Jumapili, 16 Novemba, 2025
Leo ni Jumapili 25 Mfunguo Nane Jamadul-Awwal 1447 Hijria mwafaka na 16 Novemba 2025.
Siku kama ya leo miaka 382 iliyopita Jean Chardin mtambuzi wa masuala ya Mashariki na mwanafalsafa mtajika wa Ufaransa alizaliwa katika mji wa Paris. Alikulia na kusoma katika mji huo. Baba yake Jean Chardin alikuwa sonara na alijifunza tangu akiwa mtoto mdogo utambuzi wa mawe, madini na taaluma ya usonara.
Miaka 80 iliyopita katika siku kama ya leo, vikosi vya jeshi la Ufaransa viliishambulia Vietnam na kuanza mapambano ya muda mrefu ya wananchi kwa ajili ya kuikomboa nchi hiyo. Baada ya karne moja ya kukoloniwa Vietnam na Ufaransa, wakati wa Vita vya Pili vya Dunia Japan iliidhibiti nchi hiyo. Japan iliondoka Vietnam baada ya kushindwa katika vita hivyo, na Vietnam ikaanza kukaliwa kwa mabavu na Ufaransa.

Katika siku kama ya leo miaka 39 iliyopita, aliaga dunia Ustadh Muhammad Taqi Modarres Razavi, mwandishi, mwanafasihi na mhakiki mahiri wa Kiirani. Msomi huyo aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 95. Muhammad Taqi Modarres Razavi alizaliwa katika mji wa Mash'had kaskazini mashariki mwa Iran na baadaye akahamia Tehran. Baada ya kuhitimu masomo yake alianza kujishughulisha na kazi ya uhakiki, utafiti na kujifunza lugha ya Kifaransa. Kwa miaka mingi mwalimu huyo alijishughulisha na kazi ya kufuundisha vijana na kipindi fulani alishiriki katika kazi ya kuandika kamusi kubwa ya Dekhoda. Alikuwa mahiri pia katika elimu za fikihi, mantiki na falsafa.
Siku kama ya leo miaka 27 iliyopita, Allama Muhammad Taqi Ja'fari, mwanafalsafa na mwanafikra mkubwa wa Kiislamu aliaga dunia. Alizaliwa mwaka 1304 Hijria Shamsia katika mji wa Tabriz kaskazini magharibi mwa Iran. Kipaji chake kilidhihiri na kuchomoza tangu akiwa katika kipindi cha kuinukia kwake ambapo kabla ya kuanza shule ya msingi tayari alikuwa amejifunza Qur'ani. Akiwa shule alionekana mwenye kipaji mno. Hata hivyo umasikini ulimfanya aache shule na kuanza kufanya kazi. Pamoja na kufanya kazi aliutumia muda wake wa ziada kusoma masomo ya dini. Allama Muhammad Taqi Ja'fari ameandika vitabu vingi ambapo Tarjuma na Tafsiri ya Nahajul Balagha ndio kitabu muhimu zaidi cha mwanazuoni huyo.
Miaka 25 iliyopita sawa na tarehe 25 Aban 1379 Hijria Shamsia, aliaga dunia Hujjatul Islam, Dakta Muhammad Hadi Amini Najafi, mmoja wa maulama na waandishi mahiri wa Kiirani. Alizaliwa Tabriz kaskazini magharibi mwa Iran, na katika kipindi cha ujana wake alielekea huko Najaf, Iraq akiwa pamoja na baba yake, Allama Amini, mwandishi wa kitabu mashuhuri cha al-Ghadir. Msomi huyo alifanikiwa kupata shahada ya uzamivu katika Chuo Kikuu cha Kiislamu cha al-Azhar nchini Misri. Mwaka 1350 Hijria Shamsia Dakta Muhammad Hadi Amini Najafi alirejea nchini Iran na kuanza kufanya kazi ya uandishi, kufundisha na kufanya uhakiki.