Aug 13, 2016 02:40 UTC
  • Jumamosi, Agosti 13, 2016

Leo ni Jumamosi tarehe 10 Mfunguo Pili Dhil-Qaadah mwaka 1437 Hijria mwafaka na tarehe 13 Agosti mwaka 2016 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 60 iliyopita, nchi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati ilijikomboa na kupata uhuru toka kwa mkoloni Mfaransa. Ilikuwa katikati ya karne ya 19 wakati nchi hiyo iliyokuwa ikijulikana hapo kabla kwa jina la Ubangi-Shari, ilipounganishwa na makoloni ya Ufaransa barani Afrika. Hata hivyo mwaka 1958, Jamhuri ya Afrika ya Kati ilijipatia Mamlaka ya Ndani na miaka miwili baadaye yaani mwaka 1960, ikajikomboa na kupata uhuru kamili. ***

Miaka 117 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa Alfred Hitchcock mtengeneza filamu mashuhuri wa Kiingereza. Alionesha kazi yake ya kwanza mwaka 1920 na baadaye akaanza kujihusisha na uongozaji filamu. Filamu zake za kuogopesha na za kusisimua zilikuwa mashuhuri mno katika zama hizo. Filamu hizo zilimfanya awe mashuhuri kwa jina la the Master of Suspense. Miongoni mwa filamu zake ni The Man Who Knew Too Much na Young and Innocent. Alfred Hitchcock aliaga dunia tarehe 28 Aprili 1980.***

Siku kama ya leo miaka 45 iliyopita, Bahrain ilijitangazia uhuru wake kutoka kwa Iran. Kisiwa cha Bahrain kilichoko kusini mwa Ghuba ya Uajemi mwanzoni mwa utawala wa Qajar kilikuwa kikiongozwa kwa usimamizi wa Iran. Hata hivyo miaka kadhaa baadaye Waingereza walichukua mamlaka ya kukiongoza kisiwa hicho kwa kisingizio kwamba, Iran haina kikosi cha majini. Hilo lilitimia baada ya utawala wa Qajar kutilia saini mkataba na Uiongereza. Mamlaka ya Waingereza kwa Bahrain yaliendelea kwa muda wa miaka mia moja.***

Na katika siku kama ya leo miaka 30 iliyopita, Ayatullah Ali Najafi Kashani, alimu, mwanazuoni mahiri na mfasiri wa Qur'ani aliaga dunia. Alizaliwa mjini Kashani, moja ya miji ya katikati mwa Iran na alipofikisha umri wa miaka 22 alielekea Najaf Iraq kwa ajili ya kujiendeleza zaidi katika masomo ya dini. Aliporejea kutoka Najaf, Ayatullah Najafi Kashani alisoma mjini Qum kwa muda wa miaka mitatu na wakati huo huo akifundisha. Baadaye alirejea katika mji aliozaliwa yaani Kashani na kujishughulisha na kazi ya kufundisha na kuandika vitabu. Mwanazuoni huyo amevirithisha vizazi vilivyokuja baada yake vitabu vingi na vyenye thamani kubwa.***