Dec 21, 2016 06:25 UTC
  • Hadithi ya Uongofu (61)

Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi na karibuni kujiunga nami tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. Katika sehemu hii ya 61 ya mfululuzo huu juma hili, tunazungumzi tawakkul au kutawakali na kunukuu hadithi zinazohusiana na maudhui hii. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki.

Kutawakali maana yake ni mtu kutaraji na kutegemea kwa mtu mwingine. Kutawakali na kumtegemea Mwenyezi Mungu kuna maana ya mtu anayefanya hima na idili katika mambo yake na kukabidhi hayo kwa Mwenyezi Mungu na kutaka utatuzi wa matatizo yake kutoka kwa Mola Muumba ambaye anafahamu mahitaji na hawaiji zote za wanadamu na ana uwezo wa kuyatatua matatizo yao ya kila aina.  Imenukuliwa kutoka kwa Bwana Mtume saw ya kwamba amesema: Siku moja nilimuuliza Malaika wa Wahyi Jibril kutawakali ni nini? Alinijibu kwa kusema: Hakika ya kutawakali ni mtu kutambua kwamba, yeye ni kiumbe wa Mwenyezi Mungu, hana uwezo wa kudhuru wala kunufaisha pasina ya idhini ya Allah, hana uwezo wa kutoa au kuzuia na ni kuondoa utegemezi kwa mtu na badala yake kumtegemea Mwenyezi Mungu. Hali inapokuwa namna hii, mwanadamu hawezi kufanya kazi isipokuwa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, hawezi kuwa na matarajio na matumaini kwa asiyekuwa Yeye Mola Azali, hamuogopi yeyote isipokuwa Muumba na hawi na matarajio isipokwa kwake Yeye tu. Huu ndio moyo na uhakika wa kutawakali.

Kutawakali maana yake ni kufumbia macho visababishi na nyenzo; hata hivyo haina maana ya kuweka mikono nyuma na kutofanya chochote na kutaraji kufanyiwa kitu na Mwenyezi Mungu. Kwani, kutegemea na kutumia visababishi na nyezo na vile vile sababu za kimaumbile za ulimwengu hiyo yenyewe ni kutawakali kwa Mwenyezi Mungu. Hii ni kutokana na kuwa, kila taathira hutokea kwa mujibu wa matakwa na irada ya Mwenyezi Mungu. Inakuliwa katika vitabu vya hadithi kwamba:

"Siku moja Imam Ali bin Abi Twalib as aliliona kundi Fulani la watu wenye afya na siha njema kabisa, likiwa limeamua kuacha kazi na kukaa katika kona moja ya msikiti. Imam Ali as akawauliza, ninyi ni akina nani? Wakajibu kwa kusema; Sisi ni watu tuliotawakali kwa Mwenyezi Mungu na kuamua kumtegemea yeye tu. Imam Ali as akasema; Hapana, bali nyinyi ni wala bure ambao mnapata riziki kwa juhudi na taabu za wengine."

 

Kutawakali kwa maana yake ya kweli ni mtu kujikomboa kutoka katika mafungamano na utegemezi ambao chimbuko lake ni madhila na utumwa. Kutawakali huku humpatia mtu huyo uhuru na hali ya kujiamini. Hii ni kutokana na kuwa, mtu ambaye atawakali na kutegemea kudura na nguvu azali na zisizo na kikomo za Mwenyezi Mungu hujiona kuwa amepata  ushindi na hali hiyo humfanya aongeze matumaini na hivyo kuendelea kusimama kidete huku akivishinda vitingiti vyote.

Katika Juzuu ya 11 ya Kitabu cha Mustadrak al-Waisail kuna hadithi iliyonukuliwa kutoka kwa Bwana Mtume saw ya kwamba amesema: "Mtu ambaye anataka kuwa mwenye nguvu zaidi miongoni mwa watu, anapaswa kutawakali na kumtegemea  Mwenyezi Mungu."

Aidha hadithi ifuatayo ambayo inapatikana katika Kitabu cha Bihar al-Awar imenukuliwa kutoka kwa Imam Muhammad Baqir as ambaye amesema: Mtu mwenye kutawakali na kumtegemea Mwenyezi Mungu hashindwi, na mtu mwenye kuomba hifadhi kwa Mwenyezi Mungu hawezi kukwama."

Moja ya mifano bora kabisa na kiigizo cha kutawakali kwa Mwenyezi Mungu ni kisa cha Nabii Ibrahim as ambaye akiwa katika mazingira nyeti, waabudu masanamu walikata shauri wamtupe ndani ya moto ili aungue na hivyo waepukane na kile walichokiona kuwa ni shari lake baada ya kumuona kuwa amekuwa kikwazo katika ibada zao za masanamu. Nabii Ibrahim as akiwa katika mazingira haya hakutetereka hata kidogo bali alitawakali kwa Mwenyezi Mungu. Imam Ja'far Swadiq as anasema kuwa: Wakati Nabii Ibrahim as alipowekwa juu ya panda huku waabudu masanamu wakiwa tayari kumtupia katika moto, Malaika Jibril as alimjia na baada ya kumsalimia alimuuliza, je unataka nikusaidie? Nabii Ibrahim as alimjibu kwa kumwambia: Sitaki msaada kutoka kwako. Jibril as akampendekezea Nabii Ibrahim kwamba, sasa kama hutaki msaada kutoka kwangu, basi eleza shida yako kwa Mwenyezi Mungu. Nabii Ibrahim as akasema: Hii kwamba, Mwenyezi Mungu anajua hali ninayokabiliwa nayo, basi kwangu hilo latosha.

Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 68 hadi 70 za Surat al-Anbiya kwamba:

Wakasema: Mchomeni moto, na muinusuru miungu yenu, ikiwa nyinyi ni watendao jambo! Sisi tukasema: Ewe moto! Kuwa baridi na salama kwa Ibrahim! Wao walimkusudia maovu, lakini Sisi tukawafanya wao ndio walio khasiri.

 

Kwa hakika kutawakali ni maalumu kwa waja wampwekeshao Mwenyezi Mungu. Mtu muumini na mwenye kutawakali na kumtegemea Mwenyezi Mungu anafahamu kwamba, chimbuko la uwezo na nguvu zote ni Mwenyezi Mungu pekee. Kwa hakika, mafuhumu na maana ya kutawakali haitengani na imani na Uislamu.

Mmoja wa maswahaba wa Imam Mussa al-Kadhim AS anasimulia kwamba, nilikuwa mjini Makka na nilikuwa nimesimama nyuma ya Imam Mussa al-Kadhim AS. Imam alikuwa akikariri maneno haya haya:Ewe Mwenyezi Mungu! Nakuomba uifanye dhana yangu kuwa ni dhana nzuri, na niwe ni mwenye kutawakali kwako kwa ukweli na ikhlasi.

Luqman al-Hakim anasema alipokuwa akimuusia mwanawe: Ewe mwanangu! Dunia ni bahari yenye kina kirefu ambayo watu wengi wamezama humo, tanguliza mbele imani juu ya Mwenyezi Mungu katika mashua na merikebu yako, lifanye tanga la merikebu yako kuwa ni kutawakali na kumtegemea Mwenyezi Mungu na masurufu yako yawe ni taqwa na uchaji Mungu. Kama utaokoka na kuvuka salama katika bahari hiyo, basi ni kwa baraka za Mwenyezi Mungu na kama utazama na kuangamia basi ni kwa sababu ya dhambi zako."

Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu kwa leo umefikia tamati, msikose kujiunga name wiki ijayo katika sehemu nyingine ya mfululizo huu wa Hadithi ya Uongofu.

Ninakuegeni huku nikikutakieni usikilizaji mzuri wa vipindi vyetu vilivyosalia. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabakaatuh.