Aug 10, 2017 04:23 UTC
  • Alkhamisi 10 Agosti, 2017

Leo ni Alkhamisi tarehe 17 Mfunguo Pili Dhilqaada 1438 Hijria sawa na tarehe 10 Agosti 2017.

Siku kama ya leo miaka 1259 iliyopita Imam Mussa al Kadhim (as) ambaye ni miongoni mwa Ahlubait wa Mtume wetu Muhammad (saw) alibaidishwa kutoka Madina na kupelekwa Iraq kwa amri ya mtawala dhalimu, Haroun Rashid. Mtukufu huyo aliwasili Iraq tarehe 7 Dhilhijja 179 Hijria na kufungwa katika jela mji huo. Kwa muda, Imam aliwekwa katika jela ya Issa bin Jaafar aliyekuwa mtawala wa Basra lakini mtawala huyo alimwandikia barua Haroun Rashid akimuomba amkabidhi Imam kwa mtu mwingine kwa sababu hakupata ushahidi wowote dhidi ya mtukufu huyo. Haroun Rashid alimpeleka tena uhamishoni Imam mjini Baghdad na akamtaka waziri wake, Fadhl bin Rabii amuue mjukuu huyo wa Mtume. Waziri huyo alikataa na hivyo Haroun alimtaka mtu aliyejulikana kwa jina la Yahya bin Khalid Barmaki atekeleze amri hiyo. Hatimaye Imam Kadhim (as) aliuuliwa shahidi na muovu huyo kwa amri ya mtawala Haroun Rashid.

Siku kama ya leo miaka 97 iliyopita, yalitiwa saini makubaliano yaliyojulikana kwa jina la The Treaty of Sèvres kati ya utawala wa Othmaniya uliokuwa umeshindwa katika Vita vya Kwanza vya dunia na waitifaki wake. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, utawala wa dola ya Othmaniya ulipoteza karibu asilimia 80 ya ardhi yake iliyokuwa ikiitawala, na kupunguza eneo ililokuwa ikilitawala kutoka kilomita mraba milioni tatu hadi kilomita mraba laki sita tu. Makubaliano hayo yalitambua rasmi makubaliano ya awali ya Ufaransa na Uingereza juu ya kugawana ardhi iliyokuwa ikitawaliwa na dola ya Othmania, ambapo Uingereza ilizitawala Iraq, Jordan na Palestina na Ufaransa nayo ilizitwaa na kuzidhibiti Syria na Lebanon.

The Treaty of Sèvres

Siku kama ya leo miaka 80 iliyopita, vilianza vita vya miaka miwili kati ya Japan na China juu ya mzozo wa maeneo ya Yangtze na Canton ambayo yalikuwa maeneo ya kistratijia ya ardhi ya China. Canton ilikuwa bandari muhimu mno huko kusini mwa China ambayo Wachina walipigana vita vya miaka miwili kuilinda mbele ya uvamizi wa Wajapani. Hata hivyo na baada ya kupata hasara kubwa tarehe 25 Aprili 1939 bandari ya Canton ikatwaliwa na Japan. Utawala wa Japan uliendelea kujipanua katika ardhi ya China kwa kudhibiti maeneo mengine ya mashariki mwa nchi hiyo baada ya kuanza Vita vya Pili vya Dunia. Hata hivyo Wajapani walilazimika kurudi nyuma kutokana na mapambano makali ya wananchi wa China.

vita vya Japan na China

Siku kama ya leo miaka 72 iliyopita, kufuatia kushindwa kikamilifu Japan katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia na kwa mujibu wa maazimio ya Kongamano la Potsdam, maeneo ya kaskazini mwa Korea yalidhibitiwa na Jeshi Jekundu la Urusi ya Zamani. Kabla ya kushindwa Japan, maeneo hayo yalikuwa chini ya udhibiti wa nchi hiyo. Aidha baada ya siku chache maeneo ya kusini ambayo ni kisiwa  yakadhibitiwa na Marekani. Kudhibitiwa maeneo ya kaskazini na kusini ya Korea ulikuwa utangulizi wa kugawanywa ardhi hiyo katika nchi mbili za Korea ya Kaskazini na Korea ya Kusini.

Peninsula ya Korea

Siku kama ya leo miaka 83 iliyopita alifariki dunia Ayatullahil Udhma Sheikh Abdulkarim Hairi Yazdi fakihi na mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu ambaye aliasisi chuo kikuu cha kidini cha Qum. Alimu huyo alizaliwa katika mji wa Yazd katikati mwa Iran na baada ya kupata elimu ya mwanzo alielekea nchini Iraq ili kuendelea na masomo ambako alipata elimu na maarifa kutoka kwa maulamaa maarufu wa zama hizo na kufikia daraja ya juu ya ijitihad. Ayatullah Hairi Yazdi aliporejea Iran alihisi haja ya kuwepo chuo chenye nguvu cha elimu ya dini na kwa minajili hiyo mwaka 1340 Hijiria Shamsia alinzisha Hauza ya Qum ambayo ni chuo kikuu cha kidini katika mji mtakatifu wa Qum. Hauza ya Qum ilipanuka kwa kasi na hivi sasa ni miongoni mwa vituo muhimu vya elimu katika ulimwengu wa Kiislamu.

Ayatullahil Udhmaa Abdul Karim Hairi Yazdi

 

Tags