Sep 06, 2017 02:39 UTC

Sura ya Al-Ahzab, aya ya 18-21 (Darsa ya 748)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 748 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 33 ya Ahzab. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 18 na 19 ambazo zinasema:

قَدْ يَعْلَمُ اللَّـهُ الْمُعَوِّقِينَ مِنكُمْ وَالْقَائِلِينَ لِإِخْوَانِهِمْ هَلُمَّ إِلَيْنَا ۖ وَلَا يَأْتُونَ الْبَأْسَ إِلَّا قَلِيلًا

Kwa hakika Mwenyezi Mungu anawajua miongoni mwenu wanao zuilia, na wanao waambia ndugu zao: Njooni kwetu! Wala hawaingii vitani ila kidogo tu.

أَشِحَّةً عَلَيْكُمْ ۖ فَإِذَا جَاءَ الْخَوْفُ رَأَيْتَهُمْ يَنظُرُونَ إِلَيْكَ تَدُورُ أَعْيُنُهُمْ كَالَّذِي يُغْشَىٰ عَلَيْهِ مِنَ الْمَوْتِ ۖ فَإِذَا ذَهَبَ الْخَوْفُ سَلَقُوكُم بِأَلْسِنَةٍ حِدَادٍ أَشِحَّةً عَلَى الْخَيْرِ ۚ أُولَـٰئِكَ لَمْ يُؤْمِنُوا فَأَحْبَطَ اللَّـهُ أَعْمَالَهُمْ ۚ وَكَانَ ذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرًا

Wana choyo juu yenu. Ikija khofu utawaona wanakutazama na macho yao yanazunguka, kama yule ambaye aliye zimia kwa kukaribia mauti. Na khofu ikiondoka wanakuudhini kwa ndimi kali, nao ni mabakhili kwa kila la kheri. Hao hawakuamini, basi Mwenyezi Mungu amezibat'ilisha amali zao. Na hayo kwa Mwenyezi Mungu ni mepesi.

Katika darsa iliyopita tuliashiria nafasi ya wanafiki na kuhusika kwao katika kuwavunja moyo Waislamu katika vita vya Ahzab. Aya hizi tulizosoma zinaendeleza maudhui hiyo na kueleza kwamba: Kundi moja miongoni mwa wanafiki hao walifanya kila hila ili kuwazuia watu wasijitokeze kukabiliana na adui na wakawa wanawaambia: Jiondoeni vitani kama tulivyojiondoa sisi na unganeni nasi katika hilo. Watu hao walikuwa na ubakhili; si wa kujitolea mhanga roho zao tu katika medani ya Jihadi, lakini walikuwa hivyo pia hata katika kutoa mali zao kuwasaidia wapiganaji na familia zao. Imani zao juu ya Mwenyezi Mungu zilikuwa dhaifu na legelege, kiasi kwamba wakati wa hatari walikuwa wakitetemeka na kujawa na hofu utadhani wanataka kukata roho hata kabla ya kushambuliwa na kuuliwa na adui. Lakini kama Waislamu wanapata ushindi, wao pia hujihisi wana mchango katika ushindi huo na kuwa na pupa na uchu katika kukusanya ngawira za vita. Na huzungumza kwa ukali mithili ya mdai mwenye haki, wakitaka wapewe fungu lao katika ngawira hizo. Bila ya shaka maelezo yanayotolewa na Qur'ani kuhusu sifa za wanafiki wa zama za Bwana Mtume Muhammad SAW hayahusiani na zama hizo tu. Katika kila mahala na zama, watu wa aina hiyo hupatikana miongoni mwa Waislamu, ambapo wakati wa hatari hukimbia, na wakati wa neema na raha hukimbilia mali na madaraka na kujiona wao ndio wa mbele kuliko watu wengine. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba katika kukabiliana na adui tujihadhari na watu wa ndani wenye imani dhaifu, ambao hawatoroki kwenye medani ya vita wao wenyewe tu lakini husema maneno ya kuvunja moyo ili kuwazuia wenzao pia wasiende kwenye medani ya Jihadi. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa wakati wa hatari na misukosuko, wanafiki huwa na ubakhili wa kuwasaidia wapiganaji, na wa wao wenyewe kukwepa kwenda vitani; lakini pale hatari inapoondoka, huwa na pupa na uchu wa kukusanya mali na ngawira. Hizo ni katika alama za unafiki. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba kuwa dhaifu na kuwa na woga mbele ya adui wakati wa vita na misukosuko na kuwa wakali katika kuamiliana mtu na Waislamu wenzake na kujihisi ana haki kwao ni sifa na alama nyengine ya watu wanafiki.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 20 ambayo inasema:

يَحْسَبُونَ الْأَحْزَابَ لَمْ يَذْهَبُوا ۖ وَإِن يَأْتِ الْأَحْزَابُ يَوَدُّوا لَوْ أَنَّهُم بَادُونَ فِي الْأَعْرَابِ يَسْأَلُونَ عَنْ أَنبَائِكُمْ ۖ وَلَوْ كَانُوا فِيكُم مَّا قَاتَلُوا إِلَّا قَلِيلًا

Wanadhani yale makundi ya maadui hayajaondoka. Na yakija hayo makundi watatamani laiti wao wako majangwani pamoja na mabedui, wakiuliza khabari zenu. Na lau wakiwa pamoja nanyi hawapigani isipokuwa kidogo tu.

Aya hii inadhihirisha upeo wa woga na udhaifu wa wanafiki na kueleza kwamba: Licha ya jeshi la adui kutawanyika na mji wa Madina ukawa haukabiliwi tena na hatari yoyote lakini wanafiki wangali wanadhani kuwa maadui wangaliko kandokando ya mji huo. Kwa hivyo wanahisi wanakabiliwa na hatari; na kila sauti ya farasi na ngamia wanayoisikia wanafikiri ni wapiganaji wa jeshi la adui wanawajia wao. Woga ulikuwa umewavaa kiasi cha kutaka kukimbilia majangwani wakaishi pamoja na mabedui, ili kwa mawazo yao watakuwa wameepukana na hatari; ambapo katika hali hiyo watakuwa wanaulizia kwa wasafiri wapita njia habari za yanayojiri mjini ili pale amani kamili itakaporejea warudi tena huko. Kisha aya zinawahutubu waumini kuwa: Bila ya shaka kama watabakia ndani ya mji pia, wengi wao hawatokuja kukusaidieni na wala hawatojitokeza kupambana na adui. Kwa hivyo msihofie kuondoka kwao wala msifurahie kubaki kwao. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, wanafiki na watu wenye imani dhaifu siku zote huwadhania maadui kuwa wana nguvu zaidi kuliko Waislamu. Kwa imani yao, hatima ya mpambano wowote utakaotokea ni ushindi wa maadui dhidi ya Waislamu; na wao hupanga mipango na mahesabu yao kulingana na dhana hiyo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, woga na kulegea mbele ya adui humfanya mtu akimbie na akwepe kukabiliana naye, ilhali akili na dini inahukumu kuwa mtu anapaswa kusimama imara kukabiliana na adui na kutoonyesha udhaifu na ulegevu.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 21 ambayo inasema:

 لَّقَدْ كَانَ لَكُمْ فِي رَسُولِ اللَّـهِ أُسْوَةٌ حَسَنَةٌ لِّمَن كَانَ يَرْجُو اللَّـهَ وَالْيَوْمَ الْآخِرَ وَذَكَرَ اللَّـهَ كَثِيرًا

Hakika nyinyi mnayo ruwaza njema kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa anaye mtaraji Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, na akamkumbuka Mwenyezi Mungu sana.

Aya hii inaendeleza maudhui ya aya zilizotangulia zilizozungumzia sifa za wanafiki na watu wenye imani dhaifu na kueleza kwamba: Pamoja na hayo, watu wenye imani thabiti, badala ya kushughulishwa na maneno na mwenendo wa wanafiki na kutegea katika kutekeleza wajibu na majukumu yao, wao huyazingatia na kuyapa uzito maneno ya Mtume. Waislamu hao, kama alivyo mtukufu huyo wako thabiti na wanasimama imara mbele ya maadui na wala hawategei au kuzembea katika kuulinda mji wa Madina na Waislamu wenzao.

Kwa mujibu wa mapokeo ya historia, ili kuulinda mji wa Madina, Bwana Mtume Muhammad SAW aliamuru kuchimbwa handaki kandokando ya mji katika kila sehemu ambayo kulikuwa na uwezekano wa adui kujipenyeza. Yeye mwenyewe Bwana Mtume, kama walivyokuwa Waislamu wengine, alibeba sururu na pauro na kushiriki katika uchimbaji mahandaki. Sambamba na juhudi hizo alizofanya, Bwana Mtume Muhammad SAW alikuwa akihuisha pia dhikri na utajo wa Allah ndani ya nyoyo za Waislamu, huku akiwapa ahadi ya Mola ya kupata ushindi. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba wakati wa vita vya Jihadi, Bwana Mtume SAW alikuwa akivaa nguo za vita na kubeba jukumu la ujemedari wa kuliongoza jeshi la Waislamu vitani. Dini yake haikutengana na utawala; alikuwa akiwatakia watu saada na amani ya duniani na pia saada ya milele ya huko akhera. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa Bwana Mtume SAW alikuwa akiishi maisha ya kawaida kama walivyo watu wengine; kwa hivyo anaweza kuwa kigezo na mfano wa kuigwa kivitendo na waumini wote. Yeye alikuwa kiumbe wa ardhini na kigezo cha kuigwa na kufuatwa na watu wa dunia hii. Katika medani za vita pia hakuwa akifanya mambo kulingana na elimu ya ghaibu, na akizingatia na kuchunga misingi na kanuni za vita. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba, kama Waislamu duniani wangemfanya Bwana Mtume Muhammad SAW kuwa ruwaza na mfano wao wa kuiga na kufuata, leo hii wasingekuwa dhalili na dhaifu namna hii mbele ya maadui zao na katu wasingekubali wanyogeshwe na maadui. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 748 ya Quráni imefikia tamati. Tunamwomba Allah azitakase nyoyo zetu na kila maradhi ya kinafsi, yakiwemo ya unafiki, kiburi, hasadi na ubakhili. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.