Maafa ya Mina (2)
Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Karibuni wasikilizaji wapenzi kusikiliza kipindi hiki maalumu ambacho tumekuandalieni kwa mnasaba wa kukumbuka maafa yaliyotokea katika msimu wa Hija wa mwaka uliopita wa 2015 katika eneo la Mina katika ardhi tukufu ya Makka yaliyosababisha maelfu ya mahujaji wa Nyumba Tukufu ya Allah kupoteza maisha yao.
Maafa ambayo kinyume na madai ya utawala wa Aal Saud kwamba yalikuwa ni tukio la ajali au hata kuyanasabisha na mahujaji wenyewe, yalitokana na uzembe na usimamizi mbovu wa utawala huo. Endeleeni kuwa nami kuanzia mwanzo hadi mwisho kusikiliza niliyokuandalieni katika sehemu hii ya pili ya kipindi hiki.
Kama tulivyotangulia kueleza katika kipindi kilichopita, Hija ni faradhi ya kidini ya kujumuika pamoja na yenye adhama, inayotekelezwa kwa kushiriki mamia ya maelfu ya watu; na ndio maana inahitaji kudhaminiwa usalama ulioratibiwa na wa pande zote. Lakini kwa masikitiko, utawala wa Aal Saud hadi sasa umeshindwa kudhamini usalama kwa ajili ya mahujaji wa Nyumba tukufu ya Mwenyezi Mungu. Katika kipindi cha miaka kadhaa iliyopita wafanya ziara wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu wamefikwa na maafa kadha wa kadha. Lakini kwa kuwa hali hairuhusu kuyaorodhesha yote hapa tunatumia fursa hii kuyataja baadhi tu ya maafa hayo kulingana na umuhimu wake.
Matukio mengi zaidi ya maafa ya msimu wa Hija yametokea katika ardhi ya Mina iliyoko umbali wa kilomita tano mashariki mwa mji wa Makka. Asubuhi ya mwezi 10 Dhulhijjah, yaani siku ya Idul-Adh'ha, mahujaji wote huelekea kwenye ardhi hiyo tukufu; na hadi mwezi 12 mfunguo tatu hutekeleza mara tatu amali ya kumpiga mawe shetani na hatimaye hurejea ardhi ya Makkatul-Mukarramah. Matukio ya Mina baadhi ya wakati husababishwa na kuwaka moto na wakati mwengine kutokana na msongamano wa watu; na kutokana na maafa hayo, maelfu ya mahujaji walioelekea Saudia na matumaini ya kutekeleza faradhi ya Hija katika anga ya amani na utulivu, safari yao hiyo huwa ya mwanzo na ya mwisho na ya moja kwa moja isiyo na marudio ya makwao walikotoka.
Tarehe 10 Desemba mwaka 1975, zaidi ya mahujaji 200 walifariki dunia na mamia ya wengine walijeruhiwa huko Mina katika tukio la moto mkubwa uliosababishwa na mripuko wa mtungi wa gesi. Manusura wa moto huo wangali wanasimulia mandhari za kuungulisha nyoyo na za kusikitisha za mahujaji waliouawa na kujeruhiwa kutokana na mienge mikubwa ya moto na msongamano mkubwa wa watu. Lakini ajabu ni kwamba hakukuwepo athari yoyote ya vikosi vya utoaji misaada vya Saudia wakati wa tukio hilo, bali ni mahujaji wenyewe waliokuwa wakisaidiana wao kwa wao.
Tukio hilo chungu halikuwagutusha viongozi wa serikali ya Saudia kufikiria njia za kuzuia kutokea tena matukio kama hayo. Kwani mnamo mwaka 1995, watu wanaokadiriwa kufikia 100 waliuawa na kujeruhiwa katika moto uliozuka kwenye mahema huko Mina. Lakini baada ya tukio hilo, miaka miwili tu baadaye, maafa makubwa zaidi yalitokea, baada ya kuzuka moto mkubwa uliosababisha vifo vya mahujaji 343 na kujeruhiwa wengine zaidi ya 1,500. Maafa hayo ya kusononesha nyoyo ya kupotea roho chungu nzima za mahujaji yalijiri katika hali ambayo tangu mwaka 1975 hadi 1997, utawala wa Aal Saud ulikuwa umepata muda wa kutosha wa miaka 22 kutayarisha suhula na vifaa vinavyohitajika ili kuepusha kutokea matukio kama hayo yanayosababisha maafa ya kupotea roho za watu. Lakini inavyoonesha, roho za mahujaji na wafanya ziara wa Nyumba Mwenyezi Mungu hazina umuhimu kwao na ndio maana wanaamua kutumia zaidi fedha zao katika mambo ya kujionesha mbele ya macho ya watu na ambayo yatawafaidisha wao wenyewe kipropaganda.
Kama tulivyotangulia kueleza, msongamano mkubwa wa watu ni sababu nyengine kuu ya kufariki mahujaji katika ardhi ya Mina, ambao husababishwa na kuwepo idadi kubwa ya wafanya ziara hao na kushindwa askari usalama wa Saudia kuratibu mipango mizuri na udhibiti sahihi wa mambo. Ajabu ni kwamba kadiri siku zinavyopita, kiwango cha maafa yanayotokana na matukio hayo ya kuhuzunisha kinakuwa kikubwa zaidi. Wakati wa msimu wa Hija wa mwaka 1990 njia ya chini kwa chini inayoishia kwenye ardhi ya Mina ilifungwa wakati umati mkubwa wa mahujaji ulipokuwa ukipita na chombo cha kupitisha hewa katika njia hiyo kikazimika. Matokeo yake watu 1,426 walifariki dunia na wengine wengi kujeruhiwa kutokana na joto, kukosa hewa ya kupumua na mbinyano mkubwa wa watu. Mnamo mwaka 1998 pia katika mbinyano wa watu huko Mina, mahujaji 118 waliaga dunia na wengine 180 walijeruhiwa. Matukio mengi ya Mina hutokea wakati wa Ram'i'-Jamarat, yaani kuzirembea kwa mawe nembo za shetani. Kiasi kwamba kutokana na msongamano wa watu na utaratibu mbovu wa utawala wa Saudia, jumla ya mahujaji 270 walifariki dunia mwaka 1994, 35 walifariki mwaka 2001, 251 walipoteza maisha mwaka 2004 na 360 waliaga dunia mwaka 2006 mbali na mamia ya mahujaji waliojeruhiwa. Mwaka huohuo wa 2006 watu 76 walipoteza maisha baada ya hoteli moja kuporomoka huko mjini Makka.
Matukio muhimu ya maafa yaliyotokea ndani ya mji wa Makka, ukiondoa hayo tuliyotangulia kuyataja, mengi yao yamesababishwa na vikosi vya usalama vya utawala wa Aal Saud. Mnamo mwaka 1979, baada ya kumalizika amali za Hija, kundi moja la wapinzani wa utawala huo liliuvamia na kuudhibiti msikiti mtukufu wa Makka. Mahujaji 153 waliuawa katika mapigano yaliyotokea baina ya vikosi vya utawala wa Aal Saud na wapinzani hao.
Mwaka 1987, jinai ambayo haijawahi kushuhudiwa ilitokea katika mji wa Makka wakati vikosi vya usalama vya utawala wa Aal Saud vilipowashambulia kwa silaha mahujaji waliokuwa wakiandamana kutangaza kujibari na Marekani na utawala wa Kizayuni. Askari hao waliwaua shahidi kinyama wafanya ziara 402 wa Nyumba tukufu ya Mwenyezi Mungu kwa kuwapiga risasi na kuwajeruhi wengine 650. Jinai hiyo ilibakisha doa jeusi la fedheha katika kumbukumbu za faili la ushahidi wa kuthibitisha jinsi utawala wa Aal Saud usivyo na sifa zinazotakiwa na uwezo wa kudhamini amani na usalama wa mahujaji.
Kutokuwa na ustahiki utawala wa Aal Saud na uwezo wa kusimamia Hija na kudhamini utulivu na usalama wa mahujaji wa Nyumba tukufu ya Mwenyezi Mungu kulizidi kudhihirika na kubainika kwa uwazi zaidi katika Hija ya mwaka uliopita wa 2015 ambapo Ulimwengu mzima wa Kiislamu ulibaini kuwa utawala huo hauna uwezo wowote wa kudhamini usalama wa maisha ya mahujaji.
Wapenzi wasikilizaji, sehemu ya pili ya kipindi maalumu cha Maafa ya Mina imefikia tamati. Ni matumaini yangu kuwa mumenufaika na yale mliyoyasikia katika kipindi chetu cha leo. La ziada sina ghairi ya kukuageni na kukutakieni usikilizaji mwema wa sehemu iliyosalia ya matangazo yetu…/
Kwa maelezo zaidi kuhusu Maafa ya Mina: http://kiswahili.irib.ir/habari/mina
Kwa maelezo zaidi kuhusu makala za Hija: http://kiswahili.irib.ir/uislamu/hija