Sura ya Al-Ahzab, aya ya 22-25 (Darsa ya 749)
Sura ya Al-Ahzab, aya ya 22-25 (Darsa ya 749)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 749 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 33 ya Ahzab. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 22 ambayo inasema:
وَلَمَّا رَأَى الْمُؤْمِنُونَ الْأَحْزَابَ قَالُوا هَـٰذَا مَا وَعَدَنَا اللَّـهُ وَرَسُولُهُ وَصَدَقَ اللَّـهُ وَرَسُولُهُ ۚ وَمَا زَادَهُمْ إِلَّا إِيمَانًا وَتَسْلِيمًا
Na Waumini walipo yaona makundi, walisema: Haya ndiyo aliyo tuahidi Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na Mwenyezi Mungu na Mtume wake wamesema kweli. Na hayo hayakuwazidisha ila Imani na ut'iifu.
Katika darsa iliyopita tulizungumzia mwenendo wa wanafiki katika vita vya Ahzab. Aya tuliyosoma inasema: Waumini wa kweli ambao wanamwamni Mwenyezi Mungu na Mtume wake, walipokabiliana na jeshi la adui walisema: Hapo kabla, Mwenyezi Mungu alikuwa ameshatupa habari katika aya za Quráni, kwamba kama zilivyokuwa umma zilizotangulia, nanyi pia mtafikwa na misukosuko na hujuma za maadui. Mtume wa Allah pia alikuwa ameshasema hapo kabla kwamba makabila mbalimbali ya Waarabu na maadui zenu wataungana pamoja kwa lengo la kukuangamizeni nyinyi. Kwa hivyo wakati walipoiona hali na mazingira yale, badala ya kugeuka nyuma na kukimbia kama walivyofanya wanafiki walisimama imara pasina kutetereka, wakamkabili adui na kuonyesha kuwa wanatii amri ya Mwenyezi Mungu na Mtume. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba muumini anajua kwamba adui dhalimu hawezi kumwacha kama alivyo; kwa hivyo huwa anajiandaa na kujiweka tayari muda wote kwa ajili ya makabiliano na adui. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa licha ya hitilafu na tofauti zote ambazo makafiri wanaweza kuwa nazo baina yao, lakini katika suala la kuuangamiza Uislamu na Waislamu huungana na kuwa kitu kimoja na hutumia nguvu na suhula zao zote kwa ajili ya kufikia lengo hilo. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba hata kama waumini watakuwa wachache, lakini katika kukabiliana na maadui hata kama watakuwa wengi, husimama imara na kuzisalimisha nafsi zao kwa Allah, si kwa maadui.
Tunaiendeleza darsa yetu hii kwa aya ya 23 ambayo inasema:
مِّنَ الْمُؤْمِنِينَ رِجَالٌ صَدَقُوا مَا عَاهَدُوا اللَّـهَ عَلَيْهِ ۖ فَمِنْهُم مَّن قَضَىٰ نَحْبَهُ وَمِنْهُم مَّن يَنتَظِرُ ۖ وَمَا بَدَّلُوا تَبْدِيلًا
Miongoni mwa Waumini wapo watu walio timiza waliyo ahidiana na Mwenyezi Mungu. Baadhi yao wamekwisha kufa, na baadhi wanangojea, wala hawakubadilisha (ahadi yao) hata kidogo.
Aya hii inaendeleza maudhui ya aya iliyotangulia iliyozungumzia istiqama na kusimama imara waumini wa kweli na kueleza kwamba: Waumini wa kweli wamefunga ahadi na Mwenyezi Mungu kuwa hawatozembea katika kuinusuru dini yake na watasimama kufanya hivyo hata ikibidi kuyatoa mhanga maisha yao. Kwa hivyo baadhi yao waliuawa shahidi katika vita vya Badr na Uhud. Wengine miongoni mwao wanangojea wapate fursa ili watimize ahadi yao ya kujitolea mhanga roho zao katika njia ya Allah; nao hawajayumba wala kulegalega kiimani katika kutekeleza ahadi yao hiyo. Ni kinyume na watu wenye imani dhaifu, ambao hata kama watakwenda vitani hufurahi wanaporudi salama. Na kama vitatokea vita vingine, basi huwa hawako tayari kwenda tena kwenye medani ya mapambano. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba Waislamu hawako daraja moja kiimani bali wana daraja na viwango tofauti vya imani. Miongoni mwao wanataka waishi maisha ya raha na utulivu na miongoni mwao wanasubiri kwa hamu kufa shahidi katika njia ya Mwenyezi Mungu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa kujiweka tayari kuilinda na kuihami dini hata kwa kuyatoa mhanga maisha ni alama ya imani ya kweli na utimizaji ahadi ya muumini kwa Mola wake. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba muumini wa kweli huwa hadhofu na kurudi nyuma anapowaona wenzake na wapendwa wake wanakufa shahidi na wala hakimbii katika medani ya jihadi, bali yeye mwenyewe pia anajiweka tayari kuyakabili mauti ya kufa shahidi.
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 24 na 25 ambazo zinasema:
لِّيَجْزِيَ اللَّـهُ الصَّادِقِينَ بِصِدْقِهِمْ وَيُعَذِّبَ الْمُنَافِقِينَ إِن شَاءَ أَوْ يَتُوبَ عَلَيْهِمْ ۚ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ غَفُورًا رَّحِيمًا
Ili Mwenyezi Mungu awalipe wakweli kwa sababu ya ukweli wao, na awaadhibu wanaafiki pindi akitaka, au apokee toba yao. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.
وَرَدَّ اللَّـهُ الَّذِينَ كَفَرُوا بِغَيْظِهِمْ لَمْ يَنَالُوا خَيْرًا ۚ وَكَفَى اللَّـهُ الْمُؤْمِنِينَ الْقِتَالَ ۚوَكَانَ اللَّـهُ قَوِيًّا عَزِيزًا
Na Mwenyezi Mungu aliwarudisha nyuma makafiri juu ya ghadhabu yao; hawakupata kheri yoyote. Na Mwenyezi Mungu amewatosheleza Waumini katika vita. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu na uweza.
Aya hizi zinazungumzia matokeo ya vita vya Ahzab kwa kueleza kwamba: Waumini wa kweli ambao walivaa mavazi ya vita kwa ajili ya kukabiliana na adui na wakawa bega kwa bega na Mtume ili kujitoa mhanga katika njia ya Uislamu watapata malipo yao ya thawabu kwa Mwenyezi Mungu japokuwa vita baina pande mbili havikutokea na waumini hawakupigana wala hawakuuawa shahidi. Lakini wanafiki, ambao wao wenyewe walikuwa na imani zinazoyumba na wakawa sababu pia ya kuwayumbisha wengine, wao wanastahili adhabu ya Mwenyezi Mungu, isipokuwa kama Allah SW atawasamehe madhambi yao kwa kutubia kwao au kwa rehma zake. Washirikina na makafiri wengine, ambao kwa njama yao hiyo waliyokuwa wameipanga, walidhani kama wataweza kuuangamiza Uislamu na kummaliza Bwana Mtume na masahaba zake, walilazimika kurudi makwao pasina kupata ushindi wala ngawira za vita. Katika tukio la vita vya Ahzab Mwenyezi Mungu Mtukufu aliwapa funzo na somo Waislamu kuwa wasimhofu adui katu; na wao maadui wa Allah watambue kwamba njama zao hazina athari yoyote mbele ya tadbiri ya Mola na wala haziwezi kushinda nguvu zake. Kwa hivyo maadui waliokuwa wameungana pamoja na kwenda kwenye medani ya vita kwa nia ya kuutokomeza Uislamu walirudi makwao wakiwa wamejawa na hasira na huzuni huku wakishindwa kuyafikia matamanio na matarajio waliyokuwa nayo. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba ukweli na usadikishaji usiwe wa maneno matupu bali tunapaswa kimatendo pia kuwa wakweli katika ahadi zetu kwa Mwenyezi Mungu na wala tusilegee na kuzembea katika kuinusuru dini ya Mwenyezi Mungu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa rehma za Allah haziko mbali na mtu yeyote. Hata kwa wanafiki wavunjaji ahadi pia kuna matumaini ya kusamehewa kwa kutubia au kwa irada ya hekima yake Mola. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba katika masuala tofauti ya maisha, tusitosheke na mahesabu ya kimaada tu na wala tusighafilike na msaada wa ghaibu na wa vitu vilivyo nje ya mahesabu ya kimaada. Wapenzi wasikilizaji, darsa yetu ya leo imefikia tamati. Tunamwomba Allah atujaalie kuwa miongoni mwa waja wake wenye imani thabiti na ya kweli, wanaosadikisha imani zao kwa ndimi zao na kwa matendo yao. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.