Sep 06, 2017 02:37 UTC

Sura ya Al-Ahzab, aya ya 13-17 (Darsa ya 747)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 747 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 33 ya Ahzab. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 13 ambayo inasema:

وَإِذْ قَالَت طَّائِفَةٌ مِّنْهُمْ يَا أَهْلَ يَثْرِبَ لَا مُقَامَ لَكُمْ فَارْجِعُوا ۚ وَيَسْتَأْذِنُ فَرِيقٌ مِّنْهُمُ النَّبِيَّ يَقُولُونَ إِنَّ بُيُوتَنَا عَوْرَةٌ وَمَا هِيَ بِعَوْرَةٍ ۖ إِن يُرِيدُونَ إِلَّا فِرَارًا 

Na kundi moja miongoni mwao lilipo sema: Enyi watu wa Yathrib! Hapana pa kukaa nyinyi! Basi rudini. Na kundi jingine miongoni mwao likaomba ruhusa kwa Mtume kwa kusema: Hakika nyumba zetu ni tupu. Wala hazikuwa tupu; hawakutaka ila kukimbia tu.

Katika aya tulizosoma katika darsa iliyopita tulizungumzia kuanza kwa matukio ya vita vya Ahzab. Tukasema kwamba wanafiki na wale wenye maradhi ndani ya nyoyo zao walikuwa wakiwavunja moyo watu kwa kuwaambia: Mtume ametudanganya na wala sisi hatutoshinda vita hivi. Aya tuliyosoma inaendeleza maudhui hiyo kwa kueleza kwamba kundi jengine la wanafiki haohao waliwaambia watu waliokuwa wametoka nje ya mji wa Madina kwenda kukabiliana na adui kwamba: Hapa si mahala pa kuwepo nyinyi; hakuna mnachoweza kufanya. Rudini majumbani kwenu mkazilinde nyumba zenu, wake na watoto wenu. Baadhi yao waliamua kumwendea Bwana Mtume, na kwa kutoa visingizio hivi na vile wakamtaka awaruhusu warudi Madina ilhali tokea awali walikuwa na nia ya kukwepa kwenda vitani. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba kueneza uvumi na kuwavunja moyo watu ni miongoni mwa mipango inayotekelezwa na wanafiki. Waumini wanatakiwa wajihadhari na watu wa aina hii pamoja na mienendo yao potofu wanayoeneza katika jamii. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa wakati wa vita, yeye mwenyewe Mtume wa Allah alikuwa ndo jemadari na kamanda mkuu wa jeshi. Wakati wa hatari, mtukufu huyo alikuwa bega kwa bega na watu na hakuwa akiwaacha peke yao.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 14 na 15 ambazo zinasema:

وَلَوْ دُخِلَتْ عَلَيْهِم مِّنْ أَقْطَارِهَا ثُمَّ سُئِلُوا الْفِتْنَةَ لَآتَوْهَا وَمَا تَلَبَّثُوا بِهَا إِلَّا يَسِيرًا

Na lau wangeli ingiliwa kwa pande zote, kisha wakatakiwa kufanya khiana, wangeli fanya, na wasingeli sita ila kidogo tu.

وَلَقَدْ كَانُوا عَاهَدُوا اللَّـهَ مِن قَبْلُ لَا يُوَلُّونَ الْأَدْبَارَ ۚوَكَانَ عَهْدُ اللَّـهِ مَسْئُولًا

Na hakika walikwisha muahidi Mwenyezi Mungu kabla yake kwamba hawatageuza migongo yao. Na ahadi ya Mwenyezi Mungu ni yenye kuulizwa.

Aya hizi zinaendeleza maudhui ya aya iliyotangulia na kueleza kwamba, watu hawa, ambao leo hii wanakwepa kwenda kukabiliana na adui na hawako tayari kufikwa na hatari, wanafanya hivyo kwa sababu imani yao juu ya Allah ni dhaifu na ya kulegalega. Kwani kama adui ataingia kwenye mji wa Madina na akawataka warudi tena kwenye shirki na ukafiri watakubali haraka kufanya hivyo na kuiacha imani yao. Kama ambavyo wakati wa kumbai Mtume wa Allah, walitoa ahadi kuwa watamsaidia mtukufu huyo na Waislamu kwa jumla kukabiliana na maadui na wala hawatomkimbia adui, lakini hawakufungamana na ahadi na mkataba huo bali waliukiuka licha ya kujua kwamba watakuja kuulizwa kuhusu jambo hilo. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba baadhi ya watu wenye imani dhaifu walioko katika jamii ya Kiislamu huwa tayari kuiacha njia ya haki na kuungana na adui. Watu hao huwa wako tayari wanyongeshwe na adui lakini hawako tayari kuwasaidia viongozi wa Kiislamu katika kukabiliana na adui hiyo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, imani ni aina ya ahadi ambayo mtu anawekeana na Mwenyezi Mungu, yenye maana kwamba, mtu atasimama kukabiliana na maadui wa dini hata kama itabidi kuyatoa mhanga maisha yake. Kuivunja ahadi hiyo ni alama ya kutokuwa na imani.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 16 na 17 ambazo zinasema:

قُل لَّن يَنفَعَكُمُ الْفِرَارُ إِن فَرَرْتُم مِّنَ الْمَوْتِ أَوِ الْقَتْلِ وَإِذًا لَّا تُمَتَّعُونَ إِلَّا قَلِيلًا

Sema: Kukimbia hakukufaeni kitu ikiwa mnakimbia mauti au kuuwawa, na hata hivyo hamtastareheshwa ila kidogo tu.

 قُلْ مَن ذَا الَّذِي يَعْصِمُكُم مِّنَ اللَّـهِ إِنْ أَرَادَ بِكُمْ سُوءًا أَوْ أَرَادَ بِكُمْ رَحْمَةً ۚ وَلَا يَجِدُونَ لَهُم مِّن دُونِ اللَّـهِ وَلِيًّا وَلَا نَصِيرًا

Sema: Ni nani wa kukulindeni na Mwenyezi Mungu pindi akikutakieni uovu, au akikutakieni rehema? Wala hawatapata mlinzi wala msaidizi asiyekuwa Mwenyezi Mungu.

Katika aya hizi Mwenyezi Mungu anawahutubu watu wanaokimbia kwenda vitani ili kukwepa kupambana na adui kuwa: Msidhani kama mtakimbia vitani kwa kuhofia kuuliwa kuna faida yoyote ile mtayopata, kwa sababu hamutostarehe katika dunia hii isipokuwa kwa siku chache tu lakini mtakuwa mumejinunulia adhabu ya milele ya Moto na kupatwa na ghadhabu za Mola. Isitoshe, mauti hayapatikani kwenye medani ya vita tu. Kikawaida na kimaumbile kila siku kuna watu wanakufa na kuondoka duniani. Kuna hakikisho gani kuwa, kama mtakimbia vitani hamutofikwa na mauti kwa sababu za kimaumbile au za ajali na matukio mbalimbali? Mnadhani Mwenyezi Mungu hawezi kuchukua roho zenu nje ya medani ya vita? Au nyinyi mnapo pa kukimbilia, pa kukupeni hifadhi na ngao ya kukabiliana na irada ya Allah na kukuwezesheni kutoka nje ya mipaka ya irada ya Mola? Au ghairi yake Yeye Allah mnaye mlinzi wa kukusaidieni kukabiliana na Yeye Mola? Kwa hivyo badala ya kukimbia na kukwepa kubariziana na adui jitokezeni kwenye medani ya mapambano, mpigane na mpambane kwa izza na utukufu mkijua kwamba kama mtakufa shahidi katika njia hiyo marejeo yenu ni kwake Yeye Allah. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba mauti ndio hatima na mwisho wetu sote na hakuna njia ya kuyaepuka. Iwe ni leo au kesho, lakini hatuna budi kuondoka duniani. Basi ni heri iliyoje kama mauti yatatukuta katika njia ya Mwenyezi Mungu na kwa ajili ya kutekeleza maamrisho yake Mola. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa tujihadhari tusije tukaiuza saada ya milele kwa dunia yenye mwisho na starehe zake za kupita. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba ulimwengu mzima wa maumbile unaendeshwa kwa tadbiri na irada ya Allah. Matamu na machungu na ushindi na kushindwa yote hayo yanafanyika kutokana na hekima ya Mola. Saada na kufuzu kwa mwanadamu pia kunapatikana kwa kufungamana na kufuata njia ya mafundisho na maamrisho ya Mwenyezi Mungu SW. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 747 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuonyeshe haki na atupe taufiki ya kuifuata na atuonyeshe batili na atuwezeshe kuipeuka. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.