Feb 25, 2017 02:36 UTC
  • Jumamosi, Februari 25, 2017

Leo ni Jumamosi tarehe 27 Mfunguo Nane Jamad al-Awwal 1438 Hijria sawa na tarehe 25 Februari 2017 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 260 iliyopita, aliaga dunia Abdul Karim bin Ahmad Halabi mpokezi wa hadithi wa Kiislamu. Alikuwa mashuhuri mno katika upokezi wa hadithi katika zama zake katika mji wa Halab unaopatikana hii leo huko nchini Syria. Halabi alisoma elimu za Fiqh, Usuul al-Fiqh, tafsiri, hadithi na elimu nyingine zilizokuwako katika zama zake kwa baba yake na maulama wengine. Baadaye Halabi alikuwa kipofu ingawa hata hivyo hakupoteza moyo wa matumaini aliokuwa nao na aliendelea kujihusisha na elimu ya hadithi. Msomi huyo ana vitabu mbalimbali na kimojawapo ni kile kinachoitwa Ad'ayat Safar. ***

Abdul Karim bin Ahmad Halabi

Katika siku kama ya leo miaka 61 iliyopita, alifariki dunia mtaalamu wa fasihi na malenga mkubwa wa Iran, Allamah Ali-Akbar Dehkhoda. Alizaliwa mjini Tehran mwaka 1258 Hijiria Shamsia na akawa miongoni mwa wanafunzi wa awali wa chuo cha zamani cha siasa mjini Tehran. Baada ya kukamilisha masomo yake ya awali, Dehkhoda alikwenda Ulaya na kufanya utafiti kwa miaka 5. Alirudi Iran katika kipindi cha kuchipua fikra za kupigania uhuru, kipindi ambacho alikitumia kufanya kazi za kishairi dhidi ya utawala wa wakati huo. Kazi kubwa zaidi ya msomi huyo ni kamusi maarufu ya Dehkhoda. ***

Allamah Ali-Akbar Dehkhoda

Miaka 31 iliyopita, dikteta wa zamani wa Ufilipino aliyekuwa amejitangaza rais wa maisha, Ferdinand Marcos, alikimbia nchi hiyo akiwa pamoja na familia yake. Marcos alichukua hatamu za uongozi mwaka 1965. Alidumisha utawala wake wa kidikteta na ukandamizaji nchini Ufilipino kwa himaya na uungaji mkono wa nchi za Magharibi hususan Marekani. Mwaka 1973 Ferdinand Marcos alijitangaza kuwa rais wa maisha wa Ufilipino. Wakati huo wananchi katika maeneo mbalimbali walikuwa tayari wameanzisha harakati za mapambano ya kisiasa na kijeshi dhidi ya dikteta huyo. Mapambano hayo yalishika kasi zaidi katikati ya muongo wa 1980, na Februari 25 1986 Marcos alilazimika kuikimbia Ufilipino.***

Ferdinand Marcos

Na katika siku kama ya leo miaka 23 iliyopita, Mzayuni mmoja aliyekuwa na misimamo ya kufurutu ada aliwashambulia na kuwamiminia risasi Waislamu waliokuwa wakitekeleza ibada ya Swala katika Msikiti wa Haram ya Nabii Ibrahim as mjini al Khalil, Palestina inayokaliwa kwa mabavu na kuua shahidi 29 miongoni mwao. Mauaji hayo yalitokea wakati Waislamu hao walipokuwa katika ibada ya funga ya mwezi mtukufu wa Ramadhani. Waislamu wengine wengi walijeruhiwa katika shambulizi hilo la kikatili. Mauaji hayo ambayo yalidhihirisha tena uhasama na chuki za Wazayuni wa Israel dhidi ya Waislamu, yalilaaniwa na Waislamu kote duniani. Ukatili huo ulizusha wimbi kubwa la machafuko katika ardhi za Palestina ambapo wananchi walizidisha mapambano dhidi ya maghasibu wa Tel Aviv. Israel ilimshika kwa muda na kumuachia huru mhalifu huyo katili kwa kisingizio kwamba alikuwa punguani. ***

 

Tags