Jun 20, 2017 02:27 UTC
  • Jumanne 20 Juni, 2017

Leo ni Jumanne tarehe 25 Ramadhani mwaka 1438 Hijria sawa na tarehe 20 Juni mwaka 2017.

Siku kama ya leo miaka 15 iliyopita alifariki dunia Allamah Sayyid Saiid Akhtar Rizvi, mlinganiaji mkubwa wa Uislamu katika kanda ya mashariki mwa Afrika. Hujjatul Islam Walmuslimin Rizvi alizaliwa huko mashariki mwa India na baada ya kupata masomo ya awali kwa baba yake alijifunza masomo ya juu na lugha za Kingereza, Kifarsi na Urdu na kupata daraja ya Fakhrur Afadhil. Baada ya kulingania dini kwa miaka mingi nchini India, Sayyid Akhtar Rizvi alihisi wajibu wa kuelekea Tanzania, barani Afrika na kuanza kueneza maarifa ya dini na mafundisho ya Ahlubaiti wa Mtume (saw). Allamah Rizvi ameandika na kufasiri vitabu vingi kwa lugha mbalimbali ikiwa ni pamoja na tafsiri ya Qur'ani ya al Miizan na kitabu cha Al Ghadir na kujenga makumi ya misikiti, madrasa, maktaba na zahanati. Alifariki dunia jijini Dar es Salaam katika siku kama ya leo akiwa na umri wa miaka 76.

Siku kama ya leo miaka 23 iliyopita magaidi wa kundi la Munafiqin walitenda jinai kubwa ya kutisha katika Haram tukufu ya Imam Ridha (a.s) mjukuu wa Mtume Mtukufu (s.a.w) katika mji mtakatifu wa Mash'had. Bomu liliripuka ndani ya Haram tukufu ya Imam Ridha (a.s) alasiri ya siku ya Ashura mwaka huo wakati watu walipokuwa wakifanya ziara na marasimu ya kukumbuka mapambano ya kihistoria ya kuuawa shahidi Imam Hussein (a.s). Makumi ya waumini na wapenzi wa Ahlul Bait (a.s) waliuliwa shahidi au kujeruhiwa katika haram hiyo. Mlipuko huo ulisababisha hasara na maafa mengi.

Haram ya Imam Ridhaa (as) katika mji wa Mash'had

Miaka 105 iliyopita katika siku kama ya leo msomi wa Poland kwa jina la Casimir Funk kwa mara ya kwanza kabisa alifanikiwa kugundua vitamin au virutubisho. Baada ya uhakiki mwingi Dakta Casimir Funk aligundua kwamba vyakula vinavyotumiwa na mwanadamu vina baadhi ya virutubisho (vitamins) ambavyo japokuwa ni vichache sana lakini vina udharura mkubwa katika ukuaji na usalama wa mwili na akaamua kuvipa jina la Vitamini. Kuna aina mbalimbali za vitamin kama A, B, C, D na E, na kila moja ina sifa za kipekee na matumizi ya aina yake katika mwili.

Siku kama ya leo miaka 117 iliyopita ilianza Harakati ya Wanamasumbwi nchini Uchina. Wanamasumbwi lilikuwa jina walilopewa wanajeshi wa China waliosimama kupambana na ubeberu wa nchi za kigeni hususan za Magharibi ulioambatana na harakati za wamishonari wa Kikristo ndani ya China. Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na wanamasumbwi hao ni kuteka balozi za nchi za Magharibi katika mji wa Beijing na kupambana vikali na shughuli za wahubiri wa Kikristo kutoka Ulaya. Hata hivyo Harakati ya Wanamasumbwi wa Kichina ilikandamizwa na majeshi ya Ulaya, Marekani na Japan na serikali ya China ikalazimika kulipa gharama kubwa kwa nchi hizo.

Harakati ya Wanamasumbwi nchini Uchina

na siku kama ya leo miaka 142 iliyopita kisiwa cha Okinawa kinachopatikana katika bahari ya Pacific huko Japan kilidhibitiwa na jeshi la nchi hiyo. Hata hivyo mwishoni mwa Vita vya Pili vya Dunia kisiwa hicho cha kistratijia chenye ukubwa wa kilomita mraba 1250 kilikaliwa kwa mabavu na majeshi ya Marekani licha ya mapambano makali ya jeshi la Japan. Jeshi la Marekani liliondoka Japan mwaka 1958 lakini kisiwa cha Okinawa kiliendelea kudhibitiwa na Wamarekani. Mwaka 1972 vikosi vya Marekani vilisitisha ukaliaji wa mabavu wa kisiwa hicho kufuatia mazungumzo marefu kati ya Washington na Tokyo.

Kisiwa cha Okinawa, Japan

 

Tags