May 24, 2017 18:25 UTC
  • Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain (164)

Assalaama Aleikum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Hii ni sehemu ya 164 katika mfululizo wa vipindi hivi vinavyojadili na kujibu maswali mbalimbali yanayohusiana na itikadi ya Kiislamu.

Swali la kipindi cha juma hili ni: Je, ni matunda gani muhimu yanayotajwa na hadithi tukufu kuhusiana na imani ya Ufufuo au kwa neno jingine Maad?

Jibu la swali hili bila shaka litatukamilishia swali ambalo tuliuliza katika kipindi kilichopita kuhusiana na matunda yanayotajwa na Quráni Tukufu kuhusiana na suala hilihili ambalo linahusiana na Ufufuo na maisha ya Akhera. Hivyo basi hebu tuzingagtie kwa pamoja hadithi hizi ambazo tutazizungumzia kwa urefu kidogo katika kipindi cha leo, karibuni.

***********

Mtu anayefuatilia kwa karibu hadithi za kutegemewa na kuaminika zilizopokelewa kuhusu imani ya Maad bila shaka atapata kuwa ni nyingi mno na kwamba nyingi kati yazo zinajadili matunda yanayotokana na imani hii kama inavyozungumziwa na kitabu kitakatifu cha Quráni. Tunaona pia kwamba hadithi hizi tukufu zinabainisha wazi mifano ya kimatendo ambayo inamuwezesha mwanadamu kufikia matunda na baraka hizo ambazo zimetajwa na Quráni Tukufu kwa anayezingatia Maad na maisha ya Akhera. Tutaizungumzia mifano hiyo kwa urefu kidogo katika kipindi chetu kijacho Inshallah. Kwa leo tutatosheka kwa kutaja muhimu kati ya mifano hiyo kadiri wakati utakavyoturuhusu.

Tunaanza kwa hadithi mashuhuri ambayo imetajwa kupitia wapokezi wengi tofauti nayo ni ile inayohusiana na miraji yaani kupaa mbinguni kwa Mtume Muhammad (saw). Katika hadithi hiyo Mtume anazungumzia kile alichoona kimeandikwa kwenye milango ya Pepo katika safari yake hiyo ya mbinguni kwa kusema: ‘’Na katika mlango wa nne kati ya milango hiyo palikuwa pameandikwa: La Illah Ila Allah Muhammad Rasul Allah, Aliyyun Waliyullah. Mtu ambaye anamwamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho basi na amkirimu jirani yake, mtu anayemwamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho amkirimu mgeni wake, mtu anayemwamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho awatendee wema wazazi wake, mtu anayemwamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho basi na aseme heri au anyamaze.’’

Kwa kuzingatia maandiko haya matakatifu yanatubainikia wazi matunda kadhaa ya kuwa na imani kuhusiana na Siku ya Mwisho, mojawapo ikiwa ni kwamba imani hii ni njia ya kueneza wema na matendo mema katika jamii nzima. Matunda mengine tunayoyapata kutokana na imani hii ni kuwa ni dhihirisho la kivitendo la kukamilika imani kuhusu Tauhidi, Utume na Uimamu. Kwa msingi huo imani hii ya Siku ya Mwisho ni njia ya kufikia ukamilifu wa imani.

 

Hadithi tukufu pia zinatuongoza katika kuhamu kwamba miongoni mwa matunda na manufaa ya kuwa na imani ya Maad na Siku ya Hesabu huko Akhera ni kuimarisha moyo wa kupambana na shetani na hatimaye kuepuka vishawishi na upotovu wake. Matunda haya yanaashiriwa na hadithi tukufu iliyonukuliwa na Sheikh Hussein bin Said al-Kufi katika kitabu chake cha ál-Mu’min kutoka kwa Mtume Mtukufu (saw) kwamba: ‘’Mtu anayemwamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Akhera, asiketi kwenye kikao ambacho ndani yake Imam anatusiwa au Mwislamu kusengenywa; Mwenyezi Mungu anasema:

وَإِذَا رَأَيْتَ الَّذِينَ يَخُوضُونَ فِي آيَاتِنَا فَأَعْرِضْ عَنْهُمْ حَتَّى يَخُوضُوا فِي حَدِيثٍ غَيْرِهِ وَإِمَّا يُنْسِيَنَّكَ الشَّيْطَانُ فَلَا تَقْعُدْ بَعْدَ الذِّكْرَى مَعَ الْقَوْمِ الظَّالِمِينَ

Na unapowaona wanaoziingilia Aya zetu, basi jitenge nao mpaka waingilie katika mazungumzo mengine. Na kama Shetani akikusahaulisha, basi baada ya kutanabahi usikae pamoja na watu madhaalimu.’’

Tunanufaika pia na hadithi hizo kufahamu kwamba manufaa mengine yanayotokana na imani juu ya Akhera ni kutayarishwa moyo wa mwanadamu kukubali kirahisi mawaidha ya Mwenyezi Mungu na hivyo kuyaendea mambo na matendo mema ambayo yanamridhisha Mwenyezi Mungu Mtukufu. Kwa mfano nasaha ya Mtume Mtukufu (saw) kwa sahaba wake mwema Muadh bin Jabal, ambayo imenukuliwa katika kitabu cha Tuhuf al-Uqul inasema: ‘’Na wakumbushe watu Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho na ufuatilize kwa mawaidha kwa sababu yanawaimarisha na kuwashajiisha kutenda yale yanayomridhisha Mwenyezi Mungu.’’

*********

Ni wazi kuwa kuimarishwa kwa imani ya Maad huimarisha moyo wa takwa na kujiepusha kutenda mambo ambayo Mwenyezi Mungu ameyakataza kwa mu’mini kama anavyoashiria hilo Imam Ali ar-Ridha (as) katika hadithi iliyopokelewa kutoka kwake katika kitabu cha Ilal as-Sharai’ na vitabu vingine. Hadithi hiyo inasema: ‘’Mwenyezi Mungu aliharamisha pombe kutokana na maovu yaliyomo na kubadilisha kwake akili ya wanaoinywa, jambo linalowapelekea wamkane Mwenyezi Mungu na kumzushia Yeye na Mitume wake uongo, pamoja na maovu mengine wanayoyafanya ikiwa ni pamoja na ufisadi, mauaji, tuhuma, zina na uchache wa kijizuia kufanya mambo yaliyoharamishwa. Kwa msingi huo tuliharamisha kila kinywaji kinacholevya kwa sababu kina matokeo yaleyale yanayotokana na pombe. Hivyo kila anayemwamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, kutufuata na kutupenda ajiepushe kila aina ya kileo, kwa sababu hakuna uhusiano (sisi sio kimbilio lake) baina yetu na anayekunywa kileo hicho.’

Kama ambavyo miongoni mwa manufaa yanayotokana na imani juu ya Maah ni kufanya juhudi kubwa za kujijengea nafasi nzuri huko Akhera na kuwafuata Maimamu wa wongofu (as). Kwa mfano sehemu moja ya wasia wa Imam Ali (as) ambayo imenukuliwa katika juzuu ya 7 ya kitabu cha al-Kafi kuhusiana na sadaka na wakfu zake kwa ajili ya manufaa ya Waislamu inasema: ‘Hivi ndivyo alivyoamua Ali bin Abu Talib kuhusiana na mali zake….. katika kutafuta ridhaa ya Mwenyezi Mungu na makao ya Akhera na Mwenyezi Mungu ndiye mwenye kuombwa msaada….. na wala haijuzu kwa Mwislamu anayemwamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Akhera kutoa uamuzi kuhusiana na mali yangu ambayo tayari nimeitolea uamuzi wala kupinga chochote kuhusu suala hilo.’

 

Tunafupisha yale tuliyojifunza katika kipindi cha juma hili kwa kusema kuwa hadithi tukufu zinatufahamisha kwamba manufaa yanayotokana na imani ya Maad au kwa ibara nyingine Ufufuo yanamnufaisha muumini mwenyewe katika maisha yake ya humu duniani na ya Akhera kama ambavyo yanainufaisha jamii nzima kwa ujumla.

Na kwa muhtasari huu ndio tunafikia mwisho wa kipindi kingine cha Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain ambacho mmekisikiliza kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Wassalaam Aleikum Warahmatullahi Wabarakatuh.