Hadithi ya Uongofu (59)
Assalaamu alaykum wapenzi wasikilizaji. Tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. Vipindi vyetu kadhaa vilivyotangulia tulimzungumzia shetani pamoja na njia za kukabiliana na kiumbe huyu aliyeapa kuwapotosha wanadamu.
Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 59 ya mfululizo huu, kitanukuu hadithi na baadhi ya njia nyingine za kukabiliana na shetani. Ni matumaini yangu kuwa, mtakuwa nami hadi mwisho wa dakika hizi chache kutegea sikio niliyokuandalieni kwa leo.
Kwa hakika shetani rajimi kiumbe ambaye alikula kiapo cha kufanya kila awezalo kuhakikisha kwamba, anawapotosha wanadamu, ni mwenye kuwaandama waja wa Mwenyezi Mungu akitumia mbinu mbalimbali na anataka ahakikishe kwamba, anawavuta watu wote katika dhalala na upotovu. Njia yake anayotumia kuwaathiri watu wawe pamoja naye ni ya kifikra. Shetani humshawishi mwanadamu na kumpendezesha kazi mbaya ili aziona ni nzuri. Wataalamu wa mambo wanaamini kwamba, shetani huridhiriki hata na mghafala mdogo kabisa wa mtu na hufanya bidii akitumia mghafala na usahau huo wa mja kwa ajili ya kuhakikisha kwamba, anafikia malengo yake haramu. Tab'ani kikawaida shetani huwa haridhiki na kidogo hicho na ndio maana hufanya kila mbinu kuhakikisha kwamba, anamfikisha mwanadamu huyo aliyeghafilika katika daraja baya kabisa la udhalili. Kwa msingi huo basi, ili kuweza kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, kuna haja ya kuzitambua njia za kupambana na adui shetani.
Kufanya ibada kwa ikhlasi, daima ni jambo ambalo humuweka mbali mtu na mambo mabaya na machafu. Kutekeleza mambo ya wajibu na vile vile ya mustahabu, kujiweka mbali na mambo ya haramu na makruhu yaani yanayochukiza, humfanya mtu awe karibu na Mola Mlezi. Ni kwa kuzingatia ukweli huo ndio maana siku zote shetani hufanya idili ya kumfanya mtu awe mbali na kumuabudu Mwenyezi Mungu.

Kwani kuwa mbali mtu na Mwenyezi Mungu humfanya awe masafa marefu na nuru ya Allah Jalali na kukaribia giza; na hili kimsingi ni takwa la shetani ambae aliomba muhula kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kazi hii yaani kuwapotosha watu na kuwaweka mbali na Mwenyezi Mungu. Aya za 14 hadi 17 katika Surat al-A'raf zinabainisha vyema hilo pale Mwenyezi Mungu anaposema:
Akasema: Nipe muhula mpaka siku watakapo fufuliwa. Akasema: Utakuwa miongoni mwa walio pewa muhula. Akasema: Kwa kuwa umenihukumia upotofu, basi nitawavizia katika Njia yako Iliyo Nyooka. Kisha nitawazukia mbele yao na nyuma yao na kuliani kwao na kushotoni kwao. Wala hutawakuta wengi wao wenye shukrani.
Mtume Muhammad saw amenukuliwa akisema katika hadithi moja ya kwamba, "Je nikujulisheni amali na jambo ambalo kama mtalifanya shetani atajitenga na nyinyi na kuwa mbali, umbali wa Mashariki na Magharibi? Akajibiwa, ndio ewe mjumbe wa Mwenyezi Mungu: Akasema, kufunga Saumu hupelekea sura ya shetani kuwa nyeusi na kutoa sadaka huvunja kiuno chake. Kuwa na mapenzi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na kutoa msaada kwa ajili ya amali njema, hung'oa ndevu zake na kuomba maghufira (kufanya istighfaar) hukata mishipa ya shetani."
Katika hadithi nyingine Bwana Mtume saw anasisitiza umuhimu wa kuswali Swala mwanzoni mwa wakati wake yaani bila kuchelewa na kufanya haraka katika kufanya amali ya kheri na kubainisha nukta hii kwamba, shetani yuko mawindoni na kila lahadha ni mwenye kusubiri watu wateleze katika kutekeleza mambo na amali hizi zenye kupendeza ili aweze kuwazuia wasifanye hayo.
Siku moja Bwana Mtume saw alimuusia Imam Ali as kwa kumwambia:
Ewe Ali! Mara tu unapoingia wakati wa Swala jiandae kwa ajili ya ibada hiyo, kinyume na hivyo, shetani atakushughulisha. Na kila unapotaka kufanya amali ya kheri, harakisha kwani usipofanya hivyo, shetani atakuzuia kufanya amali hiyo.
Kwa upande wake Imam Ali as amesema katika hadithi moja kuhusiana na Swala kwamba:
"Swala ni kilele, ngome na husuni imara, ambayo inawalinda wenye kuswali na mashambulio ya shetani."
Kwa hakika shetani daima hufanya kila awezalo ili kumuweka mbali mwanadamu na sifa njema na zenye kupendwa na badala yake humfanya mja huyo awe na sifa na tabia mbaya kama husuda, hasira, chuki, maneno machafu au mdomo mchafu, tabia mbaya na nyingine na kuzifanya ziwe ni ada na mazoea ya mtu huyo na hivyo kuwa miongoni mwa tabia zake. Hii ni kutokana na kuwa, kila amali mbaya na isiyofaa anayoifanya mwanadamu, humridhisha na kumfurahisha shetani.
Mtume saw amenukuliwa akisema kuwa: Wakati mtu anapofikisha umri wa miaka 40 na mema yake yakawa machache kuliko mabaya (maovu) yake, shetani humbusu katika paji lake la uso na kusema: Sura hii haioni ukweli. Aidha imenukuliwa hadithi kutoka kwa Imam Ja’far Swadiq as ya kwamba amesema: Shetani huliambia jeshi lake, enezeni husuda na uvamizi baina ya watu; kwani mambo haya mawili mbele ya Mwenyezi Mungu ni sawa na shirki.
Kupitia hadithi hii tunaweza kufahamu kwamba, shetani ana jeshi miongoni mwa majini na watu na kupitia wanajeshi hao hufanya kazi ya kueneza mambo machafu na la kufahamu ni kwamba, kila ambaye ataambatana nae huwa na hali ya kishetani na hivyo kuwa miongoni mwa majeshi ya shetani.
Kuhusiana na nukta hiyo tunaashiria hadithi nyingine kutoka kwa Imam Ja’far Swadiq as ambapo amesema: Kila utakapoona mja fulani anachunguza na kutafuta madhambi ya wengine ilihali amesahau madhambi yake, basi tambua ya kwamba, mtu huyo amehadaiwa na shetani.
Tunakamilisha kipindi chetu cha leo kwa kuashiria moja ya sifa mbaya za kimaadili ambayo ni kula riba suala ambalo limekemewa mno katika dini tukufu ya Kiislamu. Imam Ja’far Swadiq anasema kuhusiana na jambo hilo kwamba: Mla riba hataondoka duniani isipokuwa shetani atamfanya kuwa kichaa na mwendawazimu wake.
Wapenzi wasikilizaji kwa leo tunakomea hapa tukitaraji kwamba, mmenufaika na yale niliyokuandalieni kwa leo. Tukutane tena wakati mwingine Inshallah. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh…