Jumatatu 8 Mei 2017
Leo ni Jumatatu 11 Shaaban 1438 Hijria, sawa na Mei 8, 2017.
Siku kama ya leo miaka 1405 iliyopita, alizaliwa mtukufu Ali bin Hussein, mwana mkubwa wa kiume wa Imam Hussein A.S na mjukuu wa Mtume Muhammad SAW mjini Madina. Ali bin Hussein ambaye alifanana sana na babu yake Mtume Mtukufu SAW, alinufaika sana na bahari ya maadili mema na mafunzo ya dini ya Kiislamu kwa kuwa pamoja na babu yake Imam Ali AS na baba yake Imam Hussein AS. Mtukufu Ali bin Hussein, alikuwa maarufu kwa jina la Ali Akbar yaani Ali mkubwa kutokana na jina lake kufanana na majina ya mdogo wake ambaye pia alikuwa na jina hilo la Ali.
Ali Akbar alikuwa na nafasi muhimu katika mapambano ya baba yake dhidi ya dhulma na uasi wa utawala wa Bani Umayyah. Aliuawa shahidi tarehe 10 Muharram mwaka 61 Hijiria baada ya kuingia katika medani ya vita na kupigana kishujaa katika mapambano ya jeshi la Yazid bin Muawiyah na Imam Hussein A.S na wafuasi wake.

Tarehe nane ya kila mwezi Mei inatambuliwa kuwa siku ya Msalaba Mwekundu au Hilali Nyekundu. Msalaba Mwekundu ni shirika la kimataifa ambalo liliundwa kwa ajili ya kutuliza machungu ya wanadamu na kulinda maendeleo ya sekta ya afya ya kijamii kwa mujibu wa mkataba wa Geneva, Uswisi hapo mwaka 1864 Miladia. Jean Henri Dunant raia wa Uswisi, alikuwa na nafasi kubwa katika kuundwa shirika hilo la kimataifa. Hii ni kwa kuwa mwaka 1862 alitoa pendekezo la kusaidiwa wagonjwa na majeruhi wa kijeshi, pendekezo ambalo lilipokelewa na asasi za masuala ya misaada ya kibinaadamu na kukubaliwa hapo baadaye na kongamano la kimataifa mjini Geneva mwaka 1864. Ni baada ya hapo ndipo shirika hilo la Msalaba Mwekundu likaundwa na kuanza kuenea duniani. Katika nchi za Kiislamu shirika hilo linaitwa kwa jina la Hilali Nyekundu.

Siku kama ya leo miaka 222 iliyopita, Antoine Lavoisier msomi wa Ufaransa alinyongwa kufuatia kujiri harakati ya mapinduzi makubwa ya nchi hiyo. Lavoisier alikuwa mvumbuzi na msomi mashuhuri wa Ufaransa huku akiwa pia mwanzilishi wa kanuni ya kielimu ya elimu ya kemia. Licha ya kuhitimu awali masomo yake ya sheria, lakini kutokana na kwamba alipendelea sana elimu ya sayansi akaamua kuingia uwanja huo. Akiwa na miaka 25 alichaguliwa kujiunga na Chuo cha Kifalme cha Sayansi. Katika uwanja huo alifanikiwa kuvumbua gesi ya Oxygen na umuhimu wa matumizi na pia kuvumbua muundo wa hewa. Antoine Lavoisier ndiye msomi wa kwanza aliyethibitisha kuwa joto la mwili linatokana na mmeng'enyo wa sukari mwilini na kwa ajili hiyo akatambuliwa kuwa mwasisi wa elimu ya tiba na biokemia. Itafahamika kuwa, baada ya kujiri mapinduzi makubwa ya Ufaransa kila mtu aliyekuwa na mahusiano na utawala wa kifalme wa nchi hiyo alikamatwa na kuhukumiwa. Ni kwa msingi huo ndipo Antoine Lavoisier akatiwa mbaroni na kisha kuhukumiwa na kunyongwa katika siku kama ya leo mwaka 1794 Miladia akiwa na umri wa miaka 51.
Siku kama ya leo miaka 368 iliyopita inayosadifiana na tarehe 11 Shaaban 1070 Hijria, Mohammad Taqi Majlisi maarufu kama Majlisi wa Kwanza, msomi na Arif mkubwa Muirani aliaga dunia. Alizaliwa mwaka 1003 Hijria Qamari katika mji wa Isfahan ambao zama hizo ulikuwa mji mkuu wa silsila ya watawala wa Safavi. Alizaliwa wakati Iran ilikuwa inashuhudia ustawi mkubwa wa kiutamaduni na kielimu. Familia ya Allamah Majlisi ilikuwa ya wasomi na wanazuoni kiasi kwamba alipata sehemu ya masomo yake kutoka kwa baba yake na jamaa zake wengine katika familia. Baada ya kujifunza fiqhi, itikadi na tafsiri katika darasa la Sheikh Bahai, alipata umashuhuri kama alim na arif mkubwa. Alikwea daraja la juu la masomo baada ya kutembelea mji wa Najaf al Ashraf nchini Iraq. Baad ya kurejea Isfahan alijishughulisha kufunza na alitambulika kwa umahiri wake katika fiqhi, hadithi, tafsiri na itikadi.