Hadithi ya Uongofu (62)
Ni matumaini yangu kuwa, hujambo mpenzi msikilizaji popote pale yanapokufikia matangazo haya ya Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hususan huko nyumbani Afrika Mashariki. Tunakutana tena juma hili katika sehemu nyingine ya mfululizo huu wa kipindi cha Hadithi ya Uongofu. Katika kipindi chetu kilichopita tulikunukulieni baadhi ya hadithi zinazohusiana na kutawakali na kumtegemea Mwenyezi Mungu na kusema kuwa, kutawakali ni aina fulani ya uhusiano wa mja na Muumba wake.
Katika hili, Mutawakkil yaani mtu aliyetawakali huwa na imani na nguvu, hekima, huruma pamoja na mapenzi ya Mwenyezi Mungu na wakati huo huo humzingatia Mola Jalia katika harakati zake zote na kila lahadha hutegemea msaada wa mafanikio kutoka kwa Mola Mlezi. Aidha tulisema kuwa, mtu anayetawakali na kumtegemea Mwenyezi Mungu sambamba na kustafidi na visababishi vya kimaada huihesabu irada na takwa la Mwenyezi Mungu kuwa sharti kuu la kufikia natija ya lile alilolikusudia. Kipindi chetu cha wiki hii kitazungumzia matunda na faida za kutawakali na kumtegemea Mwenyezi Mungu. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki, hii ikiwa ni sehemu ya 62 ya mfululizo huu.
Kutawakali hupelekea kupatikana utulivu wa ndani na uhakika wa moyo kwa mja mwenye kutawakali. Mtu anayetakali na kukabidhi mambo yake kwa Mwenyezi Mungu mbali na kuwa hufanya juhudi na idili kwa ajili ya kupata mafanikio, huamini kwamba, matakwa ya Mwenyezi Mungu ndio yenye kutamalaki na kudhibiti mambo yote. Mtu kama huyo hata kama hatafanikiwa katika katika jambo na kazi yake, huwa hahisi hali ya kukata tamaa au kusikitika; na endapo atafanikiwa basi si mwenye kupatwa na ghururi na kujiona. Sambamba na mtu mwenye kutawakali kutumia sababu na nyenzo za kimaisha kwa ajili ya kufikia lengo lake, huwa anaamini kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu atamruzuku na kumjaalia kupata yale yenye maslahi na yeye kwa kupitia nyenzo hizo au kwa njia nyenginezo ambazo yeye hawezi hata kuzifikiria. Imepokewa katika historia kwamba siku moja kuna mtu alikwenda kwa Bwana Mtume Muhammad SAW na kumwambia:
"Ewe Mtume wa Allah, mimi ninataka kumwacha ngamia wangu na kutawakali kwa Mwenyezi Mungu ili amlinde hadi nitakaporudi". Bwana Mtume akamjibu mtu huyo kwa kumwambia:"Maneno hayo si sahihi. Wewe unapaswa kwanza umfunge ngamia wako, na kisha utawakali kwa Mwenyezi Mungu".
Kutakali na kumtegemea Mwenyezi Mungu mbali na kumpatia mwanadamu utulivu huzuia pia mtu kuhisi kuchoka na kushindwa kufanya kitu. Ndio maana Imam Ali bin Abi Taliba as anasema katika maneno yake machache lakini yaliyojaa maana kwamba, mtu ambaye anatawakali na kumtegemea Mwenyezi Mungu hana taabu wala mchoko. Katika upande mwingine kutawakali na kumtegemea Mwenyezi Mungu humuongezea mtu nguvu ya kufikiri na kumpatia muono mpana na wa wazi ambao ni maalumu.
Hii ni kutokana na kuwa, kutawakali na kumtegemea Mwenyezi Mungu humfanya mwanadamu kutokuwa na woga wala hofu mkabala na matatizo na mazonge. Aidha hali hiyo ya kumtegemea Allah na kukabidhi mambo yake kwa Mola Muumba humpa mja huyu uwezo wa kuchukua maamuzi sahihi na kupata njia ya karibu kabisa ya kuyapatia ufumbuzi matatizo yanayomkabili. Imam Ali as anaizungumzia vizuri nukta hiyo katika hadithi iliyopokewa kutoka kwake ya kwamba amesema: Mtu mwenye kutakali na kumtegemea Mwenyezi Mungu kwake giza la usiku huwa mwanga, huandaliwa sababu na mazingira ya kupata ushindi na hivyo kuyashinda matatizo yanayomkabili.
Katika kubainisha nafasi na utukufu wa kutawakali na kumtegemea Mwenyezi Mungu, Imam Ja’far Sadiq (AS) amesema: "Uwezo na izza siku zote huwa katika mzunguko. Kwa hivyo wakati vinapopata mahala penye kutawakali na kumtegemea Mwenyezi Mungu hustakimu na kukaa hapo".
Kwa maneno mengine ni kwamba, mtu mwenye kutawakali kwa Mwenyezi Mungu huwa na izza na ukwasi wa kutokuwa mhitaji kwa wengine. Katika hadithi tuliyosoma ya Imam Ja’far Sadiq, mtukufu huyo anaashiria faida za binafsi, za kijamii na za kiuchumi za kutawakali, na kutuonyesha kwamba kutawakali na kumtegemea Mwenyezi Mungu kunampa mtu ukwasi na utajiri wa nafsi pamoja na izza, heshima na utukufu kwa watu.
Tab'an ndani ya Qur'ani Tukufu mtu mwenye kutawakali na kumtegemea Mwenyezi Mungu amepewa hadhi na daraja ya juu kiasi kwamba, Yeye mwenyewe Mola Mwenyezi anasema anawapenda watu wenye sifa hiyo tukufu. Ama kuhusu athari nzuri na chanya za kutawakali imeelezwa kuwa, mtu aliyetingwa na kuzidiwa na kushindwa kujua la kufanya, pale anapoishika kamba ya Mola, akatawakali na kumtegemea Yeye, hujihisi amekuwa na nguvu na kupata uhakika kwamba, kwa auni na msaada wa Mwenyezi Mungu ataweza kuyashinda masaibu na matatizo yanayomkabili. Pamoja na hayo kuna ulazima wa kutanabahishana tena hapa kwamba, ili kuweza kufikia malengo na makusudio yake mtu, inabidi azitumie njia zile zile maalumu za kuyafikia malengo hayo, yaani nyenzo na visababishi au sababu za kidunia alizowekewa na Mola.
Imam Ja’far Sadiq (AS) amesema katika hadithi nyengine kuwa: “Mwenyezi Mungu hakubali kuyajaalia mambo yapatikane ila kwa njia na sababu alizoyawekea. Kwa maana hiyo kila kitu amekiwekea sababu yake, na kila sababu ameiwekea njia ya ufunguzi.”
Kutawakali kwa Mwenyezi Mungu wapenzi wasikilizaji humuunganisha mtu na nguvu, uwezo, elimu na hekima isiyo na kikomo ya Mola wa ulimwengu ambazo humwezesha kuneemeka na kufaidika nazo kwa namna nyingi kimaada na kimaanawi. Tuelewe kwamba, Mwenyezi Mungu huwalipa malipo mema na makubwa hapa duniani wale wanaotawakali na kumtegemea Yeye, huondoa hofu na wasiwasi ndani ya nyoyo zao na kuzijaza sakina na utulivu wa aina yake. Miongoni mwa faida nyingine za kutawakali na kumtegemea Mwenyezi Mungu ni kupata uwezo wa kiroho na nguvu za kukakabiliana na matatizo na mambo magumu. Imam Muhammad Baqir as anasema kuwa: Kila mwenye kutawakali na kumtegemea Mwenyezi Mungu hashindwi, na kila mwenye kumtegemea Mola Muumba hakimbii kutoka katika medani ya vita na jihadi. Kwa muktadha huo basi, kila ambaye anataka kuwa mtu mwenye nguvu na imara zaidi miongoni mwa watu anapaswa kutawakali na kumtegemea Mwenyezi Mungu katika mambo yake. Mtume Muhammad saw amenukuliwa akisema kuwa: Mtu ambaye anataka kuwa kipenzi miongoni mwa watu basi na ashikamane na taqwa na uchaji Mungu; na mtu ambaye anataka kuwa mwenye nguvu miongoni mwa watu basi na atawakali kwa Mwenyezi Mungu. Kwa hakika kutawakali na kumtegemea Mwenyezi Mungu huondoa woga na hali ya kumuongopa asiyekuwa Yeye Mola Muumba. Kama mtu ametawakali kwa Mwenyezi Mungu basi hapaswi kumuogoa asiyekuwa Yeye, kwani uwezo na nguvu za Mwwenyezi Mungu ziko juu na ni zenye kushinda nguvu zote na Mwenyezi Mungu akitaka, mwanadamu hupatwa na mushkili na madhara tarajiwa na kinyume na hivyo hakuna mtu anayeweza kumdhuru mwanadamu huyo. Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 107 ya Surat Yunus kwamba:
Na Mwenyezi Mungu akikugusisha madhara, basi hapana wa kukuondolea ila Yeye. Na akikutakia kheri, basi hapana awezaye kurudisha fadhila yake. Huifikisha kwa amtakaye katika waja wake, na Yeye ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu. Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu kwa leo umefikia tamati tukutane tena wiki ijayo. Wassalaamu alaykum warahmatullahi wabarakaatuh