Hadithi ya Uongofu (56)
Ni wasaa na wakati mwingine mpenzi msikilizaji tunapokutana tena katika kipindi kingine cha Hadithi ya Uongofu, kipindi ambacho hujadili maudhui mbalimbali za kidini, kijamii, kimaadili na kadhalika na kukunukulieni hadithi zinazohusiana na maudhui hizo. Kipindi chetu cha leo kitaendelea kujadili maudhui ya mghafala au kughafilika pamoja na athari zake au matokeo yake, maudhui ambayo tulianza kuijadili katika kipindi chetu kilichopita.
Tafadhali kuweni nami hadi mwisho wa dakika hizi chache kutegea sikio yale niliyokuandalieni kwa juma hili, hii ikiwa ni sehemu ya 56 ya mfululizo huu.
Moja ya matatizo makubwa ya mwanadamu ni mghafala na usahaulifu. Kama tulivyogusia katika kipindi kilichopita ni kwamba, mghafala umegwanyika katika makundi kadhaa; hata hivyo mtu "kughafilika na nafsi" yake ni aina ya mghafala wenye madhara makubwa zaidi kuliko mighafala mingine. Hii ni kutokana na kuwa, mtu aliyeghafilika na nafsi yake husahau thamani, vipaji na ustahiki wa dhati na wa kifitra ambao Mwenyezi Mungu amemtunuku na kumfanya awe na sifa maalumu mbele ya viumbe wengine. Hali hii humfanya mja huyo aporomoke na kufikia hatua ya mnyama; na hima na idili yake haiwi isipokuwa kwa ajili ya kujaza tumbo, kulala na kushibisha matamanio yake.
Kwa hakika mtu kama huyu atadhibitiwa na kutawaliwa na shetani. Aya ya 36 ya Surat Zukhruf
"Anaye yafanyia upofu dhikri ya Mwingi wa rehma tunamwekea Shet'ani kuwa ndiye rafiki yake."
Kwa msingi huo mghafala humuweka mbali mtu na Mwenyezi Mungu na adui aliyekula kiapo yaani shetani humdhibiti mja huyo aliyeghafilika na Mwenyezi Mungu.
Imam Ja'afar Swadiq (as) anasema kuwa: Mghafala ni mtego wa shetani.
Kwa hakika mghafala ni sababu ya hilaki na maangamizo duniani na akhera. Kughafilika mtu na uwezo, nguvu na maslahi yake humfanya asiwe na khabari huku vipaji vyake vikitokomea na kuangamia kabla ya kukua na kustawi. Mghafala au usahau hupelekea kupotea fursa na huteketeza suhula.
Imekuja katika sehemu ya hadithi ya Mi'raji ya Mtume (saw) kwamba, Mwenyezi Mungu alimwambia Mtume wake kuwa, "usighafilike na mimi kwani kila atakayeghafilika na mimi sijali ataangamia wapi.
Kwa hakika mghafala hufuatiwa na ugumu wa roho. Aidha ugumu wa moyo na roho huifanya roho hiyo kufa, kiasi kwamba, hakuna mawaidha na nasaha yoyote ambayo itakuwa na athari kwa moyo wa aina hiyo. Mtu wa aina hii hufungiwa mlango wa marejeo na toba na aina yoyote ile ya matumaini kwa ajili ya saada hutokomea. Imam Ali bin Abi Twalib (as) anasema kuwa: Mtu anayekumbwa na mghafala moyo wake hufa.
Aidha amesema katika hadithi nyingine kwamba: Baina yenu na mawaidha au nasaha kuna kizuizi cha mghafala na ghururi.
Vile vile Kiongozi huyo wa Waumini amenukuliwa akisema: Kuendelea na kudumu hali ya mghafala na usahau, ni jambo ambalo huufanya uono wa mtu kupofuka.
Kwa hakika mghafala hupelekea pia amali na matendo ya mtu kufisadika. Watu ambao wana mgahafala na usahaulifu ni mara chache sana hujishughulisha na amali njema na kama wakielekea upande wa kufanya amali njema, basi mghafala walionao huwazui kuzifanya amali hizo kuwa ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na kwa kuwa na mahudhurio ya moyo sambamba na kutekeleza masharti yote yanayopaswa kwa ajili ya amali njema ambayo ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu Mola jalia.
Vile vile mghafala hupelekea kutumbikia katika dhambi; na dhambi ni sababu ya kutoweka amali njema za mja. Imam Ali (as) anasema katika Nahaj al-Balagha kwamba: Kila ambaye aliichunga nafsi yake alifaidika na aliyeghafilika alipata madhara. Aidha amenukuliwa akisema pia kwamba, Mghafala hupelekea mtu kuhadaika na humkurubisha mtu kwenye hilaki na maangamio.
Moja ya natija nyingine ya kughafilika na Mwenyezi Mungu ni kuwa na mwelekeo wa kidunia na kuikumbatia dunia. Watu ambao wanaghafilika na Mwenyezi Mungu na ishara zake ulimwenguni na kuiona dunia ndio asili na kila kitu, hawana muelekeo au imani kamili na Siku ya Kiyama, Siku ya Hesabu na suala la kwamba, kila mwanadamu atakabidhiwa kitabu cha amali zake. Na ndio maana watu wa aina hii wamezama na kughiriki katika masuala ya dunia na starehe zake. Juhudi zote za watu wa namna hii ni kuhakikisha kwamba, wananufaika na dunia na vilivyomo. Ni kwa muktadha huo, ndio maana masuala kama dhulma, kukanyaga na kupora haki za wengine kwao wao ni jambo la kawaida kabisa. Qur'ani Tukufu inataja moja ya sababu za mja kukumbwa na mghafala na usahaulifu kuwa ni kuipenda dunia na kuikumbatia. Kwa maana ya kushughulishwa na dunia na vilivyomo kupita kiasi.
Aya ya Saba ya Surat Yunus inasema:
Hakika wasio taraji kukutana nasi, na wakaridhia maisha ya dunia na wakatua nayo, na walio ghafilika na Ishara zetu. Hao, makaazi yao ni Motoni kwa sababu ya waliyo kuwa wakiyachuma.
Imam Hassan bin Ali bin Abi Twalib (as) anasema: Mtu ambaye ni muumini hafanyi amali ambayo haina faida isipokuwa anapokuwa ameghafilika.
Wapenzi wasikilizaji mghafala au kughafilika ni aina nyingine ya kikwazo kinachozuia akili ya mwanadamu kukua. Imam Ali bin Abi Talib (as), Imam wa kwanza katika mlolongo wa Maimamu kumi na mbili wa madhehebu ya haki ya Shia anasema kuwa, endapo mghafala utamshinda mtu na kumdhibiti, basi moyo, akili, roho na batini yake hufa na kutofanya kazi."
Aidha anasema: Daima mkumbukeni Mwenyezi Mungu kwani hiyo ni dhikri bora kabisa.
Kwa hakika kutokana na kuwa, sababu zinazopelekea mtu kughafilika au kukumbwa na mghafala ni nyingi mno katika maisha ya kimaada na vishawishi vya shetani vimemzingira mwanadamu huyu kutoka kila upande, ili kujiokoa, njia bora kabisa ni kuomba hifadhi kwa Mwenyezi Mungu au kujinga na Allah na kumtaja na kumkumbuka Muumba.
Hata hivyo tunapaswa kutambua kwamba, kumtaja na kumkumbuka Mwenyezi Mungu ni kufanya kila kazi na amali njema, iwe ni katika kumuabudu Mola Muumba au katika uwanja wa kutoa huduma kwa wanadamu.
Imepokewa hadithi kutoka kwa Bwana Mtume (saw) ya kwamba amesema: Mwenye kumtii Mwenyezi Mungu amemtaja na kumdhukuru Muumba, hata kama Swala, Funga na kusoma kwake Qur’ani kutakuwa ni kuchache; na mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu amemsahau Muumba, hata kama Swala, Funga na kusoma kwake Qur’ani kutakuwa ni kwingi.”
Wapaenzi wasikilizaji, muda wa kipindi chetu kwa juma hili umefikia tamati, tukutane tena wiki ijayo siku na wasaa kama wa leo.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh…