Apr 26, 2017 07:13 UTC
  • Maswali yetu na Majibu ya Thaqalain (160)

Assalaam Aleikum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu inayokutangazieni kutoka mjini Tehran.

Swali letu la juma hili linahusiana na Maimamu ambao tumekuwa tukiwazungumzia katika vipindi kadhaa vilivyopina nalo limeulizwa na msikilizaji wetu Bwana Faisal Badri wa mjini Mombasa Kenya ambaye anasema je, ni nini makusudio ya aya tukufu inayosema: Siku tutakapowaita watu kwa Imam wao? Je, ni hao Maimamu ambao munawaamini nyinyi au ni Mtume? Mkisema ni Mamimamu, je mtakuwa mnawafadhilisha Maimamu hao juu ya Mtume?

Inaonekana kutokana na swali la msikilizaji wetu huyu mpendwa kwamba yeye si katika wafuasi wa madrasa ya Thaqalain yaani Quráni Tukufu na kizazi cha Mtume (as). Hii ni kwa sababu wafuasi wote wa madrasa hii wanaamini kwamba Mtume Mtukufu (saw) ndiye bwana na mbora wa viumbe wote tokea wa kwanza, wa sasa na wa baadaye na kwamba hadithi za Ahlu Beit wake (as) zinabainisha wazi jambo hilo. Wanaamini pia kwamba kila walichonacho wao (as) kimerithiwa kutoka kwa mtukufu huyo (saw) na kwamba ndiye wasila wao kuelekea kwa Mwenyezi Mungu. Hii ni hakika muhimu na msingi thabiti katika madrasa ya Thaqalain na kwa hivyo hilo haliwezi kuwa na maana ya cheo na nafasi ya Maimamu (as) kuwa juu na bora zaidi kuliko ya bwana wao na bwana wetu Mtume Mtukufu Muhammad al-Mustafa  (saw). Kwa kuthibiti hakika hiyo ya Kiitikadi tunarejea katika swali la msikilizaji wetu Bwana Faisal Badri ili tupate kujua makusudio ya aya tukufu tuliyotangulia kuisoma, karibuni.

 

Wapenzi wasikilizaji, aya iliyoashiriwa ni ya 71 ya Surat al Isra. Tayari tulizungumzia aya hii miongoni mwa aya zinazozungumzia udharura wa kuwepo Imam katika kila zama ambaye ameteuliwa moja kwa moja na Mwenyezi Mungu ali awe hoja yake kwa watu wa zama hizo. Na aya hii ni jumulishi kwa maana kwamba haizungumzii tu Maimamu wa wongofu bali inawajumuisha pia maimamu wa upotovu. Hii ni kwa sababu jambo linalobainika wazi ni kuwa aya yenyewe imetumia neno ‘’imam’’ bila kulibana kwa maumamu mahsusi na maalumu. Ina maana kwamba kila watu wataitwa Siku ya Kiama kwa msingi wa wale watu waliokuwa wakiwafuata katika maisha yao ya humu duniani. Hivyo basi kwa mfano watu waliokuwa wakiwafuata maimamu wa upotovu wataitwa kwa kuambiwa, enyi wafuasi wa fulani na fulani katika maimamu wapotoshaji! Hivyo watakuwa wametofautishwa na wafuasi wa Maimamu wa wongofu ambao watahutubiwa kwa kutumiwa maneno mazuri kwa mfano, enyi wafuasi wa fulani na fulani katika Maimamu wa wongofu ambao Mwenyezi Mungu aliwateua kwa ajili ya kuwaongoza wanadamu na viube kwa amri yake! Tunapozingatia kwamba aya hii tukufu inatumia ibara ya ‘kila watu’ yaani kila kundi kwenye jamii fulani ya watu, hilo linasisitiza wazi maana tuliyotangulia kuibanisha. Inafahamika wazi kwamba makusudio sio umma wote katika wafuasi wa Manabii (as), kama umma wa Ibrahim, Umma wa Musa, Umma wa Isa au Umma wa Nabii wa Mwisho, Mtume Muhammad (saw). Kwa hivyo inabainika wazi kwamba makusudio ya neno ‘kila watu’ ni makundi maalumu miongoni mwa umma hizo na wala sio umma wote. Lengo la aya hii ni kutofautisha kati ya wafuasi wa Maimamu wa wongofu na wafuasi wa maimamu wa walipotea njia.

 

Kwa maelezo hayo makusudio jumla ya aya hii tukufu yanajumuisha maimamu wote wawe ni wa wongofu au wa kufri kama inavyosema Quráni Tukufu au wa waliopotea kama anavyosema Mtukufu Mtume (saw) katika hadithi iliyopokelewa kutoka kwake kwa njia za madhehebu zote mbili za Kiislamu. Katika hadithi hiyo Mtume (saw) amepokelewa akisema kuwa kile anachokichelea zaidi katika umma wake ni upotovu wa maimamu wa waliopotea njia.

Wapenzi wasikilizaji tunapochambua na kuchunguza maana ya aya hii sio katika duara la madhehebu ya Ahlu Suna bali katika mdhehebu ya wafuasi na Watu wa Nyumba ya Mtume (as), tunapata kwamba aya hii tukufu inaashiria kuwa maana ya ‘kila watu’ wataitwa kwa Imam wao ni kwamba kila kundi katika watu na sio umma wote wa kila nabii litaiwa kwa jina la imam wake maalumu. Jambo lisilo na shaka ni kwamba Mtume Mtukufu (saw) ndiye bwana na mkuu wa Maimamu wote wa wongofu tokea wa mwanzo hadi wa mwisho wao. Ila kwamba makusudio ya aya yenyewe haifungamani na Mtume peke yake (saw) bali yanajumuisha kila aliyefanywa na Mwenyezi Mungu kuwa Imam ambaye watu wa zama zake wataitwa kwa jina lake.

Aya ya 124 ya Surat al-Baqarah inasema wazi kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu alimjaalia Ibrahim Khalil (as) kuwa Imam wa watu katika kipindi cha mwisho cha umri wake mtukufu. Hivyo watu wa zama zake ambao walikubali na kufuata uimamu wake wataitwa Siku ya Kiama kwa jina lake ili kuwatenganisha na wale wapotovu ambao walifuata batili. Na hivihivi ndivyo itakavyofanyika kuhusiana na manabii wengine wote (as) ambao Mwenyezi Mungu aliwafanya kuwa Maimamu wa watu. Watu wa zama zao watakuwa wakiitwa kwa majina ya watukufu hao (as). Suala hilihili pia linathibiti kuhusiana na Bwana wa Mitume na Manabii wote al-Habib al-Mustafa (saw). Wafuasi wake wa kweli na waaminifu katika zama zake wataitwa kwa jina lake Siku ya Kiama na hivyo kuwatenganisha na wale ambao hawakumfuata. Na maana hii inathibitishwa na kusisitizwa na maandiko ya Quráni Tukufu yanayosema: Siku tutakapowaita kila kikundi cha watu kwa Imam wao.  Aya hii inasisitiza juu ya kutenganishwa baina ya ufuasi wa haki na ufuasi wa batili ambapo Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema katika aya mbili za 71 na 72 za Surat al-Israa: Siku tutakapowaita kila kikundi cha watu kwa Imam wao. Basi atakayepewa kitabu chake kwa mkono wake wa kulia, basi hao watasoma kitabu chao wala hawatadhulumiwa hata chembe. Na aliyekuwa hapa kipofu, basi atakuwa kipofu Akhera, na atakuwa aliyeipotea zaidi Njia.

 

Wapenzi wasikilizaji kwa maelezo hayo tunapata kujua kutokana na ufafanuzi wa aya hii tukufu kwamba makusudio ya maneno ‘kwa Imam wao’ yanajumuisha Maimamu wa haki na maimamu wa waliopotea katika kila zama na lengo ni kutenganisha kati ya wafuasi wa haki na wafuasi wa batili. Na maana hii ya Quráni Tukufu imeashiriwa na hadithi tukufu ambazo zimenukuliwa na kupokelewa na madhehebu zote mbili za Kiislamu na tutakunukulieni mifano ya hadithi hizo katika kipindi chetu kijacho Inshallah.

Hivyo kufikia hapa ndio tunafikia mwisho wa kipindi hiki cha Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain ambacho kimekujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Tunakushukuruni nyote wapenzi wasikilizaji kwa kututegea sikio hadi mwisho wa kipindi. Basi hadi juma lijalo ambapo tutakuwa tunakuleteeni kipindi kingine cha Maswali yetu na Majibu ya Thaqalain tunakuageni nyote huku tukikutakieni usikilizaji mzuri wa vipindi vyetu vilivyosalia, kwaherini.