Jumanne 27 Juni, 2017
Leo ni Jumanne tarehe Pili Shawwal 1438 Hijria, inayosadifiana na tarehe 27 Juni 2017.
Siku kama ya leo miaka 36 iliyopita, sawa na tarehe 6 Tir 1360 Hijria Shamsia, Ayatullahil Udhma Ali Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu akiwa mjumbe wa Imam Khomeini katika Baraza Kuu la Ulinzi na Imamu wa Swala ya Ijumaa mjini Tehran, alinusurika kifo baada ya kundi la kigaidi la Munafikiin kumtegea bomu wakati alipokuwa akitoa hotuba katika mojawapo ya misikiti ya Tehran. Kwenye tukio hilo la kigaidi, Ayatullah Khamenei alijeruhiwa vibaya mkono wake wa kulia.
Siku kama ya leo miaka 40 iliyopita inayosadifiana na 27 Juni 1977, nchi ya Djibouti iliyoko karibu na eneo la Pembe ya Afrika ilijipatia uhuru wake kutoka kwa mkoloni Mfaransa baada ya kupita miaka kadhaa ya harakati ya kupigania uhuru. Tokea mwaka 1896 nchi hiyo ilikuwa ikijulikana kwa jina la Somalia Ufaransa na kuwa chini ya himaya ya Ufaransa, amma baada ya kupita miongo minane, hatimaye nchi hiyo iliweza kujipatia uhuru wake. Djibouti ilikuwa ni nchi ya mwisho kujiunga na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu. Djibouti inahesabiwa kuwa nchi muhimu iliyoko katika eneo la kiistratijia kwa kuwa inapakana na Bahari Nyekundu na Bahari ya Hindi, kweye eneo la lango la bahari lijulikanalo kama 'Bab Mandab'.
Tarehe 27 Juni 1993, Marekani ilirusha makombora 23 huko Baghdad mji mkuu wa Iraq na pambizoni mwa mji huo. Shambulio hilo lilifanyika kwa kisingizo kwamba viongozi wa utawala wa zamani wa Iraq walitaka kumuuwa George Bush 'baba', Rais wa zamani wa Marekani wakati alipokuwa safarini nchini Kuwait mwezi April mwaka huo huo. Shambulio hilo lilipelekea watu sita kuuawa na jengo la makao makuu ya Taasisi ya Usalama ya Iraq kuharibiwa kabisa.
Siku kama ya leo miaka 834 iliyopita, alifariki dunia Abubakar Naqash, msomi wa Qur’an na hadithi mashuhuri wa Iraq. Akiwa kijana mdogo, Naqash alifanya safari mjini Baghdad na kupata kusoma elimu ya dini kwa maulama wakubwa wa zama hizo. Baada ya hapo Abubakar alifanya safari katika nchi tofauti za Kiislamu kwa ajili ya kufanya utafiti katika uga wa maarifa ya dini hususan hadithi. Msomi huyo alikuwa mashuhuri katika zama zake kwa kusoma Qur’an na kunukuu hadithi. Ibn Nadim, mwanahistoria maarufu wa Kiislamu aliyeandika kitabu cha al-Fahrast, alichukua athari nyingi kutoka kwa Abubakr Naqash.