Jul 05, 2017 04:04 UTC
  • Jumatano 5 Julai, 2017

Leo ni Jumatano tarehe 110 Shawwal 1438 Hijria, inayosadifiana na tarehe 5 Julai 2017.

Siku kama ya leo miaka 206 iliyopita, nchi ya Venezuela ilijitangazia uhuru wake na kwa sababu hiyo, tarehe 5 Julai, hutambuliwa kama siku ya kitaifa nchini humo. Tangu mwanzoni mwa karne ya 16 Miladia, na kwa kipindi cha karne tatu Venezuela ilikuwa chini ya ukoloni wa Uhispania. Katika kipindi cha ukoloni huo, raia wa nchi hiyo walipatwa na matatizo mengi, kiasi kwamba makumi ya maelfu ya Wahindi Wekundu ambao ni raia asili wa taifa hilo waliuawa na mahala pao kuchukuliwa na Wahispania. Mwanzoni mwa karne ya 19 Miladia, mapambano ya wananchi yalianza chini ya uongozi wa Francisco Miranda na kuzaa matunda katika siku kama ya leo mwaka 1811.

Siku kama ya leo miaka 184 iliyopita, alifariki dunia Nicéphore Niépce, mvumbuzi wa kamera. Niépce alifanikiwa kusajili kwa mara ya kwanza uvumbuzi huo, mnamo mwaka 1826, baada ya kufanya majaribio kadhaa ya kielimu katika uwanja huo.

Nicéphore Niépce

Siku kama ya leo miaka 55 iliyopita, wananchi wa Algeria walipata uhuru dhidi ya wavamizi wa Ufaransa baada ya mapambano makali na ya muda mrefu na wavamizi hao. Ufaransa iliikalia kwa mabavu Algeria kwa kutegemea jeshi lake kubwa mnamo mwaka 1830. Kwa kipindi cha miaka 130 ya kukoloniwa taifa hilo, raia wa Algeria waliasisi harakati kadhaa za kupigania uhuru zilizokuwa zikiongozwa na Amir Abdulqadir al Jazairi, ambazo hata hivyo zilikabiliwa na ukandamizaji mkubwa wa jeshi la Ufaransa. Hata hivyo harakati hizo zilishika kasi zaidi na kuzaa matunda baada ya kumalizika Vita vya Pili vya Dunia na kujipatia uhuru wake miaka 53 iliyopita katika siku kama ya leo.

Bendera ya Algeria

Siku kama ya leo miaka 40 iliyopita, Jenerali Muhammad Zia-ul-Haq alifanya mapinduzi ya kijeshi yaliyoiondoa madarakani serikali ya Zulfiqar Ali Bhutto nchini Pakistan. Muhammad Zia-ul-Haq alitwaa madaraka yote ya waziri mkuu na rais wa Jamhuri ya Pakistan na mbali na kuwanyonga Zulfiqar Bhutto na wapinzani wake wengine, alivunja mabunge ya nchi hiyo na kusimamisha shughuli zote za vyama vya siasa nchini Pakistan. Zia-ul-Haq aliuawa katika ajali ya ndege akiwa na maafisa kadhaa wa jeshi la Pakistan, na utawala wake ukakomea hapo.

enerali Muhammad Zia-ul-Haq

Na siku kama ya leo miaka 35 iliyopita, wanadiplomasia watatu na mwandishi habari mmoja wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran walitekwa nyara na wapiganaji wa chama cha Falanja cha Lebanon kaskazini mwa Beirut. Wanadiplomasia hao na mwandishi wa habari wa Iran walitekwa nyara wakati walipokuwa wakielekea kazini katika ubalozi wa Iran huko Beirut. Wakati tukio hilo lilipojiri jeshi la utawala wa Kizayuni lilikuwa limeishambulia Lebanon na chama cha Falanja kilikuwa na ushirikiano wa karibu na utawala ghasibu wa Israel. Ushahidi na nyaraka zilizopo zinaonyesha kuwa raia hao wa Iran wanashikiliwa na utawala wa Kizayuni wa Israel.

 

Tags