Hadithi ya Uongofu (72)
Ni wasaa na wakati mwingine wa kujiunga nami wapenzi wasikilizaji katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. Kipindi chetu kilichopita kilianza kujadili moja ya tabia mbaya za kimaadili nalo ni suala la kuchunguza na kupekua aibu na mapungufu ya watu wengine. Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 72 ya mfululizo huu kitaendelea kujadili maudhui hii na kukunukulieni baadhi ya hadithi zinazohusiana na jambo hili. Karibuni.
Tunaanza kipindi chetu cha leo kwa maneno ya Imam Muhammad Baqir as ambaye amenukuliwa akisema: Aibu kubwa zaidi kwa mtu ni kuchunguza aibu za wengine ilihali yeye mwenyewe ana aibu kama hizo na hana habari juu ya hilo.
Ni jambo lisilo na shaka kwamba, wakati mtu anapojishughulisha kwa ajili ya kuondoa aibu na mapungufu aliyonayo, hawezi kupata wasaa na fursa ya kuchunguza na kufuatilia aibu na mambo ya watu wengine na kwa muktadha huo atafanikiwa kujirekebisha na kuondoa aibu na mapungufu aliyonayo. Katika mazingira kama haya mtu hawezi kuwa hamu na raghba ya kutafuta na kufuatilia aibu za wengine na wala hatakuwa na muda wa kufikiria aibu za wengine.
Kwa hakika, moja ya mambo ambayo yameusiwa katika Qur'ani na katika hadithi ni suala la mtu kujihusha na yale yanayomhusu badala ya kujihusisha na mambo ya watu wengine. Qur'ani Tukufu inawataka waumini wajishughulishe na nafsi zao na kuzichunga. Aya ya 105 ya Surat al-Maida inaashiria hilo kwa kusema: Enyi mlio amini! Kilicho lazima juu yenu ni nafsi zenu.
Kwa hakika mtu anapaswa kuizingatia nafsi yake na aibu zake, ajikosoe na kujirekebisha na akifanya hivyo bila shaka hatawakuwa na muda wa kujihusisha na aibu za watu wengine. Mtu wa namna hii hata kama ataona mabaya ya wengine kwa kuwa yeye mwenyewe ana aibu kama hiyo hujizuia kufichua na kutaja aibu za wenzake. Imam Muhammad Baqir as amenukuu hadithi kutoka kwa Bwana Mtume saw na kusema: Sifa kadhaa nzuri endapo mtu atakuwa nazo zote au hata kama atakuwa na sifa moja kati ya hizo, basi Siku ya Kiyama ambapo kutakuwa hakuna kivuli, yeye atakuwa katika kivuli cha Arshi ya Mwenyezi Mungu. Moja ya sifa hizo ni mtu kutochunguza aibu za ndugu yake Muumini.
Mtume Muhammad SAW ambaye ni mwanadamu mkamilifu kabisa na mbora wa viumbe alijipamba na suala la kufunika na kutofichua aibu za wengine na alikuwa akiwausia wafuasi wake kwa kuwaambia: Kila ambaye ataficha na kufunika aibu ya ndugu yake Mwislamu na kutomuumbua, basi Mwenyezi Mungu Siku ya Kiyama atazisitiri aibu zake.
Nukta muhimu ya kuzingatia hapa ni hii kwamba, makusudio ya kufunika na kutotaja aibu za mtu ni kutofichua mapungufu aliyonayo mtu huyo. Pamoja na hayo jukumu la kuamrishana mema na kukatazana mabaya linalazimu mtu kumueleza ndugu yake Mwislamu aibu na mapungufu aliyonayo, lakini hilo kama tulivyoashiria katika kipindi chetu cha juma lililopita ni jambo ambalo linapaswa kufanyika kwa siri na njia bora na yenye maneno mazuri na ya kuvutia kiasi cha kutomfanya mlengwa achukie.
Tunasoma katika sehemu ya barua ya Imam Ali bin Abi Twalib AS kwa Malik al-Ashtar kwamba:
"Baina ya watu kuna aibu na mapungufu yaliyojificha, hivyo usiondoe pazia lake. Mwenyezi Mungu mwenyewe anahukumu kuhusiana na mambo ya siri. Ficha na usitiri aibu na mapungufu kadiri unavyoweza ili Mwenyezi Mungu naye asitiri na kuficha aibu zako ambazo unapenda zibakie kuwa ni siri.”
Imam Ali AS amenukuliwa akisema kuwa: Hongera zimuendee mtu ambaye anazingatia aibu zake na anajizuia kufuatilia na kuchunguza aibu za wengine. Tukirejea mafunduisho na ya Uislamu na hadithi tunapata kuwa imesisitizwa na kutiliwa mkazo juu ya suala la mtu kuangalia aibu na mapungufu yake kabla ya kuangalia aibu za wengine. Imam Ali AS anasema: Mtu anayetazama aibu za watu anapaswa kuanza na aibu zake.
Inanukuliwa kutoka kwa Bwana Mtume saw ya kwamba amesema: Katika mji mmoja walikuwa wakiishi watu, lakini watu wa mji huo walikuwa na sifa moja nzuri sana, nayo ni kufumbia macho aibu za wengine. Ni kwa kuzingatia hilo ndio maana Mwenyezi Mungu Mtukufu alizifunika aibu zao. Watu hao waliaga dunia hali ya kuwa, watu wengine hawakuwa na habari juu ya aibu na mapungufu yao. Hivyo wakafa huku wakiwa wameacha jina zuri. Katika upande mwingine kuna watu ambao hawakuwa wamefanya dhambi yoyote ile, lakini hawakuwa na soni wala haya kutaja aibu na mapungufu ya watu wengine. Ndio maana kutokana na tabia yao hiyo mbaya Mwenyezi Mungu aliliondoa pazia la aibu zao kiasi kwamba, waliondokea kuwa mashuhuri kwa aibu zao hizo na kisha wakaaga dunia wakiwa na umashuhuri huo mbaya na usiopendeza.
Imekuja katika hadithi kwamba, itakafika Siku ya Kiyama, siku hiyo Bwana Mtume SAW atamuomba Mwenyezi Mungu kwamba, wakati wa kuhesabu amali za watu, umati wake usihesabiwa amali zao mbele ya Malaika, Mitume na umma nyingine. Mtume SAW anamuomba Mwenyezi Mungu umma wake uhesabiwe amali na matendo yake kwa namna ambayo ghairi ya Mtume na Mwenyezi Mungu, watu wengine wasifahamu aibu na madhambi ya umma wake. Baada ya Mtume SAW kutoa ombi lake hilo Mwenyezi Mungu atamjibu kwa kusema:
Ewe kipenzi changu, mimi ni mwenye huruma zaidi na waja wangu, kwani kama ambavyo wewe hupendi aibu zao zifahamike na watu wengine, mimi pia sipendi na sioni vizuri aibu zao zifahamike hata kwako wewe. Ni kwa sababu hiyo mimi nitalishughulikia mwenyewe suala la kuhesabu amali zao kiasi kwamba, ili ghairi yangu asipatikane mtu ambaye atafahamu aibu na makosa yao.”
Katika dua nyingi suala la kusitiriwa aibu limezingatiwa mno.
Tunahitimisha kipindi chetu cha leo kwa sehemu ya dua ya Imam Ali bin Hussein Zainul Abidiin AS katika kitabu chenye thamani kubwa cha Sahifat al-Sajjadiyah inayosema kwamba:
Ewe Mola wangu ninayekuabudu! Sifa njema na shukurani ni zako, aibu ngapi umenisitiri hukunifedhehesha, dhambi ngapi umezifunika kwa ajili yangu hukunifanya niwe mashuhuri kwazo. Makosa mangapi nimeyatenda wala hukunichania pazia la sitara, wala haukunibandika utepe wa chuki ya fedheha yake, wala haukudhihirisha aibu yake kwa atafutaye aibu zangu miongoni mwa majirani zangu na wenye husuda ya neema zako kwangu.”
Na hadi hapa ndio tunafikia tamati ya kipindi chetu cha Hadithi ya Uongofu kwa juma hili, basi hadi tutakapokutana tena tunamuomba Allah atujaalie kuwa miongoni mwa wanaojishughulisha na mambo yao na kutofuatilia na kupekua aibu na mapungufu ya wengine.
Wassalaamu Alayakum Warahmatullahi Wabarakaatuh