Sep 16, 2025 07:12 UTC
  • Jumanne, 16 Septemba 2025

Leo ni Jumanne tarehe 23 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1447 Hijria sawa na Septemba 16, 2025.

Siku kama ya leo miaka 1246 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, Bibi Fatima Maasuma, dada wa Imam Ali bin Mussa al-Ridha (as), aliwasili katika mji wa Qum, Iran.

Mwaka mmoja baada ya safari ya kubaidishiwa kaka yake huko katika mji wa Marv, Bibi Maasuma alifunga safari kutoka Madina kwa ajili ya kwenda kuonana na kaka na Imam wake huko Khorasani. Baada ya kuwasili Qum, aliishi katika mji huo kwa siku 17 na katika wakati huo alijishughulisha na ibada, dua na kujikurubisha kwa Mola Muumba. Eneo alilokuwa akifanyia ibada bibi huyo mtukufu hadi leo linajulikana kama 'Baitul Nur, na hadi leo linatembelewa na wapenzi wa Ahlul Bait wa Mtume Muhammad (saw). Mwishowe tarehe 10 Rabiul Thani mwaka 201 Hijiria, ikiwa ni kabla hajakutana na kaka yake, Imam Ridha (as), Bibi Fatima Maasuma alifariki dunia huku akiwa katika upweke na majonzi makubwa.

Hii leo Haram ya mjukuu huyo wa Mtume Muhammad (saw), Bibi Fatma Maasuma (as), katika mji wa Qum ni moja ya maeneo matakatifu ambapo watu kutoka katika maeneo mbalimbali ya dunia huenda kufanya ziara katika eneo hilo.

Miaka 289 iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia Daniel Gabriel Fahrenheit mwanahesabati na mwanafizikia wa Kijerumani aliyevumbua kipimajoto yaani thermometer, akiwa na umri wa miaka 50.

Fahrenheit alikuwa na fikra ya kubuni kifaa ambacho kingekuwa na uwezo wa kupima kiwango cha joto na mwaka 1724 mwanafizikia huyo Mjerumani akafanikiwa kutengeneza kipimajoto hicho. Kifaa hicho ambacho kimepewa jina la msomi huyo mwenyewe yaani Fahreinheit, bado kinatumika hadi leo. 

Siku kama ya leo miaka 204 iliyopita, Mexico ilijipatia uhuru.

Mexico ilipata uhuru baada ya miaka 300 ya kukoloniwa na Uhispania. Siku hii inatambulika kuwa siku ya kitaifa ya nchi hiyo. Nchi ya Mexico yenye kilomita za mraba 1,958,201 iko Amerika ya Kati na inapakana na Marekani na Guatemala. Akthari ya watu wa Mexico ni Wakatoliki.

Mji mkuu wa nchi hii ni Mexico City na sarafu yake ni peso. Wengi wa watu wa Mexico wana rangi mchanganyiko na wanazungumza Kihispania. 

Miaka 94 iliyopita mwafaka na siku hii ya leo, aliuawa Omar al Mukhtar kiongozi wa taifa la Libya katika mapambano ya ukombozi dhidi ya wakoloni wa Italia.

Omar Mukhtar aliyekuwa kiongozi wa kidini alizaliwa mwaka 1859. Mwaka 1895 alielekea Sudan na kushiriki katika harakati za kupambana na ukoloni wa Uingereza. Baada ya kushindwa kwa harakati hizo, Omar Mukhtar alirejea nchini Libya.

Mwaka 1911 Wataliano waliivamia Libya kwa lengo la kuitawala nchi hiyo. Kiongozi huyo wa kidini aliwahimiza wapiganaji wa makabila ya Libya kusimama kidete na kupambana dhidi ya wavamizi wa Kitaliano na kuwasababishia hasara kubwa. Hata hivyo, kwa kutumia askari wengi zaidi na silaha za kisasa, wavamizi hao walimzingira Omar Mukhtar na wenzake na kumkamata na kisha wakamnyonga katika siku kama ya leo.  

Siku kama ya leo miaka 93 iliyopita Sir Ronald Ross daktari mashuhuri wa Kiingereza na mvumbuzi wa chanzo cha ugonjwa wa Malaria alifariki dunia.

Alizaliwa Mei 13 mwaka 1857 katika mji wa Almora huko India. Alielekea Uingereza akiwa mdogo na kusoka akiwa huko ambapo alifanikiwa kupata shahada ya uzamivu PhD katika taaluma ya tiba.

Uvumbuzi wake wa chanzo cha Malaria ulikuwa na nafasi muhimu sana kwani uliandaa uwanja wa namna ya kukabiliana na maradhi hayo.

Mwaka 1902 Dakta Ronald Ross alitunukiwa tuzo ya Nobel. Hatimaye Daktari Ronald Ross aliaga dunia katika siku kama ya leo baada ya kuishi kwa muda wa miaka 75.   

Tarehe 16 Septemba miaka 86 iliyopita Warsaw mji mkuu wa Poland ulizingirwa na Wajerumani, katika mwezi wa kwanza wa Vita vya Pili vya Dunia.

Mashambulio ya wanajeshi wa Kinazi wa Ujerumani huko Poland yalianza siku 15 kabla ya kuanza vita hivyo.  

Na leo tarehe 16 Septemba ni Siku ya Kimataifa ya Kulindwa Tabaka la Ozoni.

Siku hii haina historia ndefu ikilinganishwa na matukio mengine ya kimataifa. Siku hii iliainishwa mwaka 1994 wakati nchi wanachama wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa zilipokubaliana kutenga siku maalumu ya kulindwa tabaka la Ozoni. Tangu wakati huo nchi zote ziliahidi kuanza kuzalisha na kutumia nyenzo na vitu ambavyo havina madhara kwa tabaka hilo.

Lengo la maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Ozoni ni kuhamasisha kulindwa tabaka hilo muhimu sana linalowalinda viumbe hai ardhini wasiathiriwe na mionzi hatari ya Kikiuka Urujuani (Ultraviolet).