Hadithi ya Uongofu (63)
Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. Katika kipindi chetu cha juma lililopita tulikunukulieni baadhi ya hadithi zinazohusiana na kutawakali na kumtegemea Mwenyezi Mungu na tulisema kwamba, kutawakali ni aina fulani ya uhusiano wa mja mwenye imani na Mwenyezi Mungu Muumba wa ulimwengu na vilivyomo.
Kama anavyosema Mwenyezi Mungu katika aya ya 23 ya Surat al-Maida:
Na mtegemeeni Mwenyezi Mungu ikiwa nyinyi ni Waumini.
Kwa msingi huo, tawakkul na egemeo la Muumini ni Mwenyezi Mungu pekee. Muumini hamuogopi mtu au kitu kingine chochote bighairi ya Mwenyezi Mungu SWT na daima tumaini lake ni Allah pekee. Kipindi chetu cha juma hili ambacho ni sehemu ya 63 ya mfululizo huu kitazungumzia katazo la kumtegemea asiyekuwa Mwenyezi Mungu. Kuweni nami kutegea sikio yale niliyokuandalieni kwa leo. Karibuni.
Sheikh al-Kulayni mmoja wa wanazuoni watajika wa fikihi na mpokezi wa hadithi wa Kishia katika nusu ya kwanza ya karne ya nne Hijria anasema katika kitabu cha Usuul al-Kafi kwamba:
“Hussein bin Al-Wan amesema: Tulikuwa katika kikao cha masuala ya kielimu tukijifunza mambo mbalimbali ya kielimu hali ya kuwa nilikuwa nimepoteza masurufu yangu ya safari. Nikiwa natafakari mtihani ulionipata, mmoja wa marafiki zangu akaniambia: Sasa utafanya nini na tumaini lako ni nani? Nikamjibu kwa kumwambia, tumaini langu ni fulani. Akasema: Kwa msingi huo ninaapa kwa Mola kwamba, hutafanikiwa katika tumaini lako hilo. Nikamuuliza kwa mshangao, kwa nini unasema hivyo? Akasema:
Kwa sababu Imam Ja’far Sadiq as amesema: Nimesoma katika vitabu vya kale kwamba, Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: Ninaapa kwa Izza na utukufu wangu na kwa adhama ya arshi yangu kwamba, kila mtu ambaye atakuwa na matumaini kwa mtu asiyekuwa mimi, basi bila shaka mimi nitakata matumaini yake na kuyabadilisha kuwa hali ya kukata tamaa, na nitamvalisha nguo ya madhila na uduni na nitamuweka mbali na mimi.
Je mja wangu anakuwa na matumaini kwa asiyekuwa mimi pindi anapokabiliwa na matatizo na mambo magumu? Katika hali ambayo ufunguo wa matatizo na magumu yote uko kwangu? vipi mtu huyo anaweka matumaini yake kwa asiyekuwa mimi? Vipi mtu huyo anagonga mlango wa nyumba ya asiyekuwa mimi? Je anafahamu kwamba, ufunguo wa milango yote uko kwangu? Je hatambui kwamba, milango ya nyumba zote imefungwa isipokuwa mlango wa nyumba yangu ndio ambao uko wazi kwa anayerejea kwangu? Ni nani ambaye amenirejea mimi na kuwa na matumaini na mimi katika matatizo na mambo magumu yake kisha mimi nikakata matumaini yake? Ni nani ambaye alikuwa na matumaini ya kutekelezewa shida yake kwangu na mimi nikamkatisha tama?...basi hali mbaya ni watu ambao wamekata tamaa na rehma na msamaha wangu na walioharibikiwa na waliokwama ni wale ambao hawatii amri zangu na hawanizingatii mimi.”
Imam Ja’far Sadiq as amenukuliwa katika hadithi tunayoinukuu katika Kitabu cha Ghurar al-Hikam ya kwamba amesema:
Yaweke matumaini yako yote kwa Mwenyezi Mungu yaani mtegemee Yeye na usiwe na matarajio kwa asiyekuwa Yeye. Kwani hakuna mtu ambaye aliweka matumaini yake kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu isipokuwa alirejea bila ya matumaini.
Ibrahim bin Daud al-Ya’qubi ananukuu kutoka kwa kaka yake kwamba: Siku moja bwana mmoja alimwambia Mtume saw amfundishe jambo ambalo akilifanya Mwenyezi Mungu atampenda mbinguni na watu wa ardhini pia nao watampenda. Mtume saw akamjibu kwa kumwambia: Kuwa na matumaini na kile ambacho kiko kwa Mwenyezi Mungu ili akupende na usitamani kile ambacho kiko kwa watu ili watu nao wakupende.
Malik ni Auf ash’jai anasema kuwa, tulikuwa yapata watu saba au wanane kwa Bwana Mtume saw kisha mbora huyo wa viumbe akasema: Je hamtaki kufanya bai na kula kiapo cha utiifu kwa Bwana Mtume? Tukasema, kwani mpaka sasa hatujakula kiapo cha utiifu kwako? Kisha Mtume saw akasema tena: Je nyinyi hamtaki kula kiapo cha utiifu kwa Mtume wa Allah? Tukanyoosha mikono yetu na kumpa bai Mtume. Mmoja wetu akasema: Tukupe kiapo cha utiifu katika nini na juu ya nini? Mtume wa Allah akasema: Muabuduni Mwenyezi Mungu na msimshirikishe na chochote na mswali Sala tano, zitiini amri za Mwenyezi Mungu na kisha akamalizia kwa kutamka kwa sauti ya chini: Msiombe kitu kutoka kwa watu.
Kwa hakika Mwenyezi Mungu ndiye mkwasi mutlaki na ghairi yake Yeye ni wenye kuhitajia. Ni Mwenyezi Mungu pekee ambaye ni muweza mutlaki na ambaye anaweza kuyatatua matatizo ya waja. Ni kwa muktadha huo kuwa na matumaini au kuweka matumaini kwa asiyekuwa yeye Mola Muumba kunahesabiwa kuwa ni aina fulani ya shirki yaani kumshirikisha Mwenyezi Mungu Jalla Jalaluh.
Imam Ja’far Sadiq as anasema kuwa: Wakati mtu anaposema laiti fulani asingelikuwepo ningeangamia, au ingekuwa sio fulani suala langu lisingetatuliwa au mke na wanangu wangeangamia, mtu anayesema hivi, kwa hakika amemshirikisha Mwenyezi Mungu na asiyekuwa Yeye katika kutoa riziki au katika kuondoa balaa na belua pamoja na ghamu. Mtu aliyekuwa pale wakati Imam Sadiq as anasema maneno hayo akamuuliza Imam: Sasa endapo mtu atatufanyia wema, kazi au jambo muhimu tunapaswa kusemaje? Je tunaweza kusema kwamba, laiti Mwenyezi Mungu asingemjaalia fulani tawfiki na uwezo wa kunihami na kunisadia mimi ningeangamia? Imam akamjibu kwa kumwambia, kusema hivyo ni sahihi kabisa. Kwani nguvu na qudra ya Mwenyezi Mungu imezingatiwa katika matamshi hayo.
Pamoja na hayo kama tulivyoashiria katika vipindi vyetu vilivyotangulia ni kuwa, haitoshi mja kukabidhi mambo yake kwa Mwenyezi Mungu na kumtegemea Muumba pasina ya kufanya bidii na idili katika jambo alilokusudia au kujihusisha na sababu au visababishi kwa kufikia lengo lake.
Wapenzi wasikilizaji kwa leo tunakomea hapa msisite kujiunga name wiki ijayo katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. Basi hadi tutakapokutana tena juma lijalo ninakuageni nikikutakieni kila la kheri.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh…