Apr 04, 2017 08:20 UTC
  • Hadithi ya Uongofu (68)

Ni wasaa na wakati mwingine wapenzi wasikilizaji wa kujiunga nami katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu.

Kama tulivyosema katika vipindi vyetu vilivvyotangulia ni kuwa, kipindi hiki hujadili na kuzungumzia masuala mbalimbali ya kijamii, kidini, kimaadili na kadhalika na kukunukulieni baadhi ya hadithi zinazohusianan na maudhui husika. Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 68 ya mfululizo huu, kitazungumzia suala la kuona mbali na kuwa na uono na mtazamo wa mbali. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki kutegea sikio niliyokuandalieni kwa leo.

Hadithi ya Uongofu

 

Kuwa na mtazamo na muono wa mbali inahesabiwa kuwa ni moja ya sifa za Mwislamu. Imam Ali bin Abi Twalib as anasema kuwa, kuwa na muono wa mbali ni kuzingatia hatima na mustakabali wa jambo na kazi. Imamu huyo wa Mashariki na Magharibi anasema: "Kuwa na muono wa mbali ni kuzingatia na kutilia maanani mwisho na hatima ya kazi na kushauriana na wenye busara na hekima."

Katika mafundisho ya Kiislamu kuwa na muono na mtazamo wa mbali ni jambo lenye nafasi aali na ya juu mno. Qur’ani Tukufu inawausia wafuasi wake kwamba, wawe na mtazamo wa mbali na wasipumbazwe na mambo na maslahi ya kupita ya duniani; bali waizingatia Akhera na maisha ya baada ya hapa duniani. Qur’ani inawataka waumini wafanye mambo yao kwa namna ambayo kesho yaani Siku ya Kiyama wawe ni wenye saada na mafanikio. Katika Surat Shams baada ya Mwenyezi Mungu kuelezea kadhia ya kaumu ya Thamud na hatima ililiyowapata anasema katika aya ya 15 na ya mwisho ya Sura hiyo kwamba, "Wala Yeye haogopi matokeo yake"

Hii ina maana kwamba, matatizo yote yaliyoipata kaumu hiyo chimbuko lake lilikuwa ni kwamba, wahusika hawakuwa na muono na mtazamo wa mbali na hawakuwa ni wenye kufikiria hatima na majaaliwa ya yale waliokuwa wakiyatenda.

Mwenyezi Mungu anabainisha tukio hilo katika Sura tuliyotangulia kuitaja ya Shams. Anasema:

"Kina Thamudi walikadhibisha kwa sababu ya upotofu wao. Alipo simama mwovu wao mkubwa. Hapo Mtume wa Mwenyezi Mungu alipo waambia: Huyu ni ngamia wa Mwenyezi Mungu, mwacheni anywe maji fungu lake. Lakini walimkadhibisha na wakamchinja ngamia, kwa hivyo Mola wao Mlezi aliwaangamiza kwa sababu ya dhambi zao na akawafuta kabisa."

Kwa mtazamo wa Imam Ali bin Abi Twalib as ni kuwa, mtu mwenye muono na mtazamo wa mbali ni yule ambaye hafikirii tu natija na matokeo ya amali na matendo yake hapa duniani, bali hutazama mbali zaidi yaani huzingatia natija na matokeo ya amali anayoifanya kwamba, itakuwa vipi huko Akhera. Fauka ya hayo, mtu huyo hutanguliza zaidi suala la Akhera kuliko la hapa duniani. Kwa maana kwamba, huyapa kipaumbele matokeo na maslahi ya Akhera zaidi kuliko ya duniani. Aidha Imam Ali as anasema kwamba: Kuwa na muono wa mbali ni kutii amri za Mwenyezi Mungu na kupingana na nafsi.

 

Moja ya mifano ya wazi ya kuwa na muono mpana na mtazamo wa mbali ni kwamba, wakati mwanadamu anapotaka kusema kitu au kufanya jambo fulani, kwanza hufikiria natija, matokeo, malengo na hatima ya neno lile au amali ile. Kama natija na matokeo yatakuwa ni mazuri basi husema neno lile na kufanya amali ile aliyokusudia kuifanya. Lakini kama baada ya kufikiri ataona kuwa, natija na matokeo ya neno na amali anayokusudia kuifanya ni mbaya, basi huacha kusema au kutenda jambo lile; kwa muktadha huo kuelekea katika njia ya saada na ufanisi.

Bwana mmoja alimuendea Bwana Mtume saw na kumwambia, Ewe mjumbe wa Allah niusie. Mtume saw akamwambia je nikikuusia utalifanyia kazi lile nitakalokwambia? Bwana yule akajibu, ndio ewe mjumbe wa Allah. Mtukufu Mtume saw akasema: Mimi ninakuusia kwamba, kila utapochukua uamuzi wa kufanya jambo Fulani, kwanza fikiria natja na matokeo ya kazi hiyo na fikiria, kama utaona matokeo yake ni sahihi na mazuri basi ifanye. Na kama utaona matokeo yake ni mabaya na yenye kupotosha na yanaambatana na kuporomoka, basi badilisha uamuzi wako na usiifanye kazi hiyo.

Moja ya siri kubwa za mafanikio ya kila mwanadamu ni hatima ya muono wa mbali. Mwanadamu anapaswa kufikiri juu ya natija ya jambo analotaka kulifanya na awe na mtazamo na muono wa mbali. Mtu ambaye ana muono wa mbali na akatambua mfumo wa utawala wa dunia na wakati huo huo akawa ni mwenye kuzingatia matokeo ya matukio na natija ya amali na matendo, akawa si mwenye kufanya jambo isipokuwa baada ya kufikiria natija na matokeo ya jambo lenyewe na vile vile akawa ni mwenye kuwa na tadbiri na tafakuri, bila shaka hawezi kujuta. Kwa maneno mengine ni kuwa, hatua zake hizo ni kinga za majuto. Ukweli ni kuwa, kama mwanadamu anataka awe mtu wa kheri na mambo mema, basi anapaswa kuwa na muono na mtazamo wa mbali zaidi. Ni kwa kuzingatia ukweli huo, ndio maana Imam Ali bin Abi Twalib as akasema kuwa: Kuwa na muono wa mbali ni kuzingatia na kutilia maanani mwisho na hatima ya kazi na kushauriana na wenye busara na hekima.

Sisitizo juu ya kutaka ushauri linatokana na ukweli huu kwamba, akili ya kila mwanadamu kadiri itakavyokuwa katika daraja ya ukamilifu, lakini uono na uwezo wa mtu hupanuka zaidi kupitia kupata ushauri kutoka kwa wengine na kwa msingi huo kupunguza kiwango cha kukosea. Hii yenyewe bila shaka ni aina fulani ya tadbiri na maarifa.

Muhammad, Mtume wa Mwenyezi Mungu

 

Kwa hakika kuwa na muono wa mbali ni jambo ambalo lina athari na baraka nyingine. Miongoni mwa athari na baraka hizo ambayo tunaweza kuiashiria hapa ni suala la kuwa na azma imara na thabiti katika kufanya mambo.

Mtu ambaye anapima na kuchunguza engo zote za kazi au jambo analotaka kulifanya na akawa na mtazamo wa mbali kisha akatathmini matokeo ya mbali na ya karibu bila shaka ataanza kuifanya kazi hiyo akiwa na irada na azma imara huku lengo lake likiwa ni kuhakikisha kwamba, anaifanikisha kazi hiyo. Hata hivyo kadiri kiwango cha mtazamo wa mbali cha mhusika kitakavyopungua basi vivyo hivyo azma ya mtu nayo huwa dhaifu. Hii ni kutokana na kuwa, mwenye mtazamo huo huwa hana uhakika na hatima pamoja na matokeo ya kazi anayoifanya.

Imam Ali bin Abi Twalib as analiashiria jambo hilo kwa kusema: Mtu ambaye mtazamo wake wa mbali ni dhaifu na mdogo basi azma na uamuzi wake pia utadhoofika.

Katika maisha tunayoishi, mwanadamu daima hukumbana na mambo ambayo humlazimu achukue uamuzi. Kuwa na hisia za huba na furaha ya hali ya juu kwa upande mmoja na akili na mantiki katika upande wa pili, ni mambo ambayo humtia katika mashinikizo ya namna ya kuchukua uamuzi. Katika mazingira kama haya kulitazama jambo kwa mapana na marefu na kuwa na mtazamo wa mbali ni jambo ambalo linaweza kumsaidia katika kuchukua uamuzi sahihi na wa kimantiki.

Inasimuliwa kwamba, siku moja bedui mmoja alimuomba Mtume saw amnasihi. Mtume saw akamwambia usikasirike. Mwarabu yule wa jangwani akatosheka na nasaha na waadhi huo na kuondoka zake. Aliporejea katika kabila lake alikuta pametokea ugomvi baina ya kabila lake na kabila jingine na pande mbili zilikuwa tayari zimejiandaa kwa ajili ya kuingia vitani. Bwana yule naye kutokana na taasubi na mapenzi makubwa aliyokuwa nayo kwa kabila lake alishikwa na hamasa na kupandwa na morali na akiwa na lengo la kutetea kabila lake alichukua silaha na kujiandaa kuingia vitani. Mara akiwa katika hali hiyo akakumbuka nasaha na maneno ya Bwana Mtume saw kwamba, asikasirike na asiruhusu hasira zimemtawale. Alituliza hasira zake na akaanza kutafakari. Akiwa katika hali hiyo alizinduka na mantiki yake ikaanza kufanya kazi. Akafikiri na kujiuliza kwa nini pande mbili ziingie vitani na kuanza kuuana? Alikwenda na kuwakaribia maadui na akwaambia yuko tayari kutoa mali yake na kuwapatia kile walichokuwa wakitaka kama dia na gharama. Maadui wale nao baada ya kusikia maneno ya kimantiki kutoka kwa Bwana yule wakawa wako tayari kuacha vita. Kwa muktadha huo ugomvi ukamalizika kwa kheri na salama na moto wa hisia za ugomvi uliokuwa ukitokota katika mioyo yao ukazimika kwa hatima ya kufikiria na kutafakari.

Na hadi wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia tamati ya kipindi chetu kwa leo. Tukutane tena wiki ijayo.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.