Sep 06, 2017 06:44 UTC

Sura ya Al-Ahzab, aya ya 1-5 (Darsa ya 744)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Baada ya kukamilisha tarjumi na maelezo ya sura ya 32 ya As-Sajdah, katika darsa hii ya 744 tutaanza kuzungumzia sura ya 33 ya Ahzab. Suratul-Ahzab imeteremshwa Madina na ina aya 73. Karibu aya 20 za sura hii zinazungumzia vita vya Ahzab ambavyo kutokana na kuchimbwa mahandaki na Waislamu kandokando ya mji wa Madina ni mashuhuri pia kwa jina la Vita vya Khandaki.

Tunaianza darsa yetu ya kwa aya ya mwanzo hadi ya tatu ya sura hiyo ambazo zinasema:

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ اتَّقِ اللَّـهَ وَلَا تُطِعِ الْكَافِرِينَ وَالْمُنَافِقِينَ ۗ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَلِيمًا حَكِيمًا

Ewe Nabii! Mche Mwenyezi Mungu wala usiwat'ii makafiri na wanaafiki. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi, Mwenye hikima.

وَاتَّبِعْ مَا يُوحَىٰ إِلَيْكَ مِن رَّبِّكَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرًا

Na fuata uliyo funuliwa kwa wahyi kutoka kwa Mola wako Mlezi. Hakika Mwenyezi Mungu anazo khabari za mnayo yatenda.

وَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّـهِ ۚ وَكَفَىٰ بِاللَّـهِ وَكِيلًا

Na mtegemee Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa ni wa kutegemewa.

Kama ilivyopokewa katika hadithi na vitabu vya historia, baadhi ya viongozi wa washirikina wa Makka akiwemo Abu Sufyan walimwambia Bwana Mtume Muhammad SAW kwamba kama utaacha kuwasema vibaya miungu yetu, na sisi pia tutaacha kukubughudhi na tutakuruhusu uwatangazie watu dini yako. Katika aya hizi tulizosoma Allah SW anamuusia Bwana Mtume kwa kumtaka ajihadhari na mapendekezo ya aina hiyo ya kufanya mapatano, kwamba asikubali kufikia maridhiano na maadui wa Uislamu kwa sababu ya kutaka kufanya tablighi na kutangaza dini yake na kuacha kukabiliana na kufru na shirki. Tab'an ni wazi pia kwamba maadui nao hawatoacha kufanya njama dhidi yako, hivyo inapasa muda wote utawakali na kumtegemea Mwenyezi Mungu na kuomba auni na msaada kwake, kwani Yeye Mola anatosha kwa muumini kumkabidhi na kumwachia mambo yake yote.

Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kufanya mapatano ya namna yoyote ile na maadui wa dini ambayo yataishia kutii matakwa yao hakuendani na taqwa na uchaji Mungu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa wanafiki wa ndani wako kitu kimoja na wana fikra moja na maadui wa nje, hivyo inapasa kujihadhari nao. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba badala ya kufanya kila njia ili kuwaridhisha makafiri tujitahidi kufuata na kushikamana na mafundisho ya dini yetu japokuwa jambo hilo wao hawalifurahii. Wa aidha tunajifunza kutokana na aya hizi kuwa kutowatii makafiri na wanafiki na kuamua kufuata njia ya wahyi kuna matatizo na misukosuko mbalimbali. Msukumo mkubwa na muhimu zaidi wa kumfanya mtu awe na subira na kuweza kusimama imara ni kutawakali na kumtegemea Allah, kwani Yeye ni mlinzi bora kabisa wa waumini.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya nne ambayo inasema:

مَّا جَعَلَ اللَّـهُ لِرَجُلٍ مِّن قَلْبَيْنِ فِي جَوْفِهِ ۚ وَمَا جَعَلَ أَزْوَاجَكُمُ اللَّائِي تُظَاهِرُونَ مِنْهُنَّ أُمَّهَاتِكُمْ ۚ وَمَا جَعَلَ أَدْعِيَاءَكُمْ أَبْنَاءَكُمْ ۚ ذَٰلِكُمْ قَوْلُكُم بِأَفْوَاهِكُمْ ۖ وَاللَّـهُ يَقُولُ الْحَقَّ وَهُوَ يَهْدِي السَّبِيلَ

Mwenyezi Mungu hakumwekea mtu yeyote kuwa ana nyoyo mbili ndani ya mwili wake. Wala hakuwafanya wake zenu - ambao mnawalinganisha migongo yao na migongo ya mama zenu - kuwa ni mama zenu. Wala hakuwafanya watoto wenu wa kupanga kuwa ni wana wenu khasa. Hayo ni maneno ya vinywa vyenu tu. Na Mwenyezi Mungu ndiye anaye sema kweli, naye ndiye anaye ongoza Njia.

Aya zilizotangulia zilimkataza Bwana Mtume na waumini kuwafuata na kuwatii makafiri. Aya hii inaashiria mifano kadhaa ya mambo ya khurafa, uzushi na upotofu wa washirikina na kueleza kuwa: Mwenyezi Mungu hayakubali mambo ya aina hiyo ambayo ni batili na ya upotofu, kwa hivyo nyinyi jiwekeni mbali nayo.  Na sababu ni kuwa mapenzi ya vitu viwili vinavyokinzana hayawezi kukaa ndani ya moyo mmoja wa mtu. Kumpenda Mwenyezi Mungu na kuwapenda washirikina na makafiri hakukusanyiki mahala pamoja. Kama mnampenda Mwenyezi Mungu basi mnapaswa mumtii Yeye na kujiweka mbali na maadui wa dini.

Moja ya mienendo isiyo sahihi iliyokuwepo zama za ujahilia ilikuwa ni kwamba kila mume anapokerwa au kumkasirikia mkewe alikuwa akimwambia: Wewe kuanzia sasa ni sawa na mama yangu; na baada ya hapo akawa hafanyi naye tena tendo la ndoa. Hali ya kuwa mke hawezi katu kuwa sawa na mama wa mtu. Hakika hayo yalikuwa maneno mabaya na yasiyofaa, ambayo watu walikuwa wakiyasema kwa madhumuni ya kuonyesha walivyochukizwa na wake zao.

Imani nyengie potofu na ya khurafa iliyokuwepo zama hizo ni kwamba, wakati wowote mtu alipomchukua mtoto wa kiume na kumfanya mwanawe, basi alimhesabu kuwa ni sawa na mwanawe wa kumzaa, na hivyo kumfanya awe na haki zote ambazo mtoto anapata kwa baba yake. Mtoto huyo alikuwa akipata urithi kwa baba yake wa kumlea, na baba mtu naye akimrithi mwanawe huyo wa kupanga. Aidha kama mmoja wao alifariki dunia au alimwacha mke wake ilikuwa haramu kwa mmoja wao kumuoa mtalikiwa wa mwenzake.

Uislamu ulipokuja, ulipambana na fikra hizo za ujahilia na ukapambanua na kumtafautisha mtoto wa kulea na mwana halisi wa mtu. Kwa kutoa mfano, baada ya Zaid bin Haritha, mtoto wa kupanga wa Bwana Mtume Muhammad SAW kumpa talaka mkewe, Mwenyezi Mungu alimwamuru Bwana Mtume amuoe mwanamke huyo aliyeachwa na Zaid ili kufuta moja kwa moja desturi hiyo potofu ya ujahilia katika jamii.

Kisha aya inaendelea kwa kuashiria msingi mmoja mkuu na kueleza kwamba matukio halisi hayawezi kubadilishwa kwa kauli na maneno na kupanga hukumu kwa msingi wa kauli hizo. Mathalani, kusema mke wangu ni mama yangu hakubadilishi uhalisia wa mambo, kama ambavyo kumkubali mtoto wa kupanga hakumfanyi awe mwana halisi wa mtu.

Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba mapenzi mawili yanayokinzana hayawezi kukaa ndani ya moyo mmoja. Kupenda kunaandamana na kufuata na kutii. Haiwezekani kiimani kumwamini Mwenyezi Mungu lakini kimatendo kufuata njia ya mwenendo wa makafiri; vinginevyo, labda mtu awe na unafiki ndani ya moyo wake. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, uhusiano wa wazazi kwa watoto wao ni uhusiano halisi na wa kimaumbile, si wa mkataba na maridhiano. Kwa hivyo hata baada ya kifo pia hauwezi kuvunjika. Vilevile tunajielimisha kutokana na aya hii kuwa, mafundisho ya wahyi ndiyo mizani ya kupimia haki na batili katika sheria za kijamii na kifamilia. Kwa hivyo mila na desturi ambazo haziendani na mafundisho ya wahyi inapasa ziwekwe kando.

Darsa yetu ya leo inahatimishwa na aya ya tano ambayo inasema:

دْعُوهُمْ لِآبَائِهِمْ هُوَ أَقْسَطُ عِندَ اللَّـهِ ۚ فَإِن لَّمْ تَعْلَمُوا آبَاءَهُمْ فَإِخْوَانُكُمْ فِي الدِّينِ وَمَوَالِيكُمْ ۚوَلَيْسَ عَلَيْكُمْ جُنَاحٌ فِيمَا أَخْطَأْتُم بِهِ وَلَـٰكِن مَّا تَعَمَّدَتْ قُلُوبُكُمْ ۚ وَكَانَ اللَّـهُ غَفُورًا رَّحِيمًا

Waiteni kwa baba zao, maana huo ndio uadilifu zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu. Na ikiwa hamwajui baba zao, basi ni ndugu zenu katika Dini, na rafiki zenu. Wala si lawama juu yenu kwa mlivyo kosea. Lakini ipo lawama katika yale ziliyo fanya nyoyo zenu kwa makusudi. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.

Aya hii ya tano ya Suratul Ahzab inaendeleza maudhui ya aya iliyotangulia na kueleza kwamba: Katika miamala ya kifamilia na kijamii, msiamiliane kwa namna ambayo watoto wa kulea wataonekana kama kwamba ni watoto wenu wa kuzaa. Kama mtakuwa mnalijua jina la baba wa mtoto huyo basi mwiteni kwa kumuunganisha na jina la baba yake; la kama hamlijui, basi watambulisheni watoto wenu wa kulea kama ndugu zenu wa kidini au sahibu zenu ili asili ya kila mtu ilindwe; na yeye mtoto mwenyewe wa kulea pamoja na watu wengine wasije wakadhani kuwa yeye ni mtoto wenu halisi.

Kisha aya inazungumzia kaida na kanuni moja kuu kwa kueleza kwamba, ikiwa jambo lolote lile litakuwa limefanywa kwa makosa na bila kukusudia Mwenyezi Mungu analisamehe; lakini kama limefanywa kwa makusudi, aliyelifanya atalipwa kwa kuadhibiwa. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba tuhifadhi uhusiano wa nasaba wa watu na baba zao halisi, wala tusiubadilishe kwa nia na dhamira mbalimbali ikiwemo ya kuwafanya watoto wetu wa kupanga. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, tunapaswa kuamiliana kwa heshima na kiudugu hata na watu ambao baba zao hawajulikani; na hatuna haki ya kuwadunisha na kuwatusi. Aidha aya hii inatuelimisha kuwa baadhi ya wakati nia na kusudio pamoja na uelewa wa mtu kuhusu sheria huwa na athari katika kosa alilofanya na aina ya adhabu anayopewa. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 744 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuonyeshe haki na atupe taufiki ya kuifuata na atuonyeshe batili na atuwezeshe kuiepuka. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.