Apr 26, 2017 07:06 UTC
  • Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain (158)

Assalaama Aleiukm wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mnaotusikiliza kutoka mjini Tehran.

Katika kipindi hiki cha 158 katika mfululizo wa vipindi vya itikadi ya Kiislamu tutaendelea kujibu swali la msikilizaji wetu Bwana Said Ahmad wa Tanga Tanzania ambalo tulianza kulijibu katika kipindi kilichopita ambalo linasema: Je, ni tofauti gani iliyopo kati ya elimu ya Maimamu  wa Ahlul Beit  (as) na watu wengine ambao wamebeba au kunakili elimu kutoka kwa Mtume Mtukufu (saw).

Tulipata kufahamu katika kipindi hicho kwamba watukufu hawa (as) wana elimu kamili na ya kitabu chote kitakatifu cha Quráni, tofauti na watu wengine waliopata au kunukuu elimu hiyo kutoka kwa Mtume (saw). Wakati huohuo elimu yao ni ya kurithi kutoka kwa Mtume jambo linalowafanya kuwa ni warithi wa mji wa elimu yote ya Mtume (saw) na wala elimu yao haiwezi kupatikana kuwa na makosa, mghafala au sahau kama inavyofanyika katika elimu ya watu wengine wa kawaida na hilo linatokana na mfangamano madhubuti na usiokatika uliopo kati ya watukufu hao wa Nyumba ya Mtume na kitabu kitakatifu cha Quráni.

 

Wapenzi wasikilizaji, tunajifunza kutokana na maandiko matakatifu pia kwamba elimu ya Ahlul Beit (as) hujibu na kwenda sambamba kabisa na mahitaji ya maisha ya wanadamu kwa sababu katika kila mlango hufunguka milango mingine mingi ya elimu ya yakini ambayo hujibu na kukidhi mahitaji yao wanayoyahitajia katika elimu na maarifa tofauti katika kila zama na sehemu wanayoishi. Tofauti hizi muhimu zinaashiriwa na hadithi mashuhuri iliyopokelewa na masahaba kadhaa kama vile Abdullah bin Masoud kama ilivyonukuliwa katika kitabu cha al-Irshad cha Sheikh Mufid, Abdallah bin Omar na wengineo na ambayo pia imepokelewa kwa njia ya Ahlu Suna kama inavyoonekana katika vitabu vya Hilyat al-Auliyaa, Kanzul Ummal na vitabu vinginevyo. Na sisi hapa kwanza tunainukuu hadithi hiyo kutoka katika kitabu cha al-Kafi ambacho kimenukuu hadithi ya Imam Ja’far as-Swadiq (as) kwamba alisema: ‘’Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) alisema katika maradhi yaliyompelekea kuaga dunia: Niitieni rafiki yangu. (Aisha na Hafsa) wakaagiza baba zao waitwe, lakini Mtume (saw) alipowatizama aliinamisha (kugeuza) uso wake na kisha kusema: Niitieni rafiki yangu. Ali akaitwa na alipomtazama alimwendea na kuanza kumzungumzisha. Alipoondoka Ali, walimkujia na kumuuliza, alikwambia nini rafiki yako? Akasema (as): Alinisimulia milango elfu moja ambapo nilifunguliwa milango mingine alfu moja katika kila mlango.’’

Na Sheikh Mufid amenukuu katika kitabu chake cha al-Irshad hadithi iliyopokelewa na Abdallah bin Masoud inayosema: ‘’Mtume alimwita Ali na kuketi naye kwenye faragha. Alipotukujia tulimuuliza, je, alikuahidi nini? Akasema: Alinifundisha milango elfu moja na kila mlango kati ya hiyo kunifungukia milango mingine alfu moja.’’

 

Ndugu wasikilizaji, na hadithi hii ndiyo ile aliyoitolea hoja Imam Ali (as) mbele ya Talha ambaye alisimama dhidi yake kwenye vita vya Jamal. Nam, imepokelewa katika kitabu cha Suleim bin Qeis hadithi ndefu inayosema kwamba Imam Ali (as) alisema: “Katika kipindi cha kuugua kwake, Mtume alinipa siri ya ufunguo wa milango elfu moja ya elimu ambapo katika kila mlango ilifunguliwa milango mingine elfu moja, na lau kama Umma, tokea alipofariki dunia Mtume (saw), ungelinifuata na kunitii ungelikula (ungelinufaika na) neema za Mwenyezi Mungu tokea vichwani na chini ya miguu yao hadi Siku ya Kiama.’’

Mwishoni mwa hadithi hii kuna ishara muhimu sana ambayo inasisitiza kwamba kutengewa Maimamu wa kizazi cha Mtume Muhammad (as) aina hii ya elimu ni dhamana tosha kwamba Uislamu unatosheleza na kukidhi mahitaji yote ya mwanadamu katika kila zama na kutatua matatizo yote yanayoikabili jamii ya mwanadamu katika kila zama na sehemu na hivyo kuifanikisha na kuiwezesha ifikie maisha bora na mema humu duniani na huko Akhera. Na hapa ndipo kuna moja ya siri za kusisitiza maandiko matakatifu na hasa hadithi ya Thaqalain kwamba wongofu na kuepuka upotovu kunapatikana katika kushikamana kwa pamoja na Quráni pamoja na kizazi kitoharifu cha Mtume (saw). Hii ni kwa sababu ni kizazi hicho tu ndicho kilicho na maarifa na elimu timilifu ya Quráni Tukufu nzima ambayo huwafungulia wanadamu milango ya kila jambo wanalolihitaji kwa ajili ya kupata ufanisi, saada na mwongozo mwema kutoka kwa Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala.

 

Wasikilizaji wapenzi, utambuzi mzuri wa hakika hii unatuelekeza kwenye sifa nyingine maalumu ambayo imetengewa Maimamu wa Ahlul Beit peke yao (as), sifa ambayo wanazuoni na wapokezi wengine wa Suna za Mtume (saw) hawakufanikiwa kuwa nayo. Sifa hii ni kwamba wao ndio wanaomiliki elimu maalumu ya Mwenyezi Mungu, elimu ambayo huwa hampi mtu yoyote isipokuwa yule anayempenda Yeye. Suala hili limezungumziwa pia na wanazuoni wa Kisuni akiwemo Ibn Hajar katika kitabu chake cha as-Swawaiq ambaye tulimzungumzia katika kipindi kilichopita. Mwanazuoni mwingine mashuhuri wa Kisuni aliyezungumzia suala hili ni mwandishi wa kitabu cha Ihyau Uluum ad-Deen, Imam Muhammad al-Ghazali ambaye amesema katika kitabu chake cha al-Ilm al-Ladunni: ‘’Ali (ra) alisema: Mtume wa Mwenyezi Mungu (sa(wa alihi)s) aliingiza ulimi wake kwenye mdomo wangu na kupuliza kwenye moyo wangu milango elfu moja ya elimu ambapo katika kila mlango ilifunguka milango mingine elfu moja. Kisha akasema (ra): Kama ningepewa madaraka (fursa) ningehukumu baina ya watu wa Torati kwa Torati yao na watu wa Injili kwa Injili yao.’’

Kisha al-Ghazali alifafanua suala hilo kwa kusema: ‘’Na daraja hii haifikiwi kwa elimu ya kusoma bali mtu huweza kuifikia kwa kwa nguvu ya elimu ya Ladunni.’’

Sifa hii ya Maimamu watoharifu wa Nyumba ya Mtume Muhammad (saw) kuwezeshwa kumiliki elimu ya Laduni ambayo Mwenyezi Mungu huipuliza kwenye nyoyo zao huwafungulia milango mingi ya maarifa ya Mwenyezi Mungu ambayo wasomi na wanazuoni wengine au wapokezi wa sunna za Mtume (saw) hawafanikiwi kuifikia. Jambo hilo huwawezesha kufikia na kunufaika daima na elimu safi, isiyo na makosa na ya kiwango cha juu  kutoka kwa Mwenyezi Mungu Muumba, na hili ndilo jambo ambalo tutalizungumzia kwa kina kidogo katika kipindi chetu kijacho cha Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain, panapo majaaliwa yake Mola.

Basi hadi wakati huo kutoka hapa Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran hatuna la ziada isipokuwa kukuageni nyote tukikutakieni usikilizaji mzuri wa vipindi vyetu vilivyosalia, kwaherini.