Aug 30, 2016 09:23 UTC
  • Hadithi ya Uongofu (49)

Assalaamu alaykum wapenzi wasikilizaji popote pale yanapokufikieni matangazi haya ya Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Ni wasaa mwingine wa kukutana nanyi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu.

Kipindi hiki hujadili maudhui mbalimbali na kukunukukieni hadithi zenye miogozo kutoka kwa Bwana Mtume SAW na Ahlul Bayt wake watoharifu AS. Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 49 kitazungumzi maudhui ya uadilifu wa Mwenyezi Mungu. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi kutegea machache niliyokuandalieni kwa juma hili. Karibuni.

Uadilifu ni moja ya misingi ya Uislamu wa kweli. Kuamini msingi na asili ya uadilifu mbali na kuwa na nafasi muhimu katika mtazamo wa mtu kuhusiana na dunia na kumtambua Mwenyezi Mungu, hatua hiyo huwa na taathira mno katika amali na matendo katika uadilifu wa mtu na jamii kwa ujumla. Kwa hakika suala la uadilifu wa Mwenyezi ni moja ya misingi muhimu ya kiitikadi katika Uislamu. Imam Ja'afar Swadiq AS, Imamu wa Sita katika mlolongo wa Maimamu watoharifu kutoka katika kizazi cha Bwana Mtume SAW anasema: Msingi wa dini ni Tawhidi na Uadilifu.

 

Bwana mmoja akamtaka Imam amfafanulie jambo hilo. Imam Swadiq AS akasema: Tawhidi ni kile ambacho kuhusiana na wewe kiumbe kinafaa na kwa Mwenyezi Mungu hakifai. Na uadilifu ni kutomnasibisha Mwenyezi Mungu na jambo au dhulma ambayo wewe umelaumiwa kwao.

Aidha imekuja katika Hadith al-Qudsi ya kwamba, Mwenyezi Mungu amesema: Enyi waja wangu! Kama ambavyo nimejiharamia dhulma ndivyo ambavyo pia nimeiharamisha dhulma baina yenu. Hivyo basi msidhulumiane."

Kwa hakika Mwenyezi Mungu  amemjaalia na kumtunuku mauhiba, ujuzi na neema kila mwanadamu kulingana na ustahiki wake. Katika aya ya 50 ya Surat Taha Mtume huyo wa Mwenyezi Mungu anamhutubu Firauni kwa kumwambia:

Akasema: Mola wetu Mlezi ni yule aliye kipa kila kitu umbo lake, kisha akakiongoa.

Kwa msingi huo basi, kila kiumbe anapokea na kupata neema za Mwenyezi Mungu kulingana na uwezo na kipaji alichonacho. Kiuhakika ni kuwa, uadilifu wa Mwenyezi Mungu umesimama juu ya msingi huu kwamba, fadhila zake zinamfikia kila kiumbe.  Hivyo basi uadilifu wa Mwenyezi Mungu ndio fadhila yenyewe.

Imani ya kweli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kama ambavyo akili ilivyo tufahamisha na dalili zikatuongoza juu ya hilo, hiyo ni Imani ya moja kwa moja ya ile nguvu iumbayo ambayo iliufanya ulimwengu huu uwepo na vyote vilivyomo na waliomo, na nguvu hii ikauwekea ulimwengu nidhamu hii iliyo pangwa na mfumo madhubuti.

Maana ya Mwenyezi Mungu kuwa ni muadilifu ni kwamba, hadhulumu haki ya kiumbe yeyote yule na humpatia neema kila kiumbe kulingana na mfumo wa ulimwengu. Neema za Mwenyezi Mungu zimeenea kiasi kwamba, kila mwanadamu aweze kunufaika nazo na kufikia ukamilifu. Hadith al-Qudsi ifuatayo imenukuliwa kutoka kwa Malaika Jibril AS ya kwamba Mwenyezi Mungu amesema: Baadhi ya waja wangu waumini ni watu ambao wanataka kuingia katika utukufu wangu kupitia njia ya ibada, lakini mimi ninazuia hilo ili isije ikajitokeza hali ya ghururi na kiburi katika nafsi zao hata ziwaharibu. Baadhi ya waja wangu wengine waumini ni watu ambao imani yao haibakii na kutengenea isipokuwa kwa kuambatana na umasikini kwani nitakapowafanya sio wahitaji hali hiyo ya kutohitajia itawaharibu. Na baadhi ya waja wangu waumini ni watu ambao imani yao haitengemai na kubakia isipokuwa kwa kuambatana na utajiri na kama nitawafanya kuwa ni wenye kuhitajia basi hali hiyo ya kuwa wahitaji huwaharibu. Baadhi ya waja wangu waumini ni watu ambao imani yao haitengemai na kubakia isipokuwa kwa kuambatana na maradhi ambapo kama nikiwapa afya njema hali hiyo huwaharivu. Baadhi ya waja wangu wengine wauminbi, ni watu amabo imani yao haitengemai na kubakia isipokuwa kwa kumabatana na afya njena ambapo kama nitawafanya wawe wagonjwa, basi maradhi hayo huwaharibu. Ukweli ni kuwa ninawaongoza na kuwasimamia waja wangu kutokana na ufahamu niliyonao katika nyoyo zao; kwani mimi ni mjuzi na mwenye kujua.”

 

Kama ambavyo tumeona kwamba, Mwenyezi Mungu ni muadilifu katika kuwapa neema waja wake kulingana na vipaji, maandalizi na ustahiki walionao, vivyo hivyo ni muadilifu katika daraja ya kuwapa ujira au kuwaadhibu waja wake. Ujira na adhabu aliyoianisha Mwenyezi Mungu inalingana na amali na matendo ya wanadamu. Kwa msingi huo, Mwenyezi Mungu huwapa ujira wale waliotenda amali njema na wale waliotenda matendo mabaya wataadhibiwa kutokana na amali zao hizo mbaya.

Aidha uadilifu wa Mwenyezi Mungu unahukumu kwamba, hakuna mwanadamu ambaye ataadhibiwa kutokana na taklifu ambayo hakufikishiwa khabari zake. Baadhi ya ujira na adhabu hizo ni hapa hapa duniani na nyingine ni Siku ya Kiyama. Mwenyezi Mungu anasema katika Surat Zilzala kwamba:

Basi anaye tenda chembe ya wema, atauona

Na anaye tenda chembe ya uovu atauona!

Wapenzi wasikilizaji kutokana na kumalizika muda wa kipindi hiki sina budi kukomea hapa kwa leo. Tukutane tena wiki ijayo, panapo majaaliwa yake Mola.

Wassalaamu alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh