Nov 13, 2025 02:35 UTC
  • Alkhamisi, 13 Novemba, 2025

Leo ni Alkhamisi tarehe 22 Jamadil Awwal 1447 Hijria ambayo inasadifiana na tarehe 13 Novemba 2025.

Siku kama ya leo miaka 55 iliyopita hayati Hafidh Assad alichukua hatamu za uongozi wa Syria baada ya mapinduzi ya kijeshi mwaka 1970 na baadaye akachaguliwa kuwa kiongozi wa chama cha Baath. 

Hafidh Assad alizaliwa mwaka 1930 na mwaka 1964 alichaguliwa kuwa kamanda wa kikosi cha anga cha jeshi la Syria. Miaka mitatu baadaye aliteuliwa kuwa Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo.

Hafidh Assad alifariki dunia mwezi Juni mwaka 2000 baada ya kuugua kwa muda mrefu.   

Hafidh Assad

Miaka 55 iliyopita katika siku kama ya leo, mwafaka na tarehe 13 Novemba 1970, tufani kubwa na kimbunga cha kutisha kiliikumba nchi ya Bangladesh.

Janga hilo lilitokea wakati mapambano ya Wabangali kwa ajili ya kujitenga na Pakistan na kupata uhuru yalipokuwa kileleni. Tufani hiyo kubwa ilisababisha vifo vya watu laki mbili na kujeruhi wengine laki nane. Kimbunga na tufani hiyo pia iliwalazimisha mamia ya maelfu ya watu kukimbia makazi yao na kusababisha hasara kubwa katika mashamba, viwanda, makazi ya raia na miundombinu ya nchi hiyo.

Bangladesh ni miongoni mwa nchi zinazokumbwa na majanga ya kimaumbile kama vimbunga, tufani na mafuriko ya mara kwa mara.  ***

Miaka 29 iliyopita katika siku kama ya leo aliaga dunia Ayatullah Sayyid Morteza Pasandideh, kaka wa Imam Ruhullah Khomeini.

Alisoma masomo ya awali ya kidini kwa maulama na wanazuoni wa mji wa Isfahan na kushiriki masomo ya elimuu ya juu ya kidini kwa maustadhi mashuhuri wa zama hizo. Baadaye alirejea katika mji wa Khomein na kujishuhulisha na ufundishaji wa fikihi, usuul na masomo mengine.

Ayatullah Pasandideh anayejulikana kama alimu na mujahidi, kipindi fulani alibaidishwa kutokana na upinzani wake kwa utawala wa kifalme wa wakati huo wa Reza Khan na kusimama kwake kidete dhidi ya utawala huo.   

سیدمرتضی پسندیده

 

Katika siku kama ya leo miaka 17 iliyopita, alifariki dunia Ayatuhil Udhma Muhammad Taqi Behjat Foumani, mmoja wa Marajii Taqlidi na maurafaa wakubwa wa Kiislamu.

Alizaliwa mwaka 1294 Hijria Shamsia katika mji wa Fouman ulioko katika mkoa wa Gilan kaskazini mwa Iran. Baada ya kupata elimu ya msingi ya kidini, mwaka 1308 Hijria Shamsia alielekea katika Chuo Kikuu cha Kidini cha Najaf nchini Iraq.

Ayatullah Bahjat alikuwa mashuhuri sana kutokana na uchamungu wake. Kitabus Swalat, Jamiul Masail na Wasilatun Najat ni baadhi ya vitabu mashuhuri vya msomi huyo. 

آیت ‌الله شیخ محمدتقی بهجت

 

Na miaka 10 iliyopita tarehe 13 Novemba saa tatu na dakika 16 usiku kwa wakati wa Ulaya ya Kati, milipuko kadhaa ya kigaidi ilitokea katika vitongoji nambari 1, 10 na 11 vya jiji la Paris nchini Ufaransa na kuua watu 130 na kujeruhiwa wengine 368.

Baadhi ya milipuko hiyo ilitokea karibu na uwanja wa michezo wa Stade de France ulioko kaskazini mwa jiji la Paris wakati wa mechi ya mpira wa miguu kati ya timu za taifa za Ufaransa na Ujerumani. Wakati huo huo watu wengine 87 waliuawa katika utekeji nyara uliofanyika katika ukumbi wa michezo ya kuigiza wa Bataclan mjini Paris.

Mashambulizi hayo yalihesabiwa kuwa makubwa zaidi kutokea nchini Ufaransa baada ya Vita vya Pili vya Dunia. Siku moja baadaye kundi la kigaidi la Daesh lilitangaza kuwa ndilo lililohusika na mashambulizi hayo.