Aug 20, 2016 05:58 UTC
  • Jumamosi, 20 Agosti 2016

Leo ni Jumamosi tarehe 17 Mfunguo Pili Dhil-Qaadah mwaka 1437 Hijria mwafaka na tareje 20 Agosti mwaka 2016 Miladia.

 

Image Caption

Siku kama ya leo miaka 1258 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, Imam Mussa Kadhim AS imam wa saba katika mlolongo wa Maimamu 12 kutoka katika kizazi cha Bwana Mtume SAW alibaidishiwa Iraq kutoka Madina kwa amri ya Harun Radhid mtawala dhalimu wa Bani Abbas. Kipindi fulani Imam Kadhim AS alikuwa katika jela ya Issa bin Ja'afar mtawala wa Basra Iraq. Baadaye mtawala huyo alimuandikia barua Harun Rashid akimtaka amkabidhi Imam Kadhim kwa mtu mwingine kwani katika kipindi chote hicho hajapata ushahidi unaoonesha kwamba yuko dhidi yake.***

Agosti 20 mwaka 1998 yaani miaka 18 iliyopita, Marekani ilizishambulia kwa makombora ya masafa marefu Sudan na Afghanistan. Serikali ya Washington ilidai kwamba, watu walioshiriki katika kulipua kwa mabomu balozi za Marekani mjini Dar es Salaam, Tanzania na Nairobi, Kenya wiki mbili kabla, walikuwa na uhusiano na nchi hizo. Aidha Washington ilisema ilikishambulia kwa mabomu kiwanda cha kuzalisha madawa cha ash-Shifaa nchini Sudan kwa madai kwamba kilikuwa kikitengeneza mada za kemikali. Hata hivyo weledi wa masuala ya kisiasa walisema kwamba, sababu ya Marekani kufanya mashambulio ya mabomu dhidi ya Sudan na Afghanistan ilikuwa ni kujaribu kufunika fedheha ya kimaadili iliyokuwa ikimkabili rais wa nchi hiyo Bill Clinton. Kwa sababu hiyo mashambulizi hayo yaliamsha hasira za fikra za walio wengi na serikali nyingi duniani dhidi ya siasa za kutumia mabavu na kujichukulia maamuzi ya upande mmoja za Marekani. ***

Ayatullahil Udhma Sheikh Abdulkarim Hairi Yazdi

Na miaka 82 iliyopita, alifariki dunia Ayatullahil Udhma Sheikh Abdulkarim Hairi Yazdi fakihi na mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu ambaye aliasisi chuo kikuu cha kidini cha Qum. Alimu huyo alizaliwa katika mji wa Yazd katikati mwa Iran na baada ya kupata elimu ya mwanzo alielekea nchini Iraq ili kuendelea na masomo ambako alipata elimu na maarifa kutoka kwa maulamaa maarufu wa zama hizo na kufikia daraja ya juu ya ijitihad. Ayatullah Hairi Yazdi aliporejea Iran alihisi haja ya kuwepo chuo chenye nguvu cha elimu ya dini na kwa minajili hiyo mwaka 1340 Hijiria Shamsia alinzisha Hauza ya Qum ambayo ni Chuo Kikuu cha Kidini katika mji mtakatifu wa Qum. Hauza ya Qum ilipanuka kwa kasi na hivi sasa ni miongoni mwa vituo muhimu vya elimu katika ulimwengu wa Kiislamu.***