Hadithi ya Uopngofu (75)
Ni matumaini yangu kuwa, mubukh wasaa na wakati mwingine wa kujiunga nami wapenzi wasikilizaji katika mfululizo wa kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. Kipindi chetu cha juma hili ambacho ni sehemu ya 75 ya mfululizo huu kitazungumzia suala la mtu kupenda jaha na kutaka uongozi. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki. Karibuni.
Kama mnavyojua kimaumbile mwanadamu ni mwenye kujipenda. Hii ni kutokana na kuwa, Mwenyezi Mungu amelijaaliwa suala hilo katika dhati ya kiumbe huyu. Kuwa na muelekeo wa mwanadamu kujipenda ambapo katika istilahi ya kidini na kiakhlaqi, jambo hilo linajulikana kama Hubbu Dhaat yaani kujipenda, katika hatua ya awali mwanadamu hushajiika huelekea upande wa kukidhi mahitaji yake ya kimatamanio na kimaisha kama vile kula, kunywa, kulala na kadhalika.
Amma katika hatua ya juu zaidi huwa katika chimbuko na msingi wa harakati jumla na muelekeo wa mwanadamu huyu katika njia ya ukamilifu na kumtafuta Mwenyezi Mungu. Lakini kama hamu na shauku hii itakengeuka mkondo na njia sahihi, mwanadamu huyu akiwa njiani ataelekea upande wa kutaka cheo, madaraka, utajiri na uongozi.
Masuala ambayo Mtume saw ameyakemea katika madhumuni ya hadithi inayosema: Hatari na uharibifu wa wanyama wawili wanaoshambulia kundi la kondoo sio kubwa ikilinganishwa na hatari na ufisadi, uharibifu wa hamu na kupenda uongozi, mali, na umashuhuri katika dini ya Mwislamu.
Kupenda jaha maana yake ni kuwa na mapenzi ya kupindukia ya uongozi na cheo kiasi kwamba, katika mazingira kama haya, mtu wa aina hii awe yuko tayari kufikia lengo hilo kwa thamani yoyote ile. Kupenda jaha na uongozi ni miongoni mwa mambo hatari mno ambayo sio tu hutoa pigo kwa mtu katika upande wa kimaanawi, bali kwa mtazamo wa kijamii humfanya mtu huyo achukiwe na kutengwa.
Hali hii ya kupenda mno jaha na uongozi hupelekea kupatikana nifaki katika moyo wa mwanadamu. Mtume Muhammad saw amenukuliwa akisema kuwa, kupenda jaha na uongozi ni mithili ya maji ambayo hupelekea kukua majani, basi ndivyo ambavyo pia nifaki hukua na kustawi katika moyo wa mwanadamu.
Maneno haya ya Bwana Mtume saw yana nafasi muhimu na yanaainisha nafasi muhimu ya kupenda jaha na uongozi katika nifaki na misimamo ya kindumakuwili ya mwanadamu. Hii ni kutokana na kuwa, wakati mwingine mwanadamu huyo akiwa na lengo la kupata jaha, uongozi na nafasi katika jamii au kulinda hali ya kupendwa kwake, hufanya hima na idili ya kutopingana na wana jamii na hivyo kuwa pamoja nao katika itikadi na matakwa yao hata kama atafahamu kwamba, watu hao wapo katika makosa na kinyume na maslahi ya jamii.
Hii hali ya kupenda jaha, uongozi na umashuhuri na cheo katika jamii, humpelekea mtu huyo kuikanyaga haki na kuipuuza moja kwa moja, ili tu aweze kufikia katika malengo yake aliyokusudia yaani ya cheo au kulinda nafasi na uongozi wake alionao.
Kupenda jaha na kuwa na muelekeo wa kutaka cheo na uongozi huandaa uwanja wa mtu kuangamia.
Dini tukufu ya Kiislamu imekemea mno suala la mtu kupenda jaha na uongozi. Moyo ambao unapiga na kudunda kutokana na kupenda kukuza jina hauwezi kuwazingatia watu bali huwa mtumwa wa hilo unalolihangaikia.
Watu wanaopenda jaha na uongozi daima hufanya hima ya kuhifadhi na kulinda uongozi wao usiwatoke na daima hufanya juhudi kadiri wawezavyo ili kuhakikisha kwamba, vyeo walivyonavyo wanaendelea kuwa navyo kwa thamani yoyote ile. Mtu wa namna hii huugua na kupata maradhi mara anapopoteza cheo au uongozi alionao. Watu wa aina hii husononeka na kupata maradhi ya nafsi mara wanapopokonywa vyeo na madaraka walionayo.
Watu wa aina hii hushughulishwa na pirika za kuhifadhi vyeo walivyo navyo kiasi cha kughafilika na Mwenyezi Mungu na Siku ya Kiyama. Natija ya kuwa na hali hiyo ni kulaaniwa na kuchukiwa na Mwenyezi Mungu. Kama anavyosema Imam Ja’afar Swadiq as: Amelaaniwa yule ambaye anashughulishwa daima na kutaka jaha na uongozi.
Hii ni kutokana na kuwa, kupenda jaha na uongoizi hupelekea mwanadamu kuasi na kuzidi jeuri na kiburi mbele ya Muumba wake na hivyo kukiuka amri za Allah. Ndio maana Bwana Mtume saw amenukuliwa akisema kuwa: Dhambi za mwanzo zilizofanywa mkabala na amri za Mwenyezi Mungu duniani sababu yake yalikuwa ni mambo sita na mojawapo ni kuwa na mapenzi makubwa na uongozi na cheo.
Kile ambacho kiko wazi ni kwamba, uongozi, madaraka na jaha havipatikani kwa urahisi. Wakati mwingi ili kupata vyeo hivyo mtu anapaswa kufanya hima na bidii kubwa sambamba na kupitia magumu na kuvumilia machungu mengi.
Tab’an yapasa ifahamike kwamba, kuna watu ambao hukubali kuchukua cheo au uongozi lengo lao likiwa ni kutoa huduma kwa viumbe na kupata ridhaa za Mwenyezi Mungu kwa kutatua matatizo ya watu katika jamii. Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 74 na 75 za Surat Furqan kwamba:
Na wale wanao sema: Mola wetu Mlezi! Tupe katika wake zetu na wenetu yaburudishayo macho, na utujaalie tuwe waongozi kwa wachamngu. Hao ndio watakao lipwa makao ya juu kwa kuwa walisubiri, na watakuta humo maamkio na salamu
Kwa msingi huo basi, daima kupenda jaha na mtu kufanya kila awezalo ili tu afanikiwe kupata jaha na uongozi ni jambo baya na lisilopendeza. Allama Majlisi mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu anasema kuwa, jaha na uongozi vimegawanyika katika sehemu mbili.
Mosi, katika haki na pili katika batili. Hata hivyo yote hayo mawili yanarejea kwa ustahiki wa mtu pamoja na nia yake ya kutaka jaha na uongozi. Kwa hakika watu ambao hutaka cheo na madaraka kwa ajili ya malengo ya Mwenyezi Mungu, hawa si wenye kupenda madaraka wala uongozi bali lengo lao kubwa ni kuhudumia jamii na kutaka kupata radhi za Mwenyezi Mungu.
Watu wa aina hiyo ni kama Imam Ali bin Abi Twalib as ambaye alikuwa akifanya harakati katika njia ya kuhakikisha hukumu za Mwenyezi Mungu zinatawala na haki ndio inayothibiti katika jamii.
Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu unakomea hapa kwa leo tukutane tena wiki ijayo katika sehemu nyingine ya mfululizo huu.
Wassalaamu alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.