Alkhamisi, 09 Februari, 2017
Leo ni Alkhamisi tarehe 11 Jamadil Awwal 1438 Hijria, sawa na Februari 9, 2017.
Siku kama ya leo miaka 38 iliyopita majenerali wa utawala wa Shah waliongeza muda wa serikali ya kijeshi katika mji wa Tehran. Majenerali hao walichukua hatua hiyo ili kuwazuia wananchi kuwaunga mkono na kuwasadia wanajeshi wa kikosi cha anga ambao walikuwa wakishambuliwa na kikosi cha gadi ya Shah, na kwa njia hiyo waweze kumtia mbaroni Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu pamoja na shakhsiya wengine muhimu waliokuwa katika harakati za Mapinduzi au kuwauwa. Lakini Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa kuona mbali na kusoma vyema nyakati, aliwatolea mwito wananchi kupuuza kizuizi hicho kilichowekwa na majenerali wa Shah cha kuongeza muda wa serikali ya kijeshi au sheria za kutotoka nje. Wananchi wanamapinduzi wa Iran pia waliitikia agizo hilo la Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu na kumininika katika mitaa mbalimbali na kueneza mapambano yao katika vituo vingine vya kijeshi vya utawala wa kidikteta wa Shah katika mji wa Tehran na miji mingineo.

Siku kama ya leo miaka 25 iliyopita, baada ya Chama cha Wokovu wa Kiislamu cha Algeria (FIS) kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa Bunge, wanajeshi waliokuwa wakitawala nchini humo walibatilisha matokeo ya uchaguzi huo na kukipiga marufuku chama hicho, hali iliyopelekea kuzuka machafuko makubwa. Machafuko hayo yalipelekea kuuawa watu wengi nchini Algeria.
Miaka 54 iliyopita katika siku kama ya leo, serikali ya Abdul-Karim Qassim rais wa wakati huo wa Iraq iliondolewa madarakani katika mapinduzi yaliyofanywa na Kanali Abdul Salam Arif. Akisaidiwa na majeshi ya anga ya Iraq, Abdul Salam Arif alilishambulia jengo la Wizara ya Ulinzi ya Iraq yalipokuwa makao ya Abdul-Karim Qassim Rais wa wakati huo wa nchi hiyo. Baada ya kumtia mbaroni na kumuua Rais huyo, Abdul Salam Arif akajitangaza kuwa Rais wa nchi hiyo. Naye Abdul-Karim Qassim alikuwa ameingia madarakani mwaka 1958, baada ya kufanya mapinduzi ya umwagaji damu dhidi ya mfalme wa mwisho wa Iraq.
Na miaka 841 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa Khaja Nasiruddin Tusi, mwanafalsafa, mwanahisabati, mnajimu na mwanazuoni mkubwa wa Kiirani katika mji wa Tusi kaskazini mashariki mwa Iran. Katika maisha yake aliasisi kituo kikubwa cha kielimu na akademia ya kwanza ya sayansi yaani mahala pa kuangalilia mwenendo wa nyota, mwezi na jua iliyojulikana kwa jina la Maraghe huko kaskazini magharibi mwa Iran. Alimu huyo aligundua namna mpya za kutumia saa ya jua kwa ajili ya kituo hicho. Kituo hicho kilikuwa na suhula muhimu zaidi ambazo kwa miaka 300 baada ya hapo hazikuweza kushushudiwa katika nchi za Magharibi.