Jul 26, 2017 03:50 UTC
  • Jumatano Julai 26, 2017

Leo ni Jumatano tarehe Pili Dhulqaada 1438 Hijria 1438 Hijria, sawa na Julai 26, 2017.

Siku kama ya leo miaka 38 iliyopita, yaani tarehe 26 Julai mwaka 1979 Miladia, Zuheir Muhsein Katibu, mkuu wa wakati huo wa Harakati ya as-Sa'iqa tawi la Harakati ya Ukombozi ya Palestina (PLO) aliuawa kigaidi na maajenti wa shirika la ujasusi la utawala wa Kizayuni (Mossad) huko katika mji wa Cannes nchini Ufaransa. Magaidi wa Kizayuni walikimbia na kutoweka baada ya kufanya mauaji hayo na polisi wa Ufaransa wakidai kuwa hawakupata uthibitisho kwamba Mossad ilihusika na mauaji hayo.

Zuheir Muhsein Katibu

Tarehe 26 Julai miaka 52 iliyopita visiwa vya Maldives huko kusini mwa bara Asia vilipata uhuru. Visiwa vya Maldives vilivamiwa na kukaliwa kwa mabavu na Wareno mwanzoni mwa karne ya 16. Visiwa hivyo baadaye vilidhibitiwa na Waholanzi na Wafaransa na hatimaye mwishoni mwa karne ya 19, vikakaliwa na Waingereza.

Bendera ya Maldives

Siku kama ya leo miaka 61 iliyopita, Gamal Abdu l-Nasser rais wa wakati huo wa Misri alitangaza habari ya kutaifishwa Mfereji wa Suez. Mfereji huo ulianzishwa mwaka 1896 baada ya Misri kukaliwa kwa mabavu na Uingereza na kwa utaratibu huo, njia ya baharini baina ya Ulaya na Asia ikawa imefupishwa. Udhibiti wa Uingereza na Ufaransa kwa Mfereji wa Suez uliendelea hadi serikali ya Abdu l-Nasser ilipokuja kuutaifisha na kuutangaza kuwa mali ya taifa. Hatua hiyo ilifuatiwa na mashambulio ya kijeshi ya Uingereza, Ufaransa na utawala dhalimu wa Israel. Hata hivyo mashinikizo ya kimataifa dhidi ya madola vamizi na mapambano ya wananchi Waislamu wa Misri, yalivifanya vikosi vamizi viondoke katika kanali hiyo muhimu na mfereji huo ukawa katika miliki ya serikali na taifa la Misri.

Gamal Abdu l-Nasser

Siku kama ya leo miaka 73 iliyopita, Reza Pahlavi maarufu kwa jina la Rezakhan mwasisi wa silsila ya Pahlavi nchini Iran alifariki dunia nchini Afrika Kusini baada ya kukalia kiti cha usultani kwa miaka 16 na kuwa uhamishoni kwa miaka mitatu. Rezakhan alizaliwa mwaka 1257 Hijria Shamsiya sawa na mwaka 1878, katika mojawapo ya vijiji vya kaskazini mwa Iran. Mwaka 1299 Hijria Shamsiya, sawa na mwaka 1920, Miladia Rezakhan alipewa amri na Uingereza ya kufanya mapinduzi nchini Iran ili kulinda maslahi ya serikali ya London, wakati alipokuwa afisa wa jeshi la Iran. Baadaye alikuwa Waziri wa Ulinzi na kisha Waziri Mkuu. Hatimaye mwaka 1304 Hijria Shamsiya sawa na mwaka 1925, Rezakhan alianzisha utawala wa silsila ya Qajar na kukalia kiti cha usultani nchini Iran licha ya kupingwa na wanazuoni na wanasiasa wapigania uhuru.

Maiti ya Reza Shah

Siku kama ya leo miaka 170 iliyopita, nchi ya Kiafrika ya Liberia ilipata uhuru na siku hiyo hutambuliwa nchini humo kama siku ya kitaifa. Liberia iko katika mwambao wa Bahari ya Atlantic na inapakana na nchi za Guinea, Sierra Leone na Ivory Coast. Idadi kubwa ya raia wa nchi hiyo wanafuata dini za kitamaduni na kimila, na asilimia 16 ya raia wake ni Waislamu. Lugha rasmi ya raia wa Liberia ni Kingereza. 

Bendera ya Liberia

Na miaka 1127 iliyopita katika siku kama ya leo, aliaga dunia Ibn Khuzaima, mpokeaji wa hadithi na faqihi mashuhuri wa karne ya nne Hijria. Ibn Khuzaima alizaliwa mwaka 223 Hijria na alifanya safari katika pembe mbalimbali duniani wakati wa ujana wake kwa lengo la kujipatia elimu mbalimbali za kidini. Mwanazuoni huyo wa Kiislamu ameandika vitabu vingi vya thamani na muhimu zaidi ni kile alichokipa jina la al Tauhidi wa Ithbati Sifatir Rabb. 

 

Tags