Sep 06, 2017 02:27 UTC

Sura ya Al-Ahzab, aya ya 6-8 (Darsa ya 745)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 745 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 33 ya Ahzab. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya sita ambayo inasema:

النَّبِيُّ أَوْلَىٰ بِالْمُؤْمِنِينَ مِنْ أَنفُسِهِمْ ۖ وَأَزْوَاجُهُ أُمَّهَاتُهُمْ ۗ وَأُولُو الْأَرْحَامِ بَعْضُهُمْ أَوْلَىٰ بِبَعْضٍ فِي كِتَابِ اللَّـهِ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ وَالْمُهَاجِرِينَ إِلَّا أَن تَفْعَلُوا إِلَىٰ أَوْلِيَائِكُم مَّعْرُوفًا ۚ كَانَ ذَٰلِكَ فِي الْكِتَابِ مَسْطُورًا

Nabii ni aula zaidi kwa Waumini kuliko nafsi zao. Na wake zake ni mama zao. Na ndugu wa kuzaliwa ni aula wao kwa wao katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu kuliko Waumini wengine na Muhajirina. Ila muwe mnawafanyia wema marafiki zenu. Hayo yamekwisha andikwa Kitabuni.

Katika darsa iliyopita tulisoma aya iliyoeleza kuwa kwa mujibu wa hukumu ya Allah, haijuzu kwa mtoto wa kulea na kupanga kurtihiana na mtu aliyemfanya kuwa mwanawe na kwamba urithi unawahusu baba na mtoto wake halisi wa kuzaa si aliyemfanya kuwa mwanawe. Baada ya maelezo hayo aya tuliyosoma inasema, hata Mtume pia ambaye ana wilayat ya kuwatawalia waumini mambo yao na ana hukumu ya kuwa baba kwa umma wake, pamoja na wake zake ambao wana hukumu ya kuwa mama wa Waislamu, nao pia hawawarithi Waislamu, wala hakuna Muislamu anayeweza kuwarithi wao. Inapasa kukumbusha hapa kuwa, mjini Madina, Bwana Mtume Muhammad SAW alifungisha ahadi ya udugu baina ya Muhajirina na Ansar na kila mmoja miongoni mwa Waislamu wa Madina Ansar akawa na ndugu yake katika Waislamu waliotoka Makka, yaani Muhajirina. Pamoja na hayo, katika mfumo wa urithi wa ujamaa wa nasaba ndugu wa dini hawi na nafasi yoyote, na kama atataka kumshirikisha mwenzake kwenye urithi wake anaweza kufanya hivyo kwa njia ya kuacha wasia kwamba, wema fulani atendewe ndugu yake wa kidini. Japokuwa maudhui ya aya hii, kwa kuzingatia aya za kabla yake, inahusu urithi lakini sehemu ya kwanza ya maelezo ya aya inataja hukumu mutlaki ya jambo. Yaani Bwana Mtume Muhammad SAW ana kipaumbele katika mambo yote ya waumini; na mamlaka yote ambayo mtu anayo juu ya nafsi yake katika mambo yake, Bwana Mtume ndiye mwenye mamlaka ya juu zaidi katika mambo yote ya kila muumini. Kwa hivyo waumini wanatakiwa watangulize na kuyapa kipaumbele maoni ya mtukufu huyo badala ya maoni yao, na wawe watiifu kwake. Aya ya 36 pia ya sura hii hii ya Ahzab inatilia mkazo suala hili, kwamba kila pale Mwenyezi Mungu na Mtume wake wanapotoa hukumu ya jambo, mtu muumini huwa hana hiyari na mamlaka juu ya jambo hilo.

Ni wazi kwamba Bwana Mtume Muhammad SAW ni mja safi na maasumu; na hafikirii isipokuwa lile lenye kheri na maslaha kwa mtu na jamii; kwa hivyo hawezi kutaka jambo kwa ajili ya maslahi yake binafsi au familia yake au kulitaka jambo hilo kutokana na matamanio, hawaa na utashi wa nafsi yake. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba Bwana Mtume ana wilayat na mamlaka ya kutawalia mambo ya waumini wote; na hukumu yake ina taathira katika masuala yote ya binafsi, ya kifamilia na ya kijamii ya mtu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa ni lazima kuwaheshimu na kuwastahi wake wa Bwana Mtume SAW wala haijuzu kusema neno au kufanya kitendo ambacho kwa namna fulani kitatafsirika kuwa ni kuwavunjia heshima. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba katika utamaduni wa Kiislamu ujamaa na nasaba vimezingatiwa na kupewa umuhimu kwa ajili ya kuufanya mfumo wa familia uwe imara.

Darsa yetu ya leo inahatimishwa na aya ya saba na nane ambazo zinasema:

وَإِذْ أَخَذْنَا مِنَ النَّبِيِّينَ مِيثَاقَهُمْ وَمِنكَ وَمِن نُّوحٍ وَإِبْرَاهِيمَ وَمُوسَىٰ وَعِيسَى ابْنِ مَرْيَمَ ۖ وَأَخَذْنَا مِنْهُم مِّيثَاقًا غَلِيظًا

Na tulipo chukua ahadi kwa Manabii na kwako wewe, na kwa Nuhu na Ibrahim na Isa mwana wa Mariamu, na tulichukua kwao ahadi ngumu,

 لِّيَسْأَلَ الصَّادِقِينَ عَن صِدْقِهِمْ ۚ وَأَعَدَّ لِلْكَافِرِينَ عَذَابًا أَلِيمًا

Ili (Mwenyezi Mungu) awaulize wakweli juu ya ukweli wao. Na amewaandalia makafiri adhabu chungu.

Aya iliyotangulia ilizungumzia wilayat na mamlaka ya Bwana Mtume Muhammad SAW juu ya waumini. Aya hizi tulizosoma zinaashiria mas-ulia mazito ya Bwana Mtume SAW na Mitume wengine wote waliotangulia na kueleza kwamba mkabala na haki ambayo Mwenyezi Mungu amewajaalia Mitume amewapa pia majukumu mazito na kuchukua ahadi kwao kwamba hawatoacha kufanya kila lililo katika uwezo wao katika kuwafikishia watu wito wake wa wahyi na kuwaelekeza kwenye uongofu na kwamba watajitahidi kuwalingania watu Tauhidi hata kama itabidi kujitolea mhanga roho zao. Aya hizi tulizosoma zimewataja Mitume wakubwa watano wa Mwenyezi Mungu ambao wanajulikana kama Ulul-azm, ambapo baada ya Bwana Mtume Muhammad SAW yamefuatia majina ya Manabii Nuhu, Ibrahim, Musa na Isa (as). Kisha aya zinaendelea kueleza kwamba watu huwa wanagawika makundi mawili wanapofikiwa na wito wa Mitume; wasadikishaji na wakanushaji! Wasadikishaji ni wale walio wakweli katika kudai kwao kuwa wameamini. Yaani kile wanachokitamka kwa ndimi zao wanakithibitisha pia katika matendo yao; na si kudai kwa ulimi kuwa wameamini lakini katika amali zao haionekani athari yoyote ya kutii na kutekeleza maamrisho ya Mwenyezi Mungu. Siku ya Kiyama, Allah SW atawauliza watu wa makundi yote hayo mawili na kuwalipa malipo mema ya thawabu au mabaya ya adhabu kwa mujibu wa fikra, kauli na vitendo vyao. Katika aya ya 23 na 24 za sura hii hii ya Ahzab pia Mwenyezi Mungu Mtukufu anaashiria waumini wa kweli na kueleza kwamba wale wanaosadikisha ahadi ya Mwenyezi Mungu na wakasimama imara katika kutekeleza ahadi waliyofungiana na Mola wao katika kuilinda dini yake hao ni wasadikishaji, na watapata malipo mema kwa sababu ya ukweli na usadikishaji wao. Hao ni watu ambao wako tayari kujitolea roho zao, mali zao na kila kitu kwa ajili ya kuilinda dini ya Mwenyezi Mungu na wamethibitisha katika wakati wa tabu, matatizo na misukosuko ukweli wa kudai kwao kuwa wameamini. Tab'an kuna nukta ya kuvutia iliyojificha katika aya hizi, nayo ni kwamba Siku ya Kiyama Allah SW ataupima ukweli wa wasadikishaji haki, kwa maana kwamba kufanya amali tu hakutoshi bali lazima uthibitike pia ukweli wa nia na kuwepo ikhlasi katika sababu ya kutendea amali njema. Kwani si hasha watu wakajitokeza hata kwenye medani za jihadi lakini nia zao zikawa hazina ikhlasi, yaani hawakufanya hivyo lillah na kwa ajili ya Mwenyezi Mungu tu; bali mbali na kutekeleza wajibu wa kidini wakawa wanajitafutia pia mali na umaarufu. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kuijua historia ya Mitume na ya kaumu zilizopita ni jambo la lazima kwa waumini ili wapate uelewa juu ya yaliyozipata kaumu hizo na kuweza kufuata njia sahihi. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa Mwenyezi Mungu ameiwekea kila haki na wajibu wake pia. Kadiri cheo na hadhi ya mtu inapokuwa ya juu akawa na mamlaka makubwa zaidi ndivyo mas-ulia na majukumu yake yanavyokuwa makubwa na mazito zaidi. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba ukweli katika maneno na matendo ni jambo la lazima katika imani mpaka imefikia hadi Mwenyezi Mungu kutumia neno wasadikishaji badala ya waumini, kama tulivyoona katika aya tulizosoma. Wa aidha aya hizi zinatutaka tuelewe kuwa Siku ya Kiyama Allah SW atazipima amali za watu kulingana na nia zao; hivyo mbali na dhahiri ya amali, batini yake pia itazingatiwa. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 745 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah azifanye zenye ikhlasi nia zetu, kauli zetu na matendo yetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.