Sep 08, 2016 09:48 UTC
  • Maafa ya Mina (7)

Huu ni mfululizo wa makala maalumu ambazo zinaangazia maafa ya kusikitisha yaliyojiri katika eneo la Mina mwaka jana wakati wa Ibada ya Hija. Hii ni sehemu ya saba ya mfululizo huu.

Katika makala zilizopita tumekuwa tukisimulia kisa cha kweli cha Haji Mohammad ambaye alishiriki katika ibada ya Hija mwaka jana na amekuwa akibainisha yale aliyoyaona kwa macho yake mwenyewe katika maafa ya Mina mwaka jana. Maafa hayo, sawa na tukio jingine chungu la kuanguka winchi au kreni katika Masjid al Haram katika eneo la Kaaba Tukufu mwaka jana ni mambo ambayo yalibainisha namna usimamizi mbovu umepelekea ibada muhimu ya Hija katika Uislamu kukumbwa na hali ya ukosefu wa usalama.

Matukio hayo ya kusikitisha ni dalili ya wazi kuwa utawala wa ukoo wa Aal Saud unaotawala ardhi ya Hijaz ambayo sasa ni Saudi Arabia, ni utawala ambao haustahiki kusimamia maeneo matakatifu ya Makka na Madina. Watawala wa Saudia ambao wanajiita eti kuwa ni wahudumu wa maeneo mawili matakatifu wameshindwa  kuleta utulivu na usalama katika ardhi hizo takatifu za Waislamu.

Ni miaka 84 sasa tokea uanzishwe utawala wa ukoo wa Aal Saud katika ardhi ya Hijaz. Ukoo wa Aal Saud ulinyakua madaraka ya Hijaz kwa msaada wa mkoloni Muingereza. Katika kipindi hicho chote cha miaka 84 ukoo wa Aal Saud haujaweza kupata njia muafaka za kudhamini usalama wa Mahujaji. Maafa ya Mina mwaka jana ni ishara ya wazi kuwa, pamoja na kuwepo ustawi mkubwa wa teknolojia ya habari na mawasiliano na pia maendeleo makubwa katika usimamizi wa maafa, watawala wa Saudi hawana uwezo wala hawastahiki kusimamia Ibada ya Hija. Maafa ya Mina yalijiri mwaka jana katika hali ambayo, idadi ya Mahujaji ilikuwa karibu nusu ikilinganishwa na mwaka uliotangulia kutokana na vizingiti vilivyokuwa vimewekwa na watawala wa Saudia.

Kuhusiana na maafa ya Mina mwaka jana, kuna maswali mengi ambayo yamebakia bila majibu. Utawala wa Saudia umetumia kiasi kikubwa cha fedha kujaribu kunyamazisha sauti zinazohoji kuhusu maafa hayo.

Msongamano eneo la Mina

 

Swali la kwanza linaloibuka ni hili kuwa, Je, ni kwa nini katika kipindi cha miaka kadhaa sasa Wasaudi wamekuwa wakidai kuwa wametumia kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya usimamizi wa Hija, lakini bado tunaendelea kushuhudia maafa katika eneo la Mina na bado utawala huo wa Saudia haujaweza kuandaa mazingira mazuri ya Mahujaji katika ardhi hiyo takatifu,?

Kuhusu maafa ya Mina mwaka jana ambapo Mahujaji zaidi ya 7,000 walipoteza maisha, bado kuna mambo mengi ambayo hayako wazi. Je, ni kwa nini maafisa wa usalama wa Saudia waliwaelekeza mahujaji Wairani katika barabara nambari 204, barabara ambayo ni nyembamba na yenye msongamano mkubwa, na pamoja na kuwa walikuwa wakiona yanayojiri kupitia kamera za usalama,  waliwaongoza Mahujaji wengine kutoka barabara za kando kujiunga na barabara hiyo nyembamba nambari 204?

Swali jingine ni hili kuwa, je, ni kwa nini maafisa wa Saudia walifunga barabara za pembeni ambazo zingeweza kutumiwa na Mahujaji waliokuwa wamesongamana katika barabara ya 204?

Katika hali ambayo miaka ya nyuma barabara kama hizo za pembeni zilikuiwa zikifunguliwa wakati wa msongamano lakini mara hii zilifungwa. Kama njia hizo zingefunguliwa, basi maafa kama ya mwaka jana Mina hayangejiri au idadi ya waathirika ingepungua.

Swali muhimu zaidi ni hili kuwa je, ni kwa nini wakuu wa Saudia walifunga sehemu ya mwisho ya barabara 204, eneo ambalo yalijiri maafa ya Mina? Tunaweza kusema kuwa, iwapo barabara hii ingekuwa wazi muda wote, basi maafa ya Mina hayangejiri.

Je, Mohammad bin Salman alisababisha maafa ya Mina?

Hakuna sababu yoyote ya kiakili au kimanatiki imetajwa kuhusu kufungwa mwisho wa njia hiyo. Habari zilizopo ni kuwa, Mwanamfalme Mohammad Bin Salman ambaye ni Naibu Mritihi wa Kiti cha Uflame na Waziri wa Ulinzi wa Saudia alikuwa katika eneo ambalo barabara ilifungwa. Inadokezwa kuwa Mohammad bin Salman akiwa na idadi kubwa ya walinzi wake, alikuwa amefika sehemu hiyo kujitayarisha katika amali ya Hija ya kumpiga mawe Shetani, na hivyo maafisa wa usalama walifunga mwisho wa barabara 204 eneo la Rami al-Jamarat ili mwanamfalme huyo asisumbuliwe na Mahujaji wengine.

Aidha utendaji kazi wa utawala wa Saudia wakati wa maafa ya Mina ni jambo ambalo limepelekea wengi kuingiwa na shaka. Wakati idadi kubwa ya Mahujaji walikuwa wanakanyagana huku kukiwa na jua kali na hivyo wengi wakiwa na kiu,  Wasaudi wangeweza kuwamiminia maji Mahujaji kwa helikopta au kwa njia nyinginezo ili kuokoa maisha ya idadi kubwa ya watu katika eneo hlo. Je, wasimamizi wa Hija Saudia hawakufahamu njia hiyo sahali ya kuokoa maisha?

Baada ya waokoaji kutoka nchi zinginezo kufahamu kumejiri maafa Mina, walifika katika eneo la tukio haraka iwezekanavyo. Lakini maafisa wa usalama wa Saudia waliwazuia kutoa huduma kwa waliokuwa wakizihitajia. Wakati waokoaji wa nchi zinginezo walipokuwa wakisisitiza kuwaokoa Mahujaji waliokuwa wakipoteza maisha, walifukuzwa kutoka eneo la tukio katika hali ambayo msaada wao ungeweza kuokoa maisha ya wengi.
Vituo viwili vya Saudia vya kutoa misaada vilikuwa karibu na barabara 204 huku idadi kubwa ya vituo vingine sawa na hivyo vikiwa kote Mina. Katika maafa hayo ya kibinadamu, wale ambao hufika eneo la tukio katika dakika za awali huwa ni waokoaji. Lakini waokoaji wa mashirika ya Saudia walichukua zaidi ya masaa mawili kufika eneo hilo baada ya maafa. Katika hali ambayo waokoaji kutoka nchi zingine walifika eneo la tukio kwa kasi, waokoaji wa Saudia walionekana kutojali hali ya Mahujaji. Badala yake maafisa wa usalama wa Saudia walijitahidi sana kusafisha eneo ili kuficha kiwango cha maafa hayo. Kwa msingi huo waliwakusanya kwa mabuldoza Mahujaji wote waliokuwa wameanguka chini kwa kukanyagwa wawe hai au walioaga dunia na kuwahamishia sehemu nyingine. Hapo wengi walipoteza maisha.  Aidha waliojeruhiwa hawakupata msaada wa kutosha wakiwa katika mahospitali.

Waokoaji Mina 

Tatizo lililofuata ni kuwa wakuu wa Saudia hawakushirikiana vizuri na wakuu wa misafara ya Hija kutoka nchi zingine katika kutambua miili ya waliokufa shahidi na hatimaye kusafirisha miili katika nchi zao. Ili kujaribu kuzuia kiwango cha maafa ya Mina kujulikana, wakuu wa Saudia walitaka miili yote izikwe Saudia katika makaburi ya umati. Saudia ilizilipa kiasi kikubwa cha fedha baadhi ya serikali ili ziache kufuatilia suala la Mahujaji wa nchi hizo waliopoteza maisha Mina. Nchi pekee ambayo ilifuatilia kadhia ya Mahujaji wake na kutetea haki zao ni Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Tehran inataka waliohusika na maafa ya Mina wafikishwe katika Mahakama ya Kimataifa na pia inaitaka Saudia iombe radhi na izilipe fidia familia za waliokufa shahidi Mina. Ni kutokana na msimamo huo imara ndipo wakuu wa Saudia wakawazuia Wairani kutekeleza ibada ya Hija mwaka huu.

Nukta hizo zote tulizotaja ni dalili za wazi kuwa ukoo wa Aal Saudi haustahiki na wala hauwezi kudhamini usalama wa mahujaji wa Nyumba ya Allah SWT. Hii ndio maudhui tutakayojadili katika makala yetu ijayo, panapo majaliwa yake Mola, kwaherini.