Jumatatu, Januari 20, 2017
Leo ni Jumatatu tarehe 22 Mfunguo Nane Jamadil Awwal 1438 Hijria sawa na Februari 20, 2017 Milaadia.
Katika siku kama ya leo miaka 151 iliyopita, vita kati ya Ufaransa na wapigania uhuru wa Mexico vilimalizika kwa ushindi wa Ufaransa na kushika hatamu za uongozi mwanamfalme wa Austria, Maximilian. Katika vita hivyo vilivyoendelea kwa kipindi cha miaka 5, awali Ufaransa iliungana na Uhispania na Uingereza na baada ya muda mfupi nchi hizo mbili zilijitenga na Ufaransa ambayo iliendeleza vita dhidi ya wapigania uhuru wa Kimexico waliokuwa wakiongozwa na rais wa zamani wa nchi hiyo Benito Juárez. Benito Juárez aliendeleza mapambano dhidi ya wakoloni wa Kifaransa hata baada ya kurudi nyuma na kukimbilia katika maeneo ya milimani ya Mexico. Kiongozi huyo hatimaye alifanikiwa kuangusha utawala wa Maximilian akisaidiwa na wapigania uhuru wa nchi hiyo.
Katika siku kama ya leo miaka 70 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 20 Februari 1947, Uingereza hatimaye ilikubali kuipatia India uhuru wake baada ya kuikoloni nchi hiyo kwa zaidi ya karne mbili. Uhuru wa India ulipatikana kutokana na mapambano ya muda mrefu yaliiyoongozwa na Mahatma Gandhi. Katika kipindi chote cha utawala wake wa kikoloni huko India, Uingereza ilipora utajiri na maliasili za nchi hiyo na kuwasababishia hasara kubwa raia wa India. Mwezi Agosti mwaka huohuo India ikajipatia rasmi uhuru wake na ikagawanyika katika nchi mbili za India na Pakistan.
Tarehe Pili Esfand miaka 20 iliyopita magaidi wa makundi ya kiwahabi na kitakfiri walishambulia ubalozi mdogo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mji wa Multan mashariki mwa Pakistan na kuua wafanyakazi 8 wa ofisi hiyo akiwemo Sayyid Muhammad Ali Rahimi aliyekuwa Mwambata wa Utamaduni wa Iran. Miaka sita kabla ya shambulizi hilo la kigaidi magaidi wa kiwahabi walimuua mwambata wa utamaduni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mji wa Lahore nchini Pakistan, Sadiq Ganji.
Shahidi Sayyid Muhammad Ali Rahimi alitishiwa kifo mara kadhaa na magaidi hao wa kiwahabi na hatimaye katika siku kama hii leo alishambuliwa na kuuawa na wanachama wa kundi la kiwahabi la Lashkar-e-Jhangvi akiwa pamoja na wafanyakazi wenzake 7. Mahakama ya Kupambana na Ugandi ya Pakistan iliwahukumu kifo mara saba mawahabi waliohusika na mauaji hayo lakini Mahakama Kuu ya nchi hiyo ilitengua hukumu hiyo na kuwaachia huru. Hata hivyo kingozi wa kundi hilo la kigaidi, Malik Is'haq alipigwa risasi na kuuawa na polisi ya Pakistan wakati alipokuwa akihamishwa kutoka gerezani.
Siku kama ya leo miaka 8 iliyopita, alifariki dunia Ayatuhil Udhma Muhammad Taqi Behjat Foumani, mmoja wa Marajii Taqlidi na maurafaa wakubwa wa Kiislamu. Alizaliwa mwaka 1294 Hijria Shamsia katika mji wa Fouman ulioko katika mkoa wa Gilan kaskazini mwa Iran. Baada ya kupata elimu ya msingi ya kidini, mwaka 1308 Hijria Shamsia alielekea katika Chuo Kikuu cha Kidini cha Najaf nchini Iraq. Ayatullah Bahjat alikuwa mashuhuri sana kutokana na uchaji Mungu wake. Kitabus Swalat, Jamiul Masail na Wasilatun Najat ni baadhi ya vitabu mashuhuri vya msomi huyo.