May 24, 2017 18:30 UTC
  • Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain (166)

Assalaam Aleikum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mnayoisikiliza kutoka mjini Tehran. Kipindi ni kipindi cha Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain ambacho hujibu maswali mbalimbali yanayohusiana na itikadi ya Kiislamu.

Kama mnavyokumbuka katika vipindi kadhaa vilivyopita tumekuwa tukizungumzia suala la Ufufuo au kwa neno jingine Maad ambayo ni katika misingi ya imani ya Kiislamu. Katika kipindi kilichopita tulipata kujua kwamba wanaopinga Ufufuo hawana dalili yoyote ya kutetea msimamo wao huo wa kupinga Ufufuo na maisha ya Akhera baada ya mauti ya humu duniani. Huo ndio uliokuwa utangulizi wa kujibu sehemu ya kwanza ya swali tulilouliza katika kipindi kilichopita ambalo lilisema je, ni dalili zipi zilizopo za kuthibitisha Ufufuo na maisha ya Akhera? Tunarejea kwa pamoja maandiko matukufu ya mwongozo wa Mwenyezi Mungu ili tupate jibu sahihi la swali hili, hivyo kuweni pamoja nasi hadi mwisho wa kipindi, karibuni.

*********

Kwanza wasikilizaji wapenzi, tunaona kwamba Quráni Tukufu inasifu Maad kuwa ni moja ya mambo yasiyokuwa na shaka ndani yake na kwa mfano kusema katika aya ya 26 ya Surat al-Jaathiyya:

قُلِ اللَّهُ يُحْيِيكُمْ ثُمَّ يُمِيتُكُمْ ثُمَّ يَجْمَعُكُمْ إِلَى يَوْمِ الْقِيَامَةِ لَا رَيْبَ فِيهِ وَلَكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُو.

Sema: Mwenyezi Mungu anakupeni uhai, kisha anakufisheni, kisha anakukusanyeni Siku ya Kiyama isiyo na shaka. Lakini watu wengi hawajui.

Na huenda kukanusha kuwepo shaka katika kuthibiti Maad na Siku ya Kiama kunarejea katika nguvu na uwazi wa dalili za kutimia suala hili kwa upande mmoja na kutegemea suala hili maombile ya mwanadamu kwa upande wa pili. Dalili hii inayotajwa kuwa ni ya kimaumbile imezungumziwa katika maandiko mengi matukufu. Tunasema katika kubainisha suala hili kwamba kimaumbile mwanadamu hutaka kuishi milele na nafsi iliyo salama huwa haipendi kuangamia. Hili ni suala la kimaumbile ambalo linaonekana katika kila mwanadamu. La muhimu hapa ni kwamba hitilafu hutokea katika uainishaji wa njia sahihi ya wongofu ambayo humdhaminia mwanadamu maisha ya milele yanayoambatana na saada. Hili ni jambo linalothibitishwa na maandiko matukufu. Kwa mfano aya tukufu ya 129 katika Surat as-Shuaraa inasema:

وَتَتَّخِذُونَ مَصَانِعَ لَعَلَّكُمْ تَخْلُدُونَ.

Na mnajenga majengo ya fakhari kama kwamba mtaishi milele!

Aya hii inaashiria kwamba hata matajiri wapenda-anasa pia hujenga majumba ya kifahari humu duniani wakitaraji kwamba wataishi humo milele. Allama Tabatabai anasema katika kufasiri aya hii kwamba wanadamu hao wanaopenda anasa hujenga majumba hayo makubwa na marefu kutokana na matarajio yao ya kuishi humo milele, la sivyo hawangejenga majengo na majumba kama hayo ambayo hudumu miaka mingi kuliko maisha ya kawaida anayoishi mwanadamu humu duniani.

 

Wpenzi wasikilizaji, hakika hii pia inasisitizwa na hadithi tukufu ambazo zinasema kwamba mwanadamu aliumbwa kwa ajili ya kuishi milele na sio kwa ajili ya kuangamia na kwamba mauti yana maana ya kumalizika maisha ya mwanadamu duniani na sio kuagamia kwake. Katika kitabu cha al-I’tikadaat cha Sheikh Swaduq, Mtume (saw) amenukuliwa akisema katika moja ya hadithi zake kwamba: ‘Hamukuumbwa kwa ajili ya kuangamia (kufa) bali muliumbwa kwa ajili ya kubaki, bali mnahamishwa kutoka nyumba moja hadi nyingine.’

Naye Imam wetu Swadiq (as) amenukuliwa katika kitabu cha Ilal as-Sharai’ akisema: ‘Tumeumbwa kwa ajili ya kubaki bali tunatoka kwenye nyumba moja kwenda nyumba nyingine.’

Na imepokelewa katika kitabu cha al-Irshad cha Sheikh Mufid hutuba ya Amir al-Mu’mineen Ali (as) akisema: ‘Enyi watu! Hakika sisi na nyinyi tumeumbwa kwa ajili ya kubaki (kudumu) milele na wala sio kwa ajili ya kuangamia. Lakini mutahamishwa kutoka nyumba (makao) moja hadi nyingine. Hivyo basi jikusanyieni masurufu kwa ajili ya kule mnakoelekea na kudumu huko milele.’

Hadithi hizi tukufu na nyinginezo mfano wa hizo zinabainisha wazi kwamba mwanadamu aliumbwa kwa ajili ya kubaki na kudumu milele na sio kwa ajili ya kuangamia. Hili ni jambo ambalo limekita mizizi kwenye maumbile ya mwanadamu tokea alipoumbwa na huenda maumbile hayo ya kimsingi ndiyo humfanya akachukia mauti kwa sababu hufahamu vyema kuwa matarajio yake ya kuishi milele hukandamizwa na mauti. Kwa msingi huo hadithi tulizosoma zilikuja ili kumfariji na kumpa matumaini kwamba kifo sio mwisho wa kuishi mwanadamu bali ni kuhama kutoka makao mamoja hadi mengine. Hii ndio maana hadithi hizo zinamsihi mwadamu kufanya juhudi zake zote kwa ajili ya kujiandalia maisha mema huko Akhera na kujiepusha kuabudu dunia na kutumia nguvu zake zote kwa ajili ya maisha ya humu duniani kwa sababu maisha haya sio ya kudumu milele.

 

Ndugu wasikilizaji, kutokana na kudiriki kimaumbile kwamba kupenda kubakia hai na kuishi milele ni jambo linalotokana na maumbile asilia ya mwanadamu tokea kuumbwa kwake, tunalazimika kukubali ukweli huu kwamba bila shaka kuna maisha mengine ambayo yanamdhaminia mwanadamu maisha ya milele yasiyokuwa na kikomo. Jambo jingine lisilokuwa na shaka ni kwamba dunia sio sehemu ya kudhaminiwa maisha hayo kwa sababu sote tunafahamu kwamba mwanadamu huwa anakufa humu duniani. Hivyo ni lazima tutafute sehemu nyingine ambako maisha ya mwanadamu hudhaminiwa kuendelea kubaki milele bila ya kukabiliwa na mauti. Kwa msingi huo dalili ya kuthibitisha udharura wa kuwepo Ufufuo na makao ya Akhera ni kama udharura wa kuwepo maji baada ya kuthibitishwa kuwepo uhai kwenye mwanadamu. Mwenyezi Mungu ni mtukufu na mwenye hekima kubwa kiasi kwamba hawezi kumuumba mwanadamu anayehitajia maji na chakula kutokana na maumbile yake asilia, bila ya kumuandalia mahitaji hayo muhimu maishani kwa ajili ya kukidhi kiu na njaa inayomkabili. Hivyo ndivyo ilivyo kuhusiana na matamanio na maumbile yake ya kupenda kuishi milele. Madamu mwanadamu atakuwa na mahitaji hayo kwenye maumbile na nafsi yake bila shaka lazima kuwepo na jambo la kukidhi mahitaji hayo na hilo linawezekana tu kupitia Maad na Ufufuo utakaomwezesha kudumu na kuishi milele katika maisha ya Akhera.

*********

Na kufikia hapa mpenzi msikilizaji ndio tunafikia mwisho wa kipindi hiki cha Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain ambacho kimekujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka hapa mjini Tehran. Tunakushukuru nyote kwa kututegea sikio hadi mwisho wa kipindi. Basi hadi tutakapokutana tena juma lijalo panapo majaaliwa hatuna la ziada ila kukuageni tukikutakieni kila la heri maishani, kwaherini.

 

Tags