Tunisia yamwita Balozi wa EU ili ajieleze kwa kukiuka itifaki ya kidiplomasia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i133648-tunisia_yamwita_balozi_wa_eu_ili_ajieleze_kwa_kukiuka_itifaki_ya_kidiplomasia
Rais Kais Saied wa Tunisia amemwita Giuseppe Perrone, balozi wa Umoja wa Ulaya nchini humo na kumtaka ajieleze kwa kufanya uchochezi na kutoheshimu itifaki za kidiplomasia. Hayo yametangazwa na Ikulu ya Rais mjini Tunis.
(last modified 2025-11-27T05:58:34+00:00 )
Nov 27, 2025 05:58 UTC
  • Tunisia yamwita Balozi wa EU ili ajieleze kwa kukiuka itifaki ya kidiplomasia

Rais Kais Saied wa Tunisia amemwita Giuseppe Perrone, balozi wa Umoja wa Ulaya nchini humo na kumtaka ajieleze kwa kufanya uchochezi na kutoheshimu itifaki za kidiplomasia. Hayo yametangazwa na Ikulu ya Rais mjini Tunis.

Katika taarifa iliyochapishwa kwenye ukurasa wake wa Facebook, Ikulu ya Rais wa Tunisia imesema kuwa, Rais  Kais Saied amemkabidhi mwakilishi huyo wa EU malalamiko ya Tunisia yenye maneno makali kutokana na balozi huyo kuchukua hatua zisizochunga itifaki za kidiplomasia dhidi ya Tunisia.

Hatua hiyo imekuja kufuatia mkutano uliofanyika Jumatatu kati ya balozi wa EU Giuseppe Perrone na Noureddine Taboubi, katibu mkuu wa Chama Kikuu cha Wafanyakazi cha Tunisia (UGTT), ambacho ni chama kikubwa zaidi cha wafanyakazi katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Uhusiano kati ya serikali ya Tunisia na chama cha wafanyakazi cha UGTT umekuwa mgumu katika wiki za hivi karibuni baada ya Taboubi kutangaza kwamba chama hicho kinapanga kuandaa mgomo mkuvwa ili kutetea haki za wafanyakazi kutokana na hali mbaya ya maisha ya wanachama wake.

Taarifa zilizotolewa na Umoja wa Ulaya zimethibitisha kufanyika mazungumzo baina ya Perrone na Taboubi na kusema kwamba EU itaendelea kufanya mazungumzo na UGTT kwa kile ilichodai ni kuwaunga mkono wananchi wa Tunisia katika sekta mbalimbali.

Vilevile Umoja wa Ulaya umekipongeza chama cha wafanyakazi wa Tunisia UGTT kwa kile ulichokiita ni kubeba jukumu chama hicho katika kukuza mazungumzo ya kijamii na kuchangia maendeleo ya kiuchumi nchini Tunisia.