Hadithi ya Uongofu (52)
Ni wasaa na wakati mwingine na wakati mwingine wapenzi wasikilizaji wa kujiunga nami katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. Kipindi chetu cha wiki hii ambacho ni sehemu ya 52 kitazungumzia Jihadi ya Nafsi au kupigana jihadi na nafsi. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi.
Kupigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu ni moja ya nguzo za dini ya Kiislamu. Katika Qur'ani na hadithi kumetajwa fadhila nyingi za kufanya jihadi.
Jihadi maana yake ni kujitolea roho na mali katika njia ya Mwenyezi Mungu na katika vita na adui. Kwa hakika katika kipindi chote cha maisha hapa duniani, mwanadamu hukumbana na anuai ya maadui. Adui wa nje na adui wa ndani. Watu ambao wanakanyaga na kupora haki za wengine, wanafanya dhulma na ukandamizaji na kufunga njia ya uja kwa Mwenyezi Mungu, hawa wanahesabiwa kuwa ni maadui wa nje. Lakini adui wa ndani ni shetani ambaye anatia wasiwasi katika vifua vya watu na humshambulia mwanadamu akipata msaada wa nguvu ya matamanio ya nafsi. Na pindi anaposhinda nguvu ya akili ya mwanadamu humfanya mwanadamu huyo kuwa mtumwa wa dhambi na matamanio ya nafsi yake. Vuta nikuvute hii kati ya mwanadamu na ushawishi wa shetani unaomvuta kutenda dhambi ambavyo kimsingi ni vita kati ya wawili hawa hujukana kuwa ni kupigana jihadi ya nafsi na jihadi hii inatajwa katika Uislamu kuwa ni Jihad al-Akbar yaani Jihadi Kubwa.
Kwa hakika, roho ya mwanadamu ni eneo na uwanja wa vita na mapambano ya nguvu mbili zinazovutana na kushindana. Nguvu ya Mungu humvutia mtu kwenye nyanja ya mbinguni, na kumhamasisha kwenye matendo ya wema. Huku nguvu za kishetani humshawishi kuelekea maeneo ya giza na aibu, na kumualika kwenye matendo maovu. Wakati nguvu ya Mungu inapopata ushindi, mtu anaibuka na kuwa mwema na mpole, huwa katika ufuasi wa Mtume (S), huwa miongoni mwa watu wa Mungu, na wacha Mungu. Aidha vikosi vya kishetani vinampomshinda mtu anakuwa muasi na muovu na kuwa katika kundi pamoja na makafiri, madhalimu, watenda maovu na wale ambao wamelaaniwa.
Neno Jihadi ya Nafsi kwa mara ya kwanza lilitajwa wakati kundi la Maswahaba wa Mtume Muhammad SAW liliporejea Madina kutoka katika vita vya jihadi. Baada ya Maswahaba hao kufika kwa Mtume SAW, mbora huyo aliwapongeza kwa kutekeleza vyema jukumu walilokuwa wamepatiwa kwa kuwambia:
"Hongereni sana, hongera kwa wale ambao wamerejea kutoka katika vita vidogo na mbele yao vimebakia vita vikubwa." Maswahaba wakashangaa na wakamuuliza Mtume SAW: Ewe mjumbe wa Mwenyezi Mungu, hivyo vita vikubwa ni vipi? Mtume akawajibu kwa kuwaambia: Vita vikubwa ni kupigana jihadi na nafsi. Kisha Mtume SAW akabainisha kwa kusema:J ihadi Kubwa kabisa ni mtu kupambana na nafsi yake.
Tukiitazama kwa makini hadithi hii ya Bwana Mtume SAW tutaona kuwa, kupambana na nafsi na kuizuia isikupeleke katika kumuasi Mwenyezi Mungu yaani huyu adui wa ndani, ni jambo lenye kipaumbele zaidi ikilinganishwa na kupambana na adui wa nje. Tab'an, kupambana na adui wa nje huitwa kuwa ni jihadi pale tu hilo linapofanyika kwa ajili ya kutaka radhi za Mwenyezi Mungu na kuwasambaratisha madhalimu na wakandamizaji.
Mujahidi wa Kiislamu katika mapambano haya ya kutaka radhi za Mwenyezi Mungu kwanza anapaswa yeye mwenyewe awe ameitakasa nafsi yake, amevumilia magumu yote na kuuweka hatarini uhai wake. Mtu wa aina hii anakuwa ameacha mfungamano wake na dunia na jambo hili kwa hakika ni katika misdaqi na mifano ya wazi ya Jihad al-Akbar yaani Jihadi Kubwa.
Mintarafu hiyo, kabla ya Mujahidi yaani mpiganaji katika njia ya Mwenyezi Mungu hajaingia katika medani ya vita vidogo yaani vya kupambana na adui wa nje, kimsingi anakuwa ameingia katika vita vikubwa. Hata hivyo tofauti ya vita hivi viwili ni kwamba, Jihad al-Asghar yaani Jihadi Ndogo au vita vidogo ni vita na jihadi ya muda maalumu na adui wa nje anapomalizwa na kusambaratishwa basi vita hivyo navyo huwa vimekwisha na kufikia tamati. Lakini Jihad al-Akbar ni vita vya daima na vya kila baada ya muda; na adui daima huwa ni mwenye kushambulia mpaka mwisho wa umri wa mwanadamu na hakuna wakati ambao anamuacha mwanadamu apumue.
Kwa hakika mtu ambaye amekuwa mtumwa na mateka wa matamanio ya nafsi, ili aweze kufikia katika kheri, ukweli na kuweza kurekebisha batini yake, anapaswa kuingia katika medani ya vita kama mpiganaji shujaa na mwenye nguvu na hivyo kupambana na matamanio ya nafsi yake. Mtu huyu anapaswa kutambua kwamba, katika vita hivi, msaada wa Mwenyezi Mungu, rehma na mapenzi ya Allah yako pamoja naye na vinampa muongozo ili aweze kupata ushindi kwa kufuata mafundisho ya Mitume wake.
Abu Dhar al-Ghifari, mmoja wa masahaba wema na mashuhuri wa Bwana Mtume SAW anasema kuwa:
Siku moja niliingia msikitini na kumwendea Bwana Mtume SAW. Msikitini hapo bighairi ya Mtume SAW na Ali AS hakukuweko na mtu mwingine. Nikatumia fursa hiyo ya kuwa tupu msikiti, hivyo nikwamwendea Mtume na kumwambia: Ewe Mtume wa Allah! baba na mama yangu wawe fidia kwako…naomba uniusie na kunipa muongozo ili kupitia hilo Mwenyezi Mungu anifaidishe. Mbora huyo wa viumbe akasema: Ni vizuri kiasi gani ewe Abu Dhar! Ninakupa muongozo na ujifunze vizuri hili. Wasia na nasaha ambazo ni chimbuko la njia na mikakati yote ya kheri na manbo mazuri. Endapo utajifunza hilo na ukalilinda, basi hilo litakuwa mithili ya mbawa mbili ambazo zinakusaidia wewe wakati wa kupaa. Kisha akasema: Ewe Abu Dhar! Mtu mjanja na mwenye akili ni yule aipuuzaye nafsi na anayefanya juhudi kwa ajili ya baada ya kufariki kwake dunia, na asiyejiweza ni mtu ambaye anafuata matamanio ya nafsi na kisha anaomba mambo mengi (ana matarajio mengi) kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Kupigana jihadi na matamanio ya nafsi ni jihadi yenye thamani kubwa kuliko jihadi nyingine yoyote ile na mwisho wa siku ni mja anayefanya hivyo kupata ujira mnono na mkubwa.
Imam Ali bin Abi Twalib AS amesema kuwa, ujira wa mpiganaji aliyeuawa shahidi katika njia ya Mwenyezi Mungu haumzidi mtu ambaye alikuwa na uwezo wa kufanya dhambi lakini akajizuia kufanya hivyo.
Hivyo basi kabla mja hajatingwa na matamanio ya nafsi na kuwa mtumwa wa sanamu hili hatari, daima anapaswa kumdhukuru na kumtaja Mwenyezi Mungu na ajilinde na uchafu wa dhambi ambapo kuilinda nafsi ni mithili ya utukufu na hupelekea kuimarika roho ya mwanadamu.
Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu cha Hadithi ya Uongofu unafikia tamati kwa leo. Tukutane tena wiki ijayo.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh