May 24, 2017 18:22 UTC
  • Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain (163)

Assalaam Aleikum wasikilizaji wapenzi wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka hapa mjini Tehran. Ni matumaini yetu kwamba nyote hamjambo na mko tayari kutegea sikio kipindi cha juma hili cha Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain ambacho kinakujieni moja kwa moja kutoka mjini Tehran, ambapo swali la juma hili ni je, ni baraka zipi muhimu zaidi ambazo tunazipata kutokana na nguvu ya imani juu ya Ufufuo na Siku ya Mwisho?

Nyote wasikilizaji wapenzi mnafahamu vyema kwamba mwanadamu kimaumbile hupenda kheri na hivyo kila anapofahamu kwamba jambo fulani lina baraka na kheri ndani yake hufanya juhudi kubwa za kuweza kulifikia ili apate kunufaika nalo. Na hapa ndipo tunapodiriki umuhimu wa jibu la swali hili na hasa baada ya kujua katika kipindi kilichopita kwamba maandiko matakatifu yameipa umuhimu mkubwa imani juu ya Ufufuo au kwa ibara nyingine Maad, jambo ambalo bila shaka linaashiria umuhimu wake katika maisha ya mwanadamu.

********

Tunapoirejea Quráni Tukufu tunapata kwamba ina aya nyingi mno ambazo zinatuelekeza kwenye matuda na baraka za kuwa na imani juu ya Siku ya Mwisho. Tutagusia hapa baadhi ya aya hizo ambapo tunaanza ni zile zinazosema kuwa imani juu ya Maad ni moja ya njia muhimu zaidi za mbinguni zinazomuwezesha mwanadamu kufikia daraja ya ‘birr’ au utendaji mema, kwa maana ya watu wema kufikia daraja za juu zaidi za mambo ya kheri. Tunasoma katika aya ya 177 ya Surat al-Baqarah ambapo Mwenyezi Mungu Mtukufu (saw) anasema:

لَيْسَ الْبِرَّ أَنْ تُوَلُّوا وُجُوهَكُمْ قِبَلَ الْمَشْرِقِ وَالْمَغْرِبِ وَلَكِنَّ الْبِرَّ مَنْ آمَنَ بِاللَّهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ وَالْمَلَائِكَةِ وَالْكِتَابِ وَالنَّبِيِّينَ وَآتَى الْمَالَ عَلَى حُبِّهِ ذَوِي الْقُرْبَى وَالْيَتَامَى وَالْمَسَاكِينَ وَابْنَ السَّبِيلِ وَالسَّائِلِينَ وَفِي الرِّقَابِ وَأَقَامَ الصَّلَاةَ وَآتَى الزَّكَاةَ وَالْمُوفُونَ بِعَهْدِهِمْ إِذَا عَاهَدُوا وَالصَّابِرِينَ فِي الْبَأْسَاءِ وَالضَّرَّاءِ وَحِينَ الْبَأْسِ أُولَئِكَ الَّذِينَ صَدَقُوا وَأُولَئِكَ هُمُ الْمُتَّقُونَ.

Sio wema kuelekeza nyuso zenu upande wa mashariki na magharibi, bali wema ni wa anayemwamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho na Malaika na Kitabu na Manabii, na akawapa mali, kwa kupenda kwake, jamaa na mayatima na masikini na wasafiri, na waombao, na katika ukombozi wa watumwa, na akawa anasimamisha Swala, na akatoa Zaka, na wanaotimiza ahadi zao wanapoahidi, na wanaovumilia katika shida na dhara na wakati wa vita; hao ndio waliosadikisha na ndio wenye takwa.

Tunaashiria hapa nukta nzuri na ya kuvutia sana katika mojawapo ya matunda ya kuwa na imani ya Siku ya Mwisho, nukta ambayo ametajwa mwishoni mwa aya hii nayo ni ya kufuzu na kufikia daraja mbili muhimu za watu waliosadikisha na mutaqeen yaani walio na takwa. Hii ina maana kwamba kuimarika na kukita mizizi imani hii ya Maad kwenye nyoyo za watu ni mojawapo ya njia za kujitakasa kutokana na ria na magonjwa mengine ya kiroho. Kwa mfano inatufikisha kwenye natija hii aya tukufu ya 264 ya Sura hiyohiyo ya al-Baqarah ambayo inasema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تُبْطِلُوا صَدَقَاتِكُمْ بِالْمَنِّ وَالْأَذَى كَالَّذِي يُنْفِقُ مَالَهُ رِئَاءَ النَّاسِ وَلَا يُؤْمِنُ بِاللَّهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ فَمَثَلُهُ كَمَثَلِ صَفْوَانٍ عَلَيْهِ تُرَابٌ فَأَصَابَهُ وَابِلٌ فَتَرَكَهُ صَلْدًا لَا يَقْدِرُونَ عَلَى شَيْءٍ مِمَّا كَسَبُوا وَاللَّهُ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الْكَافِرِينَ.

Enyi mlioamini! Msiharibu sadaka zenu kwa masimbulizi na udhia, kama yule anayetoa mali yake kwa kuwaonyesha watu, wala hamwamini Mwenyezi Mungu wala Siku ya Mwisho. Basi mfano wake ni kama mfano wa jabali ambalo juu yake pana udongo, kisha likapigwa na mvua kubwa, ikaliacha tupu. Basi hawatakuwa na uwezo wowote katika walivyochuma. Na Mwenyezi Mungu hawaongozi watu makafiri.

Kama mnavyoona wapenzi wasikilizaji, kuna baraka nyingine katika imani ya Maad nayo ni wongofu na kuepuka mwanadamu kuhasirika humu duniani na huko Akhera. Na hili ndilo suala linaloashiriwa na aya hii katika kufananisha hali ya mtu asiyemwamini Mwenyezi Mungu wala Siku ya Mwisho na ile ya udongo ulio juu ya jabali ambao haunufaiki kwa vyovyote vile na mvua ambayo huwaletea wanadamu baraka tele maishani. Hii ni kwa sababu roho ya mtu wa aina hiyo hubadilika na kuwa ngumu na ya kikatili ambapo mwishowe huhasirika na kupoteza manufaa yote ya humu duniani na Akhera. Hatima ya mtu kama huyo Siku ya Mwisho itakuwa sawa na ya kafiri ambaye alijinyima mwenyewe fursa ya kunufaika na mwongozo wa Mwenyezi Mungu.

 

Ndugu wasikilizaji, aya za Quráni Tukufu zinasema wazi kuwa moja ya athari za kuwa na imani juu ya Ufufuo ni kuathirika mja na mawaidha ya Mwenyezi Mungu na hivyo kumfanya atende mambo mema na kujiepusha na maasi. Kwa mfano Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 232 ya Surat al-Baqarah:

ذَلِكَ يُوعَظُ بِهِ مَنْ كَانَ مِنْكُمْ يُؤْمِنُ بِاللَّهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ذَلِكُمْ أَزْكَى لَكُمْ وَأَطْهَرُ وَاللَّهُ يَعْلَمُ وَأَنْتُمْ لَا تَعْلَمُونَ.

Hayo anaonywa nayo yule miongoni mwenu anayemwamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Hayo ni mazuri mno kwenu na safi kabisa. Na Mwenyezi Mungu anajua, na nyinyi hamjui.

Kama ambavyo miongoni mwa baraka za nguvu ya kuwa na imani juu ya Akhera na yakini ya kutimia Ufufuo na Siku ya Kuhesabiwa ni kuachana na kila aina ya ufisadi duniani. Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 36 ya Surat al-Ankabut:

وَإِلَى مَدْيَنَ أَخَاهُمْ شُعَيْبًا فَقَالَ يَا قَوْمِ اعْبُدُوا اللَّهَ وَارْجُوا الْيَوْمَ الْآخِرَ وَلَا تَعْثَوْا فِي الْأَرْضِ مُفْسِدِينَ.

Na kwa Wamadyana tulimtuma ndugu yao Shuaibu, naye akasema: Enyi watu wangu! Mwabuduni Mwenyezi Mungu na iogopeni Siku ya Akhera, wala msiende katika ardhi mkifanya ufisidi.

Bali imani juu ya Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho ni njia ya kujibari na kujitenga na wafisadi na maadui wa Mwenyezi Mungu na Mtume wake (saw) pamoja na waumini, kama inavyoashiria hilo mathalan kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu katika aya ya mwisho ya Surat al-Mujaadalah inayosema:

لَا تَجِدُ قَوْمًا يُؤْمِنُونَ بِاللَّهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ يُوَادُّونَ مَنْ حَادَّ اللَّهَ وَرَسُولَهُ وَلَوْ كَانُوا آبَاءَهُمْ أَوْ أَبْنَاءَهُمْ أَوْ إِخْوَانَهُمْ أَوْ عَشِيرَتَهُمْ أُولَئِكَ كَتَبَ فِي قُلُوبِهِمُ الْإِيمَانَ وَأَيَّدَهُمْ بِرُوحٍ مِنْهُ وَيُدْخِلُهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِنْ تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُمْ وَرَضُوا عَنْهُ أُولَئِكَ حِزْبُ اللَّهِ أَلَا إِنَّ حِزْبَ اللَّهِ هُمُ الْمُفْلِحُونَ.

Huwakuti watu wanaomwamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho kuwa wanawapenda wanaompinga Mwenyezi Mungu na Mtume wake, hata wakiwa ni baba zao, au watoto wao, au ndugu zao, au jamaa zao. Hao ameandika katika nyoyo zao Imani, na amewapa nguvu kwa Roho itokayo Kwake. Na atawaingiza katika Mabustani ambayo hupita mito chini yake. Humo watadumu milele. Mwenyezi Mungu awe radhi nao, na wao wawe radhi naye. Hao ndio Hizbullahi, Kundi la Mwenyezi Mungu. Hakika Kundi la Mwenyezi Mungu ndilo lenye kufaulu.

Kwa kuzingatia zaidi aya hii ndugu wasikilizaji, tunapata kujua baraka nyingine zinazotokana na imani juu ya suala zima la Maad kama vile kufaulu kupata uungaji mkono na ridhaa ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, kuimarika imani na kunufaika na saada katika maisha ya baadaye huko Akhera.

 

Tunaendelea kuzungumzia wapenzi wasikilizaji, baadhi ya aya za Quráni Tukufu ambazo zinatuongoza katika kujibu swali la kipindi hiki kuhusiana na matunda tunayoyapata kutokana na imani ya Maad. Aya hizo zinataja baadhi ya matunda hayo kuwa ni pamoja na kuimarika imani ya kumfuata bwana na mpendwa wetu al-Habib Muhammad (saw). Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 21 ya Surat al-Ahzab:

لَقَدْ كَانَ لَكُمْ فِي رَسُولِ اللَّهِ أُسْوَةٌ حَسَنَةٌ لِمَنْ كَانَ يَرْجُو اللَّهَ وَالْيَوْمَ الْآخِرَ وَذَكَرَ اللَّهَ كَثِيرًا

Hakika nyinyi mnayo ruwaza njema kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa anayemtarajia Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, na akamkumbuka Mwenyezi Mungu kwa wingi.

Kama ambavyo miongoni mwa baraka za imani juu ya Maad na Ufufuo ni kuimarishwa moyo wa kuharakisha kufanya aina zote za mambo mema. Mwenyezi Mungu anasema katika aya mbili za 114 na 115 za Surat Aal Imraan:

يُؤْمِنُونَ بِاللَّهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ وَيَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنْكَرِ وَيُسَارِعُونَ فِي الْخَيْرَاتِ وَأُولَئِكَ مِنَ الصَّالِحِينَ. وَمَا يَفْعَلُوا مِنْ خَيْرٍ فَلَنْ يُكْفَرُوهُ وَاللَّهُ عَلِيمٌ بِالْمُتَّقِينَ.

Wanamwamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, na wanaamrisha mema na wanakataza maovu na wanaharakia mambo ya kheri. Na hao ndio miongoni mwa watu wema. Na kheri yoyote watakayoifanya hawatanyimwa malipwa yake. Na Mwenyezi Mungu anawajua wenye takwa.

Kama ambavyo kukita mizizi ya imani kuhusu maisha ya Akhera na malipo na adhabu ni njia ya kupata amani na utulivu wa ndani. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema katika aya ya 69 ya Surat al-Maidah:

إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَالَّذِينَ هَادُوا وَالصَّابِئُونَ وَالنَّصَارَى مَنْ آمَنَ بِاللَّهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ وَعَمِلَ صَالِحًا فَلَا خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ.

Hakika wale walioamini, na Mayahudi na Masabii na Wakristo, waliomwamini Mwenyezi Mungu, na Siku ya Mwisho, na wakatenda mema, basi hawatakuwa na khofu wala hawatahuzunika.

Ni wazi pia kwamba kumpwekesha vilivyo Mwenyezi Mungu kunahitajia kuwa na imani juu ya Siku ya Mwisho.

***********

Ndugu wasikilizaji, je, tunaweza kupata katika Kizito cha Pili ambazo ni hadithi za Watu wa Nyumba ya Mtukufu Mtume (saw), jambo lolote linaloweza kufafanua na kutuwekea wazi jibu kuhusiana na faida na matunda yanayopatikana katika kuwa na imani juu ya Maad?

Huu ndio utakaokuwa msingi wa mjadala wetu katika kipindi kijacho cha Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain Inshallah. Tunakushukuruni nyote kwa kuwa pamoja nasi hadi wakati huu, kwaherini.