mwenye kipaji cha hali ya juu tangu akiwa mtoto mdogo. Hamilton alisoma kwa ami yake aliyekuwa kasisi. Alipofikisha umri wa miaka 13, mwanafizikia huyo mtajika wa Ireland alikuwa tayari anazifahamu lugha kadhaa za kimataifa. Hadi anafikisha umri wa miaka 22 alikuwa tayari ni mwalimu katika elimu ya nujumu.

Siku kama ya leo miaka 80 iliyopita, nchi ya Vietnam ilipata uhuru. Vietnam ilivamiwa na kukaliwa kwa mabavu na Ufaransa katikati mwa karne ya 19.
Mwaka 1940 nchi hiyo ikadhibitiwa na Japan baada ya Ufaransa kushindwa na Ujerumani wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.
Vietnam iliendelea kuwa chini ya utawala na udhibiti wa Japan hadi pale Japan iliposalimu amri mwishoni mwa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.

Tarehe Pili Septemba mwaka 1945, Vita Vikuu vya Pili vya Dunia vilifikia tamati baada ya Japan kusalimu amri bila ya masharti yoyote.
Baada ya Japan kushindwa mfululizo na majeshi ya waitifaki, ililazimika kusalimu amri katika vita hivyo, hasa baada ya miji yake miwili mashuhuri ya Hiroshima na Nagasaki kushambuliwa na Marekani kwa mabomu ya atomiki.
Baada ya tukio hilo lililotokea miezi minne tu baada ya kusalimu amri Ujerumani, nchi waitifaki ziliikalia kwa mabavu Japan kwa mujibu wa Mkataba wa Potsdam na Generali wa Kimarekani, Douglas MacArthur, akachaguliwa kuwa kamanda mkuu huko Japan.
Mwaka 1951, nchi 49 duniani zilitiliana saini mkataba wa amani na Japan, na mwaka mmoja baadaye nchi hiyo kwa mara nyingine tena ikaanza kujitawala na kujiamulia mambo yake yenyewe.

Miaka 63 iliyopita katika siku kama hii ya leo kulingana na kalenda ya Hijria shamsia, yaani tarehe 11 Shahrivar 1341 tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 7.2 kwa kipimo cha rishta lilitikisa eneo la Buin Zahra, kaskazini magharibi mwa Iran.
Katika tetemeko hilo la kutisha, zaidi ya watu elfu 20 waliuawa na maelfu ya wengine walijeruhiwa. Kutokea kwa tetemeko hilo nyakati za usiku kuliwafanya watu wachache tu waweze kunusuru maisha yao. Katika tetemeko la ardhi la Buin Zahra, vijiji 120 vilitokomezwa kikamilifu na mamia ya nyumba ziliharibiwa vibaya.
Baada ya tukio hilo, bila kupoteza muda, watu wa Iran walipeleka misaada yao katika eneo hilo na kukimbilia kuwasaidia wananchi wenzao waliojeruhiwa. Buin Zahra ni eneo la matetemeko ya ardhi kwani mwaka 2013 lilipatwa na zilzala nyingine iliyoua watu wapatao 300.
