Hadithi ya Uongofu (55)
Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. Juma hili kipindi chetu hiki ambacho ni sehemu ya 55 ya mfululizo huu kitazungumzia mghafala au usahaulifu pamoja na dalili zake. Tafadhalini kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki. Karibuni.
Mghafala au usahaulifu na kughafilika ni miongoni mwa balaa hatari ambayo yamkini ikamkumba mtu yeyote na hivyo kumfanya akose saada na ufanisi wa duniani na akhera. Kuna wakati mwanadamu kutokana na mghafala na kughafilika kwake hupoteza rasilimali yake yote. Wakati mwingine kutokana na mtu kughafilika kidogo tu hupata ajali ambayo humpelekea apoteze uzima wa mwili na kupatwa na kilema cha maisha au hata kupoteza maisha yake. Huu ni upande wa mambo ya kidunia; amma kwa upande wa masuala ya akhera uwezekano huo upo pia. Kwa maana kwamba, yamkini mwanadamu kutokana na mghafala na usahau akapoteza akiba yake yote ya kimaanawi kwa lahadha moja na hivyo kuangukia katika korongo la upotovu na dhalala.
Imam Ali bin Abi Twalib AS amesema: Mghafala ni chimbuko la upotevu na dhalala.
Katika madhumuni ya hadithi nyingine kutoka kwa Imam Ali AS, kiongozi huyo wa wacha Mungu anawausia watu kwa kuwaambia kwamba, kama ni wenye kutafuta wokozi na ukweli, basi waachane na mghafala na washikamane na juhudi na idili.
Kwa hakika mghafala ni hatari na wenye madhara makubwa kwa moyo. Moyo ulioghafilika ni moyo ambao uko mbali na Wahyi wa Mwenyezi Mungu pamoja na mafundisho ya Manabii, Maimamu na watu wenye busara wa Mwenyezi Mungu.
Kughafilika na Mwenyezi Mungu ni chimbuko la mtu kujisahau mwenyewe na hilo linatajwa kuwa sababu kuu ya dhambi zote na kutumbikia katika maadili machafu. Mghafala na usahaulifu humvuta mwanadamu upande wa kuporomoka.
Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 179 ya Surat al-A'raf:
Na tumeiumbia Jahannamu majini wengi na watu. Wana nyoyo, lakini hawafahamu kwazo. Na wana macho, lakini hawaoni kwayo. Na wana masikio, lakini hawasikii kwayo. Hao ni kama nyama howa, bali wao ni wapotofu zaidi. Hao ndio walio ghafilika.
Aya hii inaonyesha kwamba, pindi watu wanapokumbwa na mgahafala basi masikio yao huwa hayasikii, macho nayo hayaoni huku wakishindwa kuzitumia nyoyo zao kufahamu mambo.
Mintarafu hiyo, mghafala au kughafilika ni adui ambaye anaweza kumpokonya mwanadamu utu wake na kumfikisha katika daraja ya mnyama bali hata kumfanya kuwa mbaya kuliko mnyama. Ni kwa kuzingatia ukweli huo ndio maana Imam Ali bin Abi Twalib AS anautaja mghafala na kughafilika kwamba, ni adui mkubwa wa mwanadamu.
Mghafala au usahau ni moja ya misiba mibaya kabisa. Mwenye aliyeghafilika ni mithili ya mtu aliye usingizini huku nyumba yake ikiwa inaungua moto ilihali yeye hana habari kwamba, nyumba yake inaungua na roho na maisha yake yako hatarini.
Imam Ali AS anawazungumzia wale wenye kuitafuta dunia hali ya kuwa wameghafilika. Anasema: Watu wenye kuipenda dunia ni mithili ya watu walioko katika msafara hali ya kuwa wako usingizini. Wakati wanapofungua macho wanakuta kwamba, loo wameshachelewa, kwani umri umekwenda ilihali hawajanufaika na johari ya utu na ubinadamu.
Mtume SAW amenukuliwa katika maneno yake yaliyojaa hekima wakati alipokuwa akiwatambulisha watu walioghafilika kwamba, ni watu wa aina gani pale aliposema:
Ishara na dalili za mtu aliyeghafilika ni vitu vinne: Upofu ambao ni ile hali ya kufumbia macho ukweli, kusahau, kujihusisha na mambo ya kipuuzi na kukumbwa na mghafala; yaani kutumbukia katika usahaulifu na kujipumbaza na matamanio na kutozingatia hatima na majaaliwa yao.
Ishara nyingine muhimu za mghafala ni kupuuza ishara za maonyo na thadhari ambazo humzindua mtu. Kwa mfano walioghafilika pindi wanapopita karibu na makaburi hawafikiri kwamba, yamkini kesho hayo ndiyo yakawa makazi yao au wakati wanaposindikiza maiti ya mmoja wa watu wanaowafahamu kwa ajili ya mazishi husahau kwamba, kuna siku na yeye watu watashiriki katika maziko na mazishi yake.
Ishara nyingine ya kughafilika ni mtu kutumia muda na umri wake katika mambo ambayo hayana sudi wala faida yoyote ile kwa akhera yake, au kujishughulisha na mambo ambayo hayana faida hata kwa dunia yake.
Imam Ali AS anasema: Mghafala kwa mwanadamu unamtosha pale anapopoteza umri wake katika vitu ambavyo havimsaidii chochote katika wokozi wake.
Moja ya ishara nyingine za mghafala na kughafilika ni mtu kuwa na kiburi. Mtu mwenye kiburi hujiona yeye ndiye bora kuliko wengine na hujikweza. Kwa hakika mtu huyu ameghafilika na Mwenyezi Mungu kwani hafahamu kwamba, kiburi ni sababu kuu ya mja kuporomoka.
Kwa mfano, usalama wa mwili na viungo vyake kama roho na kadhalika, licha ya kuwa ni moja ya ujazi na neema za Mwenyezi Mungu, lakini endapo mtu anajitia kiburi na kutokana na kupewa viungo salama vya kimwili na akajiona na hata pengine kumdharau kilema, huhesabiwa kuwa, ameghafilika. Ni kutokana na sababu hiyo, wakati mwigine Mwenyezi Mungu akiwa na lengo la kuondoa kiburi na hali ya kujiona ya mja, humpa mtihani wa maradhi au maumivu ya mwili. Maradhi na maumivu hayo huondoa pazia la mghafala na kumzindua yule mwenye kujiona kutokana na kuwa na mwili salama.
Tunakamilisha kipindi chetu cha leo kwa kisa kifupi kifuatacho. Siku moja Bwana Mtume SAW alimtembelea mmoja wa maswahaba wake watukufu yaani Salman al-Farsi ambaye alikuwa mgonjwa kitandani. Baada ya kumjulia hali na kumuombea apone haraka, mbora huyo wa viumbe alitumia fursa hiyo kutaja athari na baraka anazozipata mtu wakati akiwa mgonjwa au mwenye kukabiliwa na maumivu. Mtume SAW alisema kumwambia Salman al-Farsi:
Wakati wa maumivu na maradhi kuna neema ambazo unazipata: Moja ya neema hizo ni kwamba, unamkumbuka Mwenyezi Mungu na pazia la mghafala huondoka. Ni kwa sababu hiyo ndio maana dua yako hukubaliwa.
Muda wa kipindi chetu umefikia tamati, basi hadi tutakapokutana tena juma lijalo ninakuageni nikikutakieni kila la kheri.