Jumapili, 14 Disemba, 2025
-
Leo katika historia
Leo ni Jumapili mwezi 23 Mfunguo Tisa 1447 Hijria ambayo inasadifiana na 14 Disemba 2025 Miladia.
Katika siku kama ya leo miaka 226 iliyopita, George Washington, alifariki dunia. George Washington, Rais wa kwanza wa Marekani, alizaliwa huko Virginia Februari 12, 1732. Licha ya kufiwa na baba yake, aliendelea na elimu yake na kuwa mtu mashuhuri katika Mapinduzi ya Marekani wakati wa Vita vya Wafaransa na kupinga sera za ukoloni wa Uingereza.Washington aliteuliwa kuwa kamanda wa majeshi ya kikoloni wakati wa Mapinduzi ya Marekani na, kwa azma na irada, aliweza kufanikisha uhuru wa Marekani. Mnamo 1787, alikuwa Mkuu wa Taasisi ya Kuandaa Katiba na mwaka uliofuata, alichaguliwa kuwa Rais wa kwanza wa Marekani.

Katika siku kama ya leo miaka 121 iliyopita, alizaliwa Dk. Mahmoud Najmabadi mmoja wa madaktari na wahakiki mahiri wa Iran. Baada ya kumaliza elimu yake ya msingi, alienda katika shule ya tiba na kuhitimu huko. Mbali na kutibu wagonjwa, Dk. Najmabadi pia alifundisha katika chuo kikuu na alikuwa na hamu maalum ya kusoma tiba ya Kiislamu-Kiirani. Kuhusiana na hilo, ameandika vitabu vinavyotambulisha watu mashuhuri wa kitabibu kutoka katika ulimwengu wa Kiislamu na Iran, hususan Muhammad bin Zakariyya al-Razi, na pia ametafsiri idadi ya vitabu vyao.

Siku kama ya leo miaka 113 iliyopita inayosadifiana na tarehe 14 Disemba 1911, baada ya juhudi na jitihada za miaka mingi, hatimaye Ncha ya Kusini yaani South Pole ilivumbuliwa na kwa mara ya kwanza na wavumbuzi kadhaa waliwasili katika eneo hilo. Katika siku hii, Roald Amundsen baharia mashuhuri wa Kinorway aliyekuwa akishindana na Robert Falcon Scott wa Uingereza ili kuifikia ncha hiyo ya kusini, aliibuka mshindi na kuitundika bendera ya Norway katika ncha hiyo. Robert Falcon Scott akiwa na wenzake walikumbana na theluji kali wakati wanarejea na kupoteza maisha yao.

Katika siku kama ya leo miaka 43 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 14 Disemba 1981 Bunge la utawala haramu wa Israel 'Knesset' liliiunganisha rasmi miinuko ya Golan ya huko Syria na ardhi za Palestina unazozikalia kwa mabavu. Hatua hiyo ya kinyama ilikabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa nchi za Kiislamu, Kiarabu pamoja na jamii ya kimataifa. Utawala dhalimu wa Israel uliikalia kwa mabavu miinuko hiyo ya Golan ya Syria katika vita baina yake na Waarabu mwaka 1967.

Katika siku kama ya leo miaka 28 iliyopita, makubaliano ya amani ya Bosnia yaliyojulikana kwa jina la "Dayton Peace Agreement" yaani Makubaliano ya Amani ya Dayton" yalithibitishwa kwa mara ya mwisho katika kikao kilichofanyika mjini Paris, Ufaransa. Makubaliano hayo ambayo yalifanyika kwa mashinikizo ya viongozi wa Marekani tarehe 21 Novemba 1995, yalitiwa saini na Marais wa wakati huo wa Bosnia Herzegovina, Serbia na Croatia. Mafanikio pekee ya makubaliano hayo kwa upande wa Waislamu, yalikuwa ni kuhitimishwa mauaji ya kinyama yaliyokuwa yakifanywa dhidi yao na Waserbia.
