May 24, 2017 18:27 UTC
  • Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain (165)

Assalaam Aleikum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Swali la kipindi hiki cha 165 katika mfululizo huu wa vipindi vya Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain linasema: Je, ni dalili zipi zinazothibitisha Maada na maisha ya Akhera na wanaopinga suala hili wanategemea hoja zipi?

Swali hili hujitokeza baada ya sisi kufahamu umuhimu wa imani juu ya Ufufuo na Siku ya Mwisho na athari kubwa ya imani hiyo katika maisha ya mwanadamu na mienendo yake maishani. Tumechunguza katika vipindi vitatu vilivyopita maandiko matakatifu ambayo yanatuongoza kufikia matunda na manufaa makubwa ya imani hii inayohusiana na Maad. Msingi wa itikadi hii ni kujua dalili na hoja zake. Kuzijua hoja hizo ndiko kunakoimarisha imani ya Ufufuo na maisha ya Akhera kwenye nyoyo za wanadamu na kuwafanya watekeleza yale yanayopaswa kutekelezwa kwa mujibu wa imani hiyo. Hivyo basi hebu na tuanze kujibu swali la kipindi hiki kwa kutegemea misingi na nguzo mbili muhimu za wongofu ambazo ni Quráni Tukufu na Ahlu Beit wa Mtume Mtukufu (saw).

***********

Ndugu wasikilizaji, kuna ishara ya kuvutia katika aya za Quráni Tukufu ambayo inaashiria hakika hii ya kiitikadi kwamba ni vigumu kuthibitisha kiakili, kinafsi (kisaikolojia) na kimatendo kutokuwepo Maada na maisha ya Akhera. Kwa msingi huo uthibitisho wa Maad hauhitajii kuvunjwa kwa dalili zinazotolewa na wakanushaji wa hakika hiyo wala kuzijadili kwa sababu kimsingi wakanushaji hao hawana dalili wala hoja yoyote ya kuthibitisha madai yao isipokuwa kutegemea matamanio tu jambo ambalo halina itibari yoyote. Suala hili linaashiriwa na Quráni Tukufu katika aya za 24 hadi 27 za Surat al-Jaathiya ambapo Mwenyezi Mungu anawazungumzia wapinzani na wakanushaji wa hakika hiyo iliyo wazi kwa kusema:

وَقَالُوا مَا هِيَ إِلَّا حَيَاتُنَا الدُّنْيَا نَمُوتُ وَنَحْيَا وَمَا يُهْلِكُنَا إِلَّا الدَّهْرُ وَمَا لَهُمْ بِذَلِكَ مِنْ عِلْمٍ إِنْ هُمْ إِلَّا يَظُنُّونَ.

وَإِذَا تُتْلَى عَلَيْهِمْ آيَاتُنَا بَيِّنَاتٍ مَا كَانَ حُجَّتَهُمْ إِلَّا أَنْ قَالُوا ائْتُوا بِآبَائِنَا إِنْ كُنْتُمْ صَادِقِينَ.

قُلِ اللَّهُ يُحْيِيكُمْ ثُمَّ يُمِيتُكُمْ ثُمَّ يَجْمَعُكُمْ إِلَى يَوْمِ الْقِيَامَةِ لَا رَيْبَ فِيهِ وَلَكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ.

وَلِلَّهِ مُلْكُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَيَوْمَ تَقُومُ السَّاعَةُ يَوْمَئِذٍ يَخْسَرُ الْمُبْطِلُونَ.

Na walisema: Hapana ila huu uhai wetu wa duniani - tunakufa na tunaishi, na hapana kinachotuhilikisha isipokuwa dahari. Lakini wao hawana ilimu ya hayo, ila wao wanadhani tu. Na wakisomewa Aya zetu zilizo wazi hawana hoja ila kusema: Waleteni baba zetu, ikiwa nyinyi ni wakweli. Sema: Mwenyezi Mungu anakuhuisheni, kisha anakufisheni, kisha anakukusanyeni Siku ya Kiyama isiyo na shaka. Lakini watu wengi hawajui. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye ufalme wa mbingu na ardhi. Na siku itaposimama Saa ya Kiyama, siku hiyo wataangamia wenye kushikamana na upotovu.

Aya hizi wapenzi wasikilizaji zinaashiria zaidi ya hakika moja kuhusiana na Maad ya kwanza ikiwa ni ile ambayo tumeiashiria hivi punde kwamba wanaokanusha imani ya Maad hufanya hivyo bila ya kuwa na dalili yoyote ya kielimu na kwamba hupinga ukweli huo kwa kudhani tu ambako hakuna msingi wala hoja yoyote ya maana mbele ya haki na ukweli.

 

Kutokana na kutokuwa na hoja yoyote ya kimantiki wale wanaokana kuwepo kwa Ufufuo, tunaona kwamba huwa wanatoa matakwa ya kupotosha ma kuonyesha kuchanganyikiwa kwao na hiyo ndiyo hakika ya pili inayozungumziwa na aya hizi tukufu. Wanaposomewa aya zinazofafanua na kubainisha wazi mambo kwa msingi wa hoja zinazothibitisha Maad na maisha ya Akhera huwa wanakwepa mjadala wa kimantiki kuhusu suala hilo na kuanza kutoa madai yasiyo na msingi ya kutaka kurejeshwa duniani baba zao walioaga dunia miaka na karne nyingi zilizopita. Huku ni kuchanganya mambo kuliko wazi kwa sababu kuthibitisha Maad ni kuthibitisha Ufufuo na maisha ya Akhera na sio uhai kwenye dunia hii. Siku hiyo ni siku ya kuhesabiwa wanadamu huko Akhera kutokana na matendo yao waliyoyatenda humu duniani, ambapo waliotenda mema wataishi milele Peponi na waliotenda maovu wataungua motoni milele, tunamwomba Mwenyezi Mungu atuepushie mbali hilo. Katika kujibu shubha na upotovu huo wa wakanushaji, Quráni Tukufu inathibitisha kupitia aya kadhaa uwezo mkubwa wa Mwenyezi Mungu katika kuhuisha wafu kama tunavyoshuhudia katika kisa cha Nabii Ibrahim al-Khalil (as), kisa cha Nabii Uzeir (as) na visa vingine vingi. Shubha na kuchanganyikiwa huko bila shaka kunatokana na ukaidi dhidi ya haki na kuafuata matamanio ambako kuko mbali na akili timamu na hakika ya mambo. Ukweli huu unaashiriwa na Maulana al-Imam Jawad as-Swadiq (as) katika hadithi inayozungumzia aina tofauti za ukaidi, ambayo imepokelewa katika kitabu cha al-Kafi ambapo Imam ananukuliwa akisema: ‘Ama ukaidi wa kukufuru ni ule wa kukana Umola wa Mweyezi Mungu ambapo mkaidi husema: Hakuna Mola wala Pepo, wala Moto nayo ni kauli ya makundi mawili katika makafiri wanaoitwa ad-Dahriyya. Wanasema: ‘Na hapana kinachotuhilikisha isipokuwa dahari.’ Nayo ni dini ambayo walijibunia kwa matamanio yao wenyewe bila ya kuwathibitikia hilo wala kutafiti wanachokisema.’

*********

Wapenzi wasikilizaji, ama hakika ya tatu ni ile inayoashiriwa na Mweyezi Mungu Mtukufu katika aya ya mwisho tuliyoisoma hivi punde inayosema: Na siku itaposimama Saa ya Kiyama, siku hiyo wataangamia wenye kushikamana na upotovu.

Kwenye aya hii kuna ishara inayobainisha kwamba kukanusha Ufufuo na maisha ya Akhera kuna maana ya mwanadamu kujiweka katika hatari ambayo kwa uchache itampata mtu anayekana Ufufuo kinyume na yule anayeuthibitisha, na hili ni jambo ambalo linapingwa na akili iliyo salama.

Na huu ndio ukweli ambao Maimamu wetu watoharifu wa Nyumba ya Mtume (as) waliuthibitisha katika mihadhara na mijadala yao mingi na makafiri. Tutakunukulieni hapa baadhi ya mifano hiyo ambayo imenukuliwa katika kitabu cha Mizaan al-Hikma kama thibitisho la hakika hii. Katika moja ya mijadala ya Imam Swadiq (as) na mmoja wa wakanushaji wa Maad, Imam (as) alisema: ‘Kama hali itakuwa unavyosema wewe – yaani kwamba hakuna Maad – je, mimi nitakuwa na chochote cha kuhofia kutokana na yale ninayokutahadharisha wewe kuhusiana na adhabu ya Mwenyezi Mungu? Yule mkanushaji akasema: Hapana, kutokana na ukweli kwamba kimsingi yeye anapinga kuwepo Maad na kwa hivyo hakuna hofu kwa yoyote kupatwa na adhabu ya Mwenyezi Mungu…. Hapo Imam (as) akasema: Je, kama hali itakuwa ninavyosema mimi – yaani kuthibiti Maad – na haki kuwa mikononi mwangu, si nitakuwa nimesibu kutokana na kufuata kile nilichokuwa nikikutahadharisha kuhusiana na adhabu ya Muumba na wewe kuangamia kutokana na ukaidi na upingaji wako?

Mkanushaji huyo akasema: Ndio. Imam (as) akasema: ‘Basi ni nani kati yetu anapasa kuwa na imani ya kuwa karibu nusura (kunusurika)? Hapo yule mkanushaji akakiri makosa yake kwa kusema: ‘Ni wewe.’

Na Imam Musa al-Kadhim (as) alimwambia mmoja wa wakanushaji wa Maad: ‘Kama suala hilo ni kama unavyosema wewe - na bila shaka sio unavyosema wewe – basi tutakuwa  tumenusurika na wewe pia utakuwa umenusurika lakini kama ukweli wa mambo utakuwa tunavyosema sisi – na bila shaka ni kama tunavyosema – tutakuwa tumenusurika na wewe kuangamia.’

 

Na muhtasari wa mambo tuliyojifunza katika kipindi hiki wapenzi wasikilizaji ni kuwa ni muhali kuthibitisa kutokuwepo Ufufuo na maisha ya Akhera katika hali ambayo kupinga jambo hilo kwa uchache  ni kuiweka nafsi ya mwanadamu mbele ya hatari inayoweza kutokea, jambo ambalo bila shaka akili salama haikubaliani nalo. Na huu ni utangulizizi wa kujadili maandiko matakatifu ambayo yanathibitisha Maad. Hili ndilo suala tutakalolijadili katika kipindi chetu kijacho cha Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain Inshallah.

Tunakushukuruni nyote kwa kuwa pamoja nasi hadi mwisho wa kipindi hiki ambacho kimekujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutoka mjini Tehran. Basi hadi Juma lijalo panapo majaaliwa, tunakuageni nyote kwa kusema Wassalaam Aleikum Warahmatullahi Wabarakatuh.