Hadithi ya Uongofu (57)
Ni wasaa na wakati mwingine wapenzi wasikilizaji wa kuwa nami katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. Vipindi vyetu kadhaa vilivyopita vilizungumzia matamanio ya nafsi na tulisema kuwa, kufuata hawaa na matamanio ya nafsi ndio kikwazo kikubwa katika njia ya saada na ufanisi wa mwanadamu. Aidha kusalimu amri kibubusa mbele ya matamanio na matakwa ya nafsi ndio adui mkubwa wa saada ya kiumbe mwanadamu.
Hata hivyo tulisema kuwa, katika hili, shetani ana nafasi kubwa katika kumhadaa na kumrubuni mwanadamu. Kuweni nami katika sehemu hii ya 57 ya mfululizo huu ambapo tutanukuu baadhi ya hadithi kuhusiana na shetani pamoja na sifa zake. Karibuni.
Sifa kuu ya shetani ni kiburi na kutakabari. Shetani ndiye aliyekuwa wa kwanza kupinga amri ya Mwenyezi Mungu. Imam Ja'afar Swadiq AS mjukuu wa Mtume SAW anasema: "Kutakabari ni dhambi ya kwanza aliyoasiwa Mwenyezi Mungu." Kisha Imam anaendelea kusema kuwa, Ibilisi alimwambia Mwenyezi Mungu nisamehe kumsujudia Adam, halafu nitakuabudu kwa namna ambayo hakuna Malaika aliyekurubishwa wala Nabii Mursali ambaye amekuabudu namna hiyo. Kisha Mwenyezi Mungu akasema: "Mimi sina haja ya ibada yako, ibada ni ile ambayo mimi nakutaka uifanye na sio ile unayotaka kuifanya wewe.
Mwenyezi Mungu anaashiria mkasa wa kiburi na takaburi ya shetani katika aya ya 34 ya Surat al-Baqarah kwa kusema:
Na tulipo waambia Malaika: Msujudieni Adam, wakamsujudia wote, isipo kuwa Iblis, alikataa na akatakabari na akawa katika makafiri.
Kuhusiana na aya hii Mtume SAW alimwambia Abu Dhar al-Ghifari mmoja wa Masahaba zake mashuhuri kwamba:
" Ewe Abu Dhar! Mtu ambaye atafariki dunia hali ya kuwa katika moyo wake kuna chembe ya kiburi, hatanusa harufu ya pepo, isipokuwa kama atatubu kabla ya kufariki kwake dunia. Ewe Abu Dhar! Watu wengi ambao wataunguzwa katika moto wa Jahanamu ni wale wenye kiburi."
Aidha imekuja katika kitabu cha Nahaj al;-Balagha katika kubainisha aya ya 34 ya Surat al-Baqarah tuliotangulia kuisoma kwamba: " Chukua ibra na mazingatio kupitia muamala wa Mwenyezi Mungu kwa Ibilisi.
Kutokana na kiburi alichokionyesha Iblisi mbele ya Allah, Mwenyezi Mungu alizibatilisha ibada zake na uja wake kwa Allah uliodumu kwa miaka elfu 6.
Hivyo basi ni nani baada ya Iblis ambaye atasalimika na hukumu ya Mwenyezi Mungu kwa kufanya maasi yale yale? La hasha! Katu haiwezekani Mwenyezi Mungu amuingize peponi mtu kwa amali ile ile ambayo kwayo amemfukuza Malaika kutoka peponi. Amri za Mwenyezi Mungu ni za namna moja kwa watu wote.
MUZIKI
Moja ya sifa nyingine za shetani ni kumzuia mtu kufanya amali za kheri na mambo mema. Kwani anatambua kwamba, amali njema na kufanya mambo mema hupelekea mwanadamu kuondolewa dhambi na mambo machafu. Ni kwa kuzingatia ukweli huo, ndio maana shetani kutokana na uadui alionao kwa wanadamu hufanya juhudi za kuzuia kufanyika amali za kheri za mtu binafsi na jamii kwa ujumla.
Imam Ja'afar Swadiq AS anazungumzia umuhimu wa amali njema na kuwatendea wema watu wengine kwa kusema: " Fanyeni hisani na wema kadiri mnavyoweza, kwani hakuna wema na msaada wa waumini isipokuwa humkasirisha shetani na kumkwarua uso na kumjeruhi moyo wake.
Moja ya matendo ya shetani ni kwamba, hurembesha matendo machafu mbele ya mwanadamu na kuyaonyesha kuwa ni mazuri. Aya nyingi katika Qur'ani Tukufu zimemkumbusha na kumtanabahisha mwanadamu kuhusiana na suala hili.
Kwa mfano aya ya 63 ya Surat an-Nahl inasema:
Wallahi! Sisi tulituma Mitume kwa umati zilizo kuwa kabla yako, lakini Shetani aliwapambia vitendo vyao. Kwa hivyo leo yeye ndiye rafiki yao; nao watapata adhabu chungu.
Kikawaida shetani hutumia vibaya mghafala na ujahili wa mtu na kulipamba kosa la mtu kwa pambo la dini na kwa msingi huo humnasa mja huyo katika mtego wake. Imam Ali bin Abi Twalib AS anasema kuwa: "Watu waliopotea wamemfanya shetani kuwa kigezo chao na shetani amewafanya watu hao kuwa windo lao. Kwa msingi huo ameweka mayai katika nyoyo zao na kulea vifaranga vyake katika mapaja yao. Na akapenya taratibu katika hekima na busara zao. Shetani hulia kwa macho yao na huzungumza kwa ndimi zao. Hivyo basi, shetani amewatumbukiza katika makosa na hali ya kuteleza na kukosea, na ameyafanya matendo mabaya kuwa mazuri mbele ya macho yao…"
Moja ya matendo mengine ya shetani kwa ajili ya kumhadaa mtu ni ucheleweshaji na uakhirishaji wa mambo. Kuchelewesha na kuakhirisha kazi ya kheri na kuahidi kuifanya kesho; na kesho ikifika huaikhirisha hasa katika kufida makosa kama vile kufanya toba au kutekeleza haki za watu, ni moja ya mitego ya shetani. Shetani daima huwashawishi watu kwa fikra kama hii bado fursa ipo, na hivyo mtu kusema, aa bado sijachelewa nitaifanya amali hii ya kheri, au ya toba baadaye kwani nina muda wa kutosha.
Kikawaida mtu wa namna hii huwa amehadaiwa na shetani kwani siku zote huwa namna hiyo na kukosa huo muda wa kufanya jambo hilo la kheri na kwa mintarafu hiyo huzidi kupoteza fursa siku baada ya siku. Katika hili shetani hutumia vyema fursa ya uvivu, udhaifu wa irada ya watu pamoja na hali ya kupenda raha waliyonayo baadhi ya watu kwa ajili ya kufikia malengo yake.
Kwa hakika mwanadamu anapaswa kutambua kwamba, kuna wakati anapotaka kusema au kutenda jambo fulani la haki, shetani humshawishi katika nafsi yake na kutaka kumuonesha kwamba, jambo analotaka kulisema litampunguzia heshima yake. Lakini la msingi ni kwamba, mwanadamu anapaswa kuelewa kuwa, kusema neno la haki hata kama kidhahiri ni kuchungu au hata huenda kusimpendeze anayeambiwa haki hiyo, lakini atapata izza na heshima ya Mwenyezi Mungu kwa kusema haki.
Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 98 ya Surat Nahl:
"Na ukisoma Qur'ani mwombe Mwenyezi Mungu akulinde na Shetani maluuni."
Kuomba ulinzi na hifadhi ya Mwenyezi kutokana na shetani, ni amri ya Mwenyezi Mungu kwa wasomaji wa Qur'ani na Mtume SAW kabla ya kusoma Qur'ani alikuwa akikariri maneno haya:
اعوذبالله من الشّیطان الرّجیم
Yaani "Najilinda na Mwenyezi Mungu kutokana na shetani aliyelaaniwa". Tab'an kujilinda kunapaswa kufanyika kwa sura ya kweli ili iwe na athari.
Muda wa kipindi chetu kwa juma hili umefikia ukingoni, msikose kujiunga name katika sehemu nyingine ya mfululizo huu, wiki ijayo ninakuageni nikikutakieni kila la kheri maishani.
Wassalaamu Alaykum Warhmatullahi Wabarakaatuh