Sep 08, 2016 16:27 UTC
  • Maafa ya Mina (8) Mwisho

Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Natumai hamjambo wapenzi wasikilizaji popote pale yanapokufikieni matangazo haya ya Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hususan hapo nyumbani Afrika Mashariki.

Karibu tena kujiunga nami katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Maafa ya Mina hii ikiwa ni sehemu ya nane na ya mwisho ya mfululizo huu. Karibuni

Katika kipindi kilichopita, tuliashiria kwamba, nchi nyingi ambazo zilipoteza Mahujaji wake katika Maafa ya Mina mwaka uliopita wa 2015, hazikufuatilia haki zao bali ni Jamhuri ya Kiislamu ya Iran tu ndio iliyokuwa mstari wa mbele katika hili. Hapana shaka kuwa, kufuatilia nchi moja pekee kuhusiana na kadhia hiyo ni hatua mabyo haitoshi. Bila shaka umewadia wakati sasa kwa utawala wa Saudi Arabia kufahamu kwamba,  kwa mujibu wa vigezo vya Kiislamu na sheria za kimataifa una jukumu na masuulia ya usalama wa Mahujaji, na unapaswa kutoa majibu ya matukio machungu kama Maafa ya Mina au kuanguka winchi katika Masjidul Haraam. Hata hivyo yumkini katika utawala wa kifalme na wa kidikteta kama Saudi Arabia ambako haki za awali za watu zinakanyagwa na katika uga wa kimataifa haufungamani na akthari ya sheria, jambo hilo likawa mushkili. Lakini pamoja hayo, serikali ya Saudia inapaswa kudiriki kwamba, kwa uchache ina jukumu na masuuliya muhimu mbele ya Mahujaji wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu wanaokwenda kutekeleza ibada tukufu ya Hija katika ardhi ya nchi hiyo.

 

Utawala wa Aal Saud unapaswa kutoa majibu ya tukio la MINA

Haki ya awali ya kila mwanadamu ni haki ya kuishi. Tunasoma katika kipengee cha pili cha hati ya haki za binadamu kwamba: “Maisha ni hiba ya Mwenyezi Mungu na haki ambayo amedhaminiwa kila mwanadamu na ni wajibu kwa watu wote wa jamii na tawala zote kuunga mkono haki hii na kusimama kukabiliana na kila aina ya uvamizi dhidi ya haki hii.”

Aidha katika kipengee cha tatu cha tangazo la kimataifa la haki za binadamu inaelezwa kuwa: “Kila mtu ana haki ya kuishi na ana haki ya kuwa na uhuru na usalama.”

Hata hivyo utawala wa Aal Saud nchini Saudi Arabia kutokana na kufanya uzembe katika kusimamia ibada ya Hija, hadi sasa umepelekea maelfu ya Mahujaji kukosa neema ya kuishi na viongozi wa utawala huo unapaswa kufungamana na ahadi zake za kisheria mkabala na uzembe huu. Hatua ndogo kabisa inayowezwa kufanywa na utawala wa Saudia ni kuziomba radhi familia za mashahidi na wahanga wa matukio ya maafa katika ibada ya Hija na kuzilipa fidia na wakati huo huo kuchukua hatua za kuzuia kukaririwa tena matukio machungu na ya kuhuzunisha kama hayo.

Mashahidi wa Mina

Hapana shaka kuwa, utawala wenye kiburi wa Aal Saud ambao daima umekuwa ukijitoa makosani na kuwatupia makosa wengine umekuwa haukubali kufungamana na sheria za Kiislamu na za kimataifa. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana Jamhuri ya Kiislamu ya Iran umeliweka katika ajenda zake sualala kuishtaki Saudia katika vyombo vya kimataifa. Bila shaka mashtaka haya yatakuwa na taathira chanya endapo nchi nyingine zilizopoteza Mahujaji wake katika Maafa ya Mina zitakuwa pamoja na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mashtaka hayo.

Hata hivyo inasikitisha kwamba, madola hayo hayajachukua hatua yoyote katika uwanja huo kutokana na satua na ushawishi wa Saudia. Hii ni katika hali ambayo, nchi hizo zina jukumu na masuuliya ya kulinda roho za raia wake.

Watawala wa Saudia sio tu kwamba, hawana uwezo wa kuandaa na kusimamia ibada ya Hija katika mazingira salama na ya amani, bali kwa uoni wa kisiasa na kidini hawana ustahiki wa kusimamia ibada ya Hija. Utawala wa Saudia unaendeshwa na familia ambayo inapuuza vigezo vilivyozoeleka vya kisiasa vya ndani na nje na inafanya juhudi za kusukuma mbele malengo yake kwa kutumia pesa. Kiasi kwamba, hivi sasa nchini Saudia hakuna demokrasia wala uhuru ambapo wanawake hawana ruhusa ya kuendesha magari huku Waislamu wa madhehebu ya Kishia wakikandamizwa nchini humo. Hayo yakiwa ni masuala ya ndani, kwa upande wa masuala ya nje, utawala wa Saudi Arabia umekuwa ukiingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine na hata kufanya hujuma na mashambulio ya kijeshi. Mfano wa hilo ni mashambulio ya kijeshi ya Saudia dhidi ya nchi ya Yemen. Saudia hufanya hayo na kupuuza malalamiko yoyote yale dhidi ya hatua zake hizo. Watawala wa Saudia wameibadilisha ibada ya Hija na kuifanya kuwa wenzo wa kusukuma mbele gurudumu la malengo ya siasa zao za kigeni; ambapo mwaka huu Mahujaji wa Iran, Syria na Yemen wamezuiwa kwenda kutekeleza ibada ya Hija.

Kwa upande wa kimadhehebu pia, utawala wa Saudia unafuata fikra potofu za na utumiaji mabavu za Kiwahabi. Kundi potofu la Mawahabi haliko tayari kustahamili mitazamo ya madhehebu mengine na Mawahabi nchini Saudia hawako tayari kuwapatia uhuru wa Kimadhehebu Mahujaji wanaoelekea nchini humo kutekeleza ibada ya Hija wakitokea katika nchi mbalimbali.

Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana mapolisi na maafisa usalama wa Saudia wamekuwa wakiamiliana vibaya mno na Mahujaji wa madhehebu mengine katika msimu wa ibada ya Hija na kupelekea kutokea mivutano baina yao. Kwa hakika   vitendo vya wana usalama hao chimbuko lake ni fikra mgando na zenye taasubi zinazotawala baina ya Mawahabi waliopotea njia ya haki.

Uwahabi

Kutokana na udhaifu wa utawala wa Saudia, inafahamika wazi kwamba, utawala huo hauna sifa na ustahiki wa kusimamia ibada ya Hija au viongozi wake kustahiki kuitwa kuwa ni wahudumu wa haramu mbili tukufu za Makka na Madina. Kwa miaka kadhaa sasa kwa kuzingatia kwamba, maeneo matukufu ya Makka na Madina ni mali ya Waislamu na sio miliki ya Saudia, baadhi ya makundi, shaksia na hata tawala zimekuwa zikitoa mapendekezo mbalimbali ili kuboresha usimamizi na uendeshaji wa ibada ya Hija.

Baadhi wanaamini kwamba, ili kuboresha uendeshaji wa ibada ya Hija, usimamiaji wake ufanyike kwa sura ya mzunguko baina ya nchi mbalimbali. Kundi jingine linaamini kwamba, kuna haja ya kuundwa kamati maalumu ikizijumuisha nchi za Kiislamu kwa ajili ya kusimamia ibada ya Hija. Aidha wataalamu wengine wa mambo katika ulimwengu wa Kiislamu wanaamini kwamba, ni bora jukumu la kusimamia ibada ya Hija likakabidhiwa Jumuiya ya Ushirikiano ya Nchi za Kiislamu OIC ambayo inaundwa na nchi zote za Kiislamu.

Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC

Alaa kulli haal, kwa kuzingatia maafa makubwa na machungu ya Mina mwaka jana na kuuawa zaidi ya Mahujaji elfu saba wa nyumba tukufu ya Mwenyezi Mungu ambapo sababu yake hasa ilikuwa ni uzembe wa utawala wa Saudia, utawala huo hauna tena sifa ya kusimamia ibada hiyo tukufu. Mwaka huu Mahujaji wana haki ya kuhisi kutokuwa na amani kuliko mwaka jana, hasa katika eneo la Mina na wana wasiwasi huenda wakati wowote likatokea tukio lisilo la kawaida. Hii ni kutokana na kutokuweko usimamizi sahihi na wa kustahiki wa ibada tukufu ya Hija.

Katika mazingira kama haya kuna haja ya suala la usimamiaji na uendeshaji wa ibada ya Hija kukakabidhiwa haraka iwezekanavyo kwa asasi ambayo ina sifa na ustahiki sambamba na ubunifu ambayo itawajibika kutoa majibu kwa vitendo vyake na matukio yatakayojitokeza katika ibada ya Hija.

Muda wa kipindi hiki umefikia tamati. Wapenzi wasikilizaji hii ilikuwa ni sehemu ya nane na ya mwisho ya mfulilizo huu wa vipindi vya Maafa ya Mina ambavyo vilichunguza matukio machungu ambayo yamekuwa yakitokea mara kwa mara katika msimu wa ibada ya Hija. Ni matumaini yetu vipindi hivi vimekunufaisheni na kukupeni mwanga kuhusiana na utawala wa Saudi Arabia.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh

Tags