Jumanne, 07 Oktoba 2025
Leo ni Jumanne 14 Mfunguo Saba Rabiuthani 1447 Hijria ambayo inasadifiana na 7 Oktoba 2025 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1381 iliyopita Mukhtar bin Abi Ubaida al-Thaqafi alianza mapambano ya kulipiza kisasi cha damu ya Imam Hussein bin Ali (a.s), mjukuu wa Mtume Muhammad SAW. Mwaka 61 Hijria Imam Hussein (as) akiwa pamoja na wafuasi na watu wa familia yake, aliuawa shahidi na jeshi la Yazid akiwa katika harakati za kuilinda dini tukufu ya Uislamu. Mukhtar alianzisha harakati zake za mapambano katika mji wa Kufa. Kabla yake, kulijitokeza kundi la 'Tawwabiin' ambalo lilipigana na utawala wa Bani Umayyah, kwa lengo la kulipiza kisasi cha damu ya Imam Hussein AS. Mukhtar Thaqafi alitawala Kufa kwa kipindi cha karibu mwaka mmoja na mwishowe alishindwa na jeshi la Mus'ab bin Zubair na kuuawa shahidi.

Siku kama ya leo miaka 118 iliyopita, Muhammad Ali Shah Qajar alitia saini kikamilisho cha Katiba. Kufuatia kushadidi harakati za kupigania katiba nchini Iran na mapambano ya kila upande ya wananchi na viongozi wa kidini, Mozaffar ad-Din Shah Qajar alilazimika kukubaliana na matakwa ya wananchi ambapo mbali na mambo mengine alitoa amri ya kuundwa Bunge la Taifa. Awali Muhammad Ali Shah alikuwa akipoteza muda katika kufanikisha kikamilisho hicho cha Katiba, lakini mashinikizo ya wananchi na wanazuoni yalimlazimisha katika siku kama ya leo alazimika kutekeleza jambo hilo. ***

Siku kama ya leo miaka 97 iliyopita, Sohrab Sepehri malenga na mchoraji wa Kiirani alizaliwa katika mji wa Kashan moja ya miji ya katikati mwa Iran. Mwaka 1330 Hijiria Sepehri alitoa majimui ya kwanza ya tungo zake za mashairi zilizoitwa "Marge Rang" na akatoa tena majimui nyingine ya vitabu vinane. Aidha mbali na Sohrab Sepehri kuwa malenga mkubwa, alipendelea sana taaluma ya uchoraji. Miongoni mwa athari za Sepehri ni pamoja na majimui za vitabu vya mashairi vinavyoitwa "Zendegi Khob'ha", "Musafir" na "Aavaz Oftaab." Sohrab Sepehri alifariki dunia mwaka 1359 Hijiria na kuzikwa mahali alipozaliwa yaani mjini Kashan. ***

Katika siku kama ya leo miaka 76 iliyopita, Ujerumani ya Mashariki iliasisiwa na kuwa na mfumo wa Jamhuri ya Kidemokrasia. Katika miezi ya mwishoni mwa Vita vya Pili vya Dunia, Shirikisho la Umoja wa Sovieti lilivamia na kuikalia kwa mabavu ardhi ya Ujerumani ya Mashariki, na madola ya Magharibi yakadhibiti sehemu ya magharibi mwa nchi hiyo. Hata hivyo baadaye Umoja wa Sovieti ulijitoa katika Baraza la Makamanda Waitifaki baada ya kutofautiana na madola ya Magharibi juu ya namna ya kuiendesha nchi hiyo.

Miaka 32 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsia, mwanazuoni wa fakihi Ayatullah Hassan Muhammadi Laini aliaga dunia. Alizaliwa katika moja ya vijiji vya Busheh Iran. Laini alimpoteza baba yake aliyeaga dunia wakati yeye akiwa angali mdogo na kulelewa na mama yake. Baada ya masomo ya msingi alielekea Najaf Iraq na kubakia huko kwa muda wa miaka 12 akihudhuria darsa na masomo ya wanazuoni wakubwa wa zama hizo kama Sayyid Mahmoud Shahroudi na Mirza Hashhim Amoli. Ayatullah Hassan Muhammadi Laini alishiriki pia katika harakati za mapambano ya wananchi wa Iran dhidi ya utawala dhalimu wa Kipahlavi na baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kkiislamu alikuwa mwakilishi wa wananchi wa Mazandaran kwa duru mbili katika Baraza la Wanazuoni la Kumchagua Kiongozi Muadhamu na kusimamia kazi zake. ***

Miaka 24 liyopita katika siku kama ya leo yaani tarehe 7 Oktoba 2001, Marekani iliivamia Afghanistan. Uvamizi huo ulifanyika kwa kisingizio cha kuliangamiza kundi la wanamgambo wa Al-Qaida ambao kwa mujibu wa Washington walihusika na tukio la Septemba 11 mwaka 2001 nchini Marekani. Katika kipindi cha wiki kadhaa, ndege za kivita za Marekani, zilifanya mashambulizi dhidi ya ngome za kundi la Taliban ambalo katika kipindi hicho lilikuwa likidhibiti eneo kubwa la ardhi ya Afghanistan sambamba na kuliunga mkono kundi la Al-Qaida lililokuwa likiongozwa na Osama bin Laden. Mashambulizi hayo mazito ya Marekani yaliua na kujeruhi maelfu ya raia wasio na hatia wa Afghanistan huku wengine wakilazimika kuwa wakimbizi.

Miaka miwili iliyopita katika siku kama ya leo, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS ilitekeleza operesheni ya kushtukiza kwa kupenya ndani ya ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu (Israel). Operesheni hiyo iliyojulikana kwa jina la Kimbunga cha al-Aqswa ilipelekea kuchukuliwa mateka makumi ya Wazzayuni. Operesheni ya Kimbucha cha al-Aqswa ilitekelezwa wakati ambao Israel ilikuwa katikka harakati za kuanzisha uhusiano wa kawaida na baadhi yya mataifa ya Kiarabu. Israel ikiwa na lengo la kujibu operesheni ya Hamas ilianzisha ahujuma kubwa ya kijeshi ya anga na baharini dhidi ya Ukandaa wa Gaza. Katika kipindi hiki cha miaka miwili, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahuu na serikali yake wamefanya mauaji makubwa ya kimbari katika Ukanda wa Gaza. Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC imetoa waranti wa kuutiwa mbaroni Netanyahu kwa Kutenda jinai za kivita.
